Umeme kizungumkuti


editor's picture

Na editor - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SERIKALI haijielewi. Inapanga kuipatia nchi umeme wa kutosha na wa uhakika, lakini inachokifanya ni kinyume na mipango yake.

Haitaki kuona ukweli wa tatizo la uhaba wa umeme. Matokeo yake, inachukua hatua ambazo siyo tu ni za kubabaisha, bali pia zinaongeza ukubwa wa tatizo.

Hata juzi ilipoamua kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imethibitisha tu ilivyoshindwa kushughulikia jambo hili zito kwa maslahi ya nchi na watu wake.

Inasikitisha viongozi wakuu wa nchi hawajajiuliza sababu za kushindwa kutimiza ahadi waliyotoa kwenye mkutano wa bajeti bungeni mwaka jana.

Wakati ule, serikali iliahidi kutatua tatizo la uhaba wa umeme na kupigia magoti bunge liidhinishe zaidi ya Sh. 55 bilioni kwa ajili ya hatua za awali.

Zimetumikaje fedha zile? Kwanza zilipatikana? Haya ni maswali ambayo majibu yake yanasubiriwa hapohapo bungeni.

Tatizo kubwa la serikali ni kukataa kuacha ujinga. Laiti viongozi wangeamua kwa dhati ya moyo wao kusema “ujinga basi,” tatizo lingetatuka. Hawataki.

Hivi kwanini hawaiwezeshi TANESCO itekeleze miradi yake ya maendeleo wakati wanajua fika chimbuko la uwezo duni wa shirika hili ni mipango yao ya kulinyonya?

Shirika hili limenyonywa mpaka linakaribia kufilisika. Hata hapo lilipo, wanaendelea kulazimisha kufanya kazi katika mazingira magumu.

Sasa TANESCO haijiwezi. Ina utitiri wa miradi mizuri isiyotekelezeka kwa kukosekana fedha. Badala ya kuamini ukweli na hali halisi, viongozi wanapiga ramli.

Majibu ya ramli yao ni kumsimamisha mkurugenzi mtendaji, Mhandisi William Mhando ambaye wanajua ameongoza shirika kijasiri bali ndani ya matatizo mengi.

Serikali yenyewe imekataa kudhamini shirika ili lipate mkopo benki ya CitiBank ya Uingereza wa Sh. 408.

Sababu ni nini? Shirika linadaiwa madeni makubwa na hivyo kukopeshwa ni sawa na kutosa pipa la maji baharini, hakuna kitakachobadilika.

TANESCO linadaiwa Sh. 320 bilioni na sehemu kubwa ya wadai ni kampuni binafsi za nje zilizoitwa na viongozi wakuu na kupewa mikataba ya ulaji.

Ni mikataba hii inalimaliza shirika. Sasa haliwezi kusimama na wakati wowote nchi itaingia gizani.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)