Umebaki mnara tu


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 25 May 2011

Printer-friendly version

UMEBAKIA mnara
Mnara tu!

Wanaita kumbukumbu
Paleee! Igoma;
Mjini Mwanza.

Hakuna zaidi.

Hakuna kingine.

Nakwambia hakuna!

Zaidi ya 1,000 walikufa
Ndani ya mv. Bukoba
Na leo kuna mnara tu
Hakuna zaidi.

Wako wapi
Wale waliosababisha
Vifo vya watoto,
Wanafunzi
Walokutwa
Wamegandana;
Vijana, watu wazima,
Vikongwe?

Wako wapi
Waliojaza mtu juu ya mtu
Mzigo juu ya mzigo?

Hatujawaona
Hatujawasikia;
Ndweo kama kawa:
Serikali
Mkono mrefu!

Wako wapi
Wale waloshindwa
Meli kukagua
Walioipapasapapasa
Wakalipwa;
Wakala, wakanywa
Wakapiga mbwewe
Wakasinzia
Na kuangamiza umati?

Umebaki mnara
Mnara tu!

Paleee! Igoma
Mjini Mwanza

Ilikuwa 21 Mei
Ilikuwa mwaka 1996
Ilikuwa asubuhi
Ilikuwa kilometa nane
Kabla ya kuingia
Mwanza bandarini.

mv Bukoba
Ile meli iliyotoka Bukoba
Ilipinduka;
Ikagota topeni
Wajinga wakaamua
Haijazama vema;
Tundu juu wakatoboa
Hewa ikaingia
Lote likadidimia.

Hauonekani tena
mv Bukoba
Imezama
Imepotea
Imekwenda na wetu
Wapendwa
Tumebaki na mnara
Paleee! Igoma.

Walikufa
Walifia majini
Wakazikwa majini
Wakapotea
Hawakuonekana tena
Hawapo;
Kuna mnara tu
Paleee! Igoma
Mjini Mwanza.

Vilio
Simanzi
Waliozika wachache
Watawala wakaja
Wakasema wanalia
Wakafuta nyuso
Kwa leso zing’arazo
Wakafuta macho
Eti tunalia pamoja

Wasikilize!

Ndimi zao nyororo
Hazina hata kwikwi
Wanaporomosha
Rambirambi,
Wanaporomosha ahadi,
Mojamoja, mojamoja.

Wale mabingwa
Mabingwa wa kusema
Mabingwa wa ahadi
Mabingwa wa usanii.

Tunawapa pole!

Walisema kwa sauti
Tunalia pamoja!

Walisema kwa sauti
Zile za kupindapinda.

Tutawafariji
Kwa gharama yoyote ile.

Tutafaya uchunguzi
Tutatafuta chanzo
Kile cha msiba mkubwa
Tutakamata wahusika
Sheria itawatafuna;
Walitamka kwa
Zile sauti za kisiasanii
Waliaminiwa.

Bale leo
Miaka 15 yapita
Umebaki mnara
Paleee! Igoma,
Mwanza mjini
Mnara tu!

Tutanunua meli
Kubwa kuliko ile
Kuliko mv Bukoba;
Walisikika wakiimba
Wakijirudiarudia
Hadharani, mikutanoni
Serikalini na bungeni
Walijiapiza.

Leo, miaka 15
Hakuna meli
Hakuna mtoto wake
Hakuna shangazi wake
Hakuna mfano wake
Mfano umetundikwa
Pale juu
Pale kwenye mnara;
Mnara tu
Paleee! Igoma
Mwanza mjini.

Ahadi juu ya ahadi!

Kwenye bajeti
Meli haiingii
Uwanja wa ndege
Matope bin Matope
Ahadi, ahadi
Bukoba, Kagera
Sawa na ahadi;
Ahadi sawa
Na Bukoba
Na Kagera na ahadi!

Umebaki mnara
Katikati ya mawe
Paleee! Igoma;
Kwamba walikufa
Wengi elfu na zaidi
Walobaki wala ahadi
Ahadi, ahadi.

Yesu aweza
Kutangulia kurudi!

0713 614872
0
No votes yet