Umeme: Mboma kumuona rais


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version

MWENYEKITI wa bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Umeme (Tanesco), Jenerali Robert Mboma sasa anataka kukutana na rais kutafuta ufumbuzi wa tatizo la umeme nchini.

Katika waraka maalum kwa waziri wa nishati na madini, Mboma anasema, “…hali ndani ya shirika imekuwa mbaya kwa sababu hatuna fedha za kuendesha shirika. Hatuwezi kununua mafuta wala vipuri.”

Mboma anapendekeza viitishwe vikao vya dharura ndani ya wizara na hatimaye wahusika wakutane na “Rais Jakaya Kikwete ili kunusuru shirika.”

Waraka wa Mboma kwa Waziri William Ngeleja unaanza kuwa kulaumu hatua ya serikali kwa kile anachoita kuweka shirika “njiapanda” baada ya kushindwa kutimiza ahadi ya kulipa ruzuku kufidia gharama kubwa za uendeshaji.

Anasema kuna upungufu wa maji katika baadhi ya mabwawa na kwa hali hiyo, serikali italazimika mwakani kukodi mitambo mingine  ya dharura, kwa kuwa muda wa mitambo iliyopo sasa utakuwa umekwisha.

Tanesco imekuwa ikifuatilia ahadi ya serikali ya kutoa ruzuku ya Sh. 136 bilioni, kupunguza kodi ya mafuta yatakayotumiwa na mitambo yake; na dhamana kwa ajili ya mkopo wa Sh. 408 bilioni.

“Wizara na Tanesco vimekuwa vikifuatilia suala hili kwa miezi mitatu sasa bila mafanikio,” analalama mkuu wa majeshi mstaafu.

“Rais aliagiza mkopo huo wa Sh. 408 bilioni upatikane haraka. Lakini sisi tunazungukazunguka na hivyo kushindwa kutii amri ya amiri jeshi mkuu wa Tanzania,” Mboma anamweleza waziri.

Anasisitiza, “Katika hali ya kawaida tunatakiwa tufanye kazi usiku na mchana kwa nia ya kukamilisha maagizo halali ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Lakini Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando ameliambia MwanaHALISI kuwa Sh. 136 bilioni zilipokelewa na shirika lake miezi mitatu iliyopita na zimemalizika kutumiwa.

“Hizo fedha tumekwishazipokea, tumezitumia zimekwisha. Unajua makusanyo yetu ni Sh. 55 bilioni lakini matumizi yetu katika kuwalipa wazalishaji wa umeme ni Sh. 80 bilioni; hivyo hizi zimeishia huko,” alisema Mhando.

Amesema fedha ambazo hazijaingia ni zile za mkopo wa Sh. 408 bilioni ambao “uko hatua za mwisho.” Mkopo huo umeombwa City Bank ya Uingereza.

Kuhusu punguzo la kodi kwenye mafuta, alilosema “liko katika mchakato,” amesema Tanesco inatakiwa kuthibitisha kuwa fedha hizo zitanufaisha shirika peke yake.

Alipoulizwa waziri Ngeleja iwapo ameona waraka ulioandikwa na Mboma alisema juzi, “Kimsingi barua hiyo ilifika. Katika kuifanyia kazi, pamoja na mambo mengine, imejadiliwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.”

Alisema mjadala kuhusu suala hilo ulianza juzi Jumatatu na kwamba ungeendelea jana. “Ikifika saa tisa kesho (jana Jumanne), tutakuwa na taarifa juu ya nini cha kufanya, kwani tunashauriana. Kumbuka na kamati huwa na maoni yake kulingana na hali halisi,” alisema Ngeleja.

Vyanzo vya habari ndani ya Tanesco na serikalini vinaeleza kuwa hali ngumu ya shirika hilo itakuwa imemstua mwenyekiti ambaye aliamua kujitokeza kwa kutaka kukutana na rais.

Mboma anasema katika waraka wake kuwa kukatikakatika kwa umeme maeneo ya katikati ya jiji la Dar es Salaam kunatokana na kuharibika kwa transfoma mbili.

Anasema upungufu unaotokana na hilo, ungeweza kuzibwa na mitambo ya Aggreko au Symbion “kama tungekuwa na mafuta ya kuendesha mitambo hiyo.”

Ingawa Tanesco na wizara ya nishati wamekanusha madeni kuwa sababu ya umeme kukosekana, gazeti hili limegundua kuwa baadhi ya wenye mitambo wamesitisha ufuaji baada ya shirika kushindwa kuwalipa.

MwanaHALISI ina taarifa kuwa ni Tanesco, iliyoiarifu bodi yake, 12 Machi 2012, kuwa kuchelewa kwa dhamana ya mkopo, “kumesababisha hali ya shirika kuwa mbaya.”

Taarifa inaongeza kuwa hali hiyo ndiyo imesababisha “…shirika lishindwe kulipa wadeni wake, wakiwamo wakodishaji wa mitambo, ambao wamesimamisha uzalishaji wa umeme kwa wiki tatu sasa.”

Taarifa hiyo inaongeza, “Hali hiyo imesababisha kukosekana kwa megawati 60 hadi 150 katika gridi ya taifa.”

Akizungumzia hali hiyo juzi, Mhando alisema “wewe chukua ninachokwambia; sisi tunao uwezo wa kuzalisha umeme wa kutosha tatizo ni uchakavu wa miundombinu.”

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Mboma, shirika linahofia kupata wakati mgumu katika Mkutano wa Bunge unaoanza terehe 10 Aprili 2012, akisema, “tayari wabunge wa Dar es Salaam wamekwishalalamika juu ya ukataji wa umeme katika jiji.”

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Jenerali Mboma amemweleza Waziri pia kuwa “hali ya mabwawa ya Mtera na Nyumba ya Mungu ni mbaya sana”.

“Mtera ina mita 1.24 juu ya kiwango cha chini kinachoruhusiwa…Nyumba ya Mungu ina mita 3.22 juu ya kina kinachoruhusiwa. Maji haya ni kidogo hasa kama hali ya mvua itaendelea kuwa mbaya maeneo ya Mbeya, Iringa, Dodoma, Singida, Kilimanjaro na Tanga,” Mboma amenukuliwa akimweleza waziri Ngeleja.

Mboma anasema ukosefu wa mafuta utalilazimisha shirika kutumia maji hayo kidogo, hatua ambayo itasababisha Tanesco kukodi mitambo mingine ya dharura mwakani.

Kutokana na hali hiyo, anamwomba waziri wafanye vikao mbalimbali vitakavyohitimishwa kwa mazungumzo na Rais Kikwete.

Mboma, kwa mujibu wa waraka wake, alikuwa anataka kikao cha kwanza kiitishwe 21 Machi 2012 na kiwashirikishe yeye, waziri Ngeleja, katibu mkuu nishati na madini, Eliakim Maswi, wajumbe wawili wa bodi, menejimenti ya Tanesco na wajumbe wengine ambao waziri angeona wanafaa.

Vilevile anapendekeza kuwa Maswi azungumze na katibu mkuu Hazina, baada ya Tanesco kumuarifu matokeo ya kikao cha awali, na baada ya hapo ndipo wakutane na rais.

0
No votes yet