Umeme umeishinda Serikali


editor's picture

Na editor - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

HALI ya uzalishaji umeme katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa mara nyingine, inatia wasiwasi. Kuna taarifa kwamba kiwango cha maji katika mabwawa yanayotumika kuzalisha umeme kinazidi kupungua.

Mabwawa ambayo TANESCO inayategemea kwa ajili ya uzalishaji wa umeme ni Mtera, Kihansi na Kidatu.

Kulingana na ofisa wake aliyepo Bonde la Mto Rufiji, Willy Mwaluvanda, katika bwawa la Mtera peke yake, kina cha maji kimepungua kufikia mita 693.11 kutoka mita 698.5 maji yanapojaa.

Mwaluvanda anasema kima cha maji ambacho kinaleta hofu ya uwezekano wa kusitisha ufanyaji kazi wa mitambo ya kuzalisha umeme, ni mita 690.

Zimebaki mita tatu tu kukifikia kima ambacho TANESCO italazimika kusimamisha mitambo yake. Hakuna mvua zilizotarajiwa.

Lipo tatizo sugu. TANESCO ina mipango mingi, tena ya muda mfupi, wa kati na muda mrefu, lakini isiyoleta majibu ya haraka ya vipi itaendelea kuwahakikishia wananchi huduma ya umeme.

Wakati wataalamu wakieleza hali ilivyo, bila ya hofu yoyote, Waziri William Ngeleja, aliyerudishwa kusimamia Wizara ya Nishati na Madini, ameendeleza kauli tata kuhusu tatizo la umeme wa uhakika.

Ngeleja aliyebahatika kuyajua vizuri matatizo yanayokabili TANESCO, hali hii ingetosha kumsukuma kutoa majibu muafaka ya namna serikali inavyopanga kukabiliana na tatizo liliopo.

Badala yake anarudi na kauli zilezile akisema “nitahakikisha tatizo la uhaba wa umeme tunalipatia ufumbuzi haraka” bila kueleza miujiza anayokuja nayo.

Ukweli unabaki palepale. Serikali imechangia kudhoofisha uwezo wa TANESCO kujiendesha. Shirika limezidiwa na madeni, serikali yenyewe ikiwa haijatimiza wajibu wake ipasavyo.

TANESCO imebebeshwa mzigo mzito kwa miaka mingi na bila ya msaada wa maana haiwezi kujitutumua kivyake kwa kutaraji huruma ya kupatiwa ruzuku isiyotosha kutekelezea mipango yake.

Ilipo ina mipango mingi lakini haina raslimali za kuitekeleza kimatarajio. Shirika halizalishi vya kutosha, miundombinu yake mingi imechoka, na lina matatizo mengi kuliko uwezo wa kuyatatua.

Inasikitisha kuona shirika halijiwezi na serikali inajivuta katika kuonyesha uwezo wake wa kulisaidia likakidhi matumaini ya wananchi.

Katika hali kama hiyo, tunabaki kuuliza iko wapi hasa busara ya uongozi wa juu wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kutimiza wajibu wake wa kuhudumia wananchi wake iwapo hata wale asilimia 15 inaowahudumia hawapati huduma ya uhakika?

Hakika, ni mtihani kwa serikali. Haitaki kutamka kuwa imeshindwa. Lakini imeshindwa wajibu wake kwa Watanzania kwa kuwa wamekuwa wakishuhudia tatizo la umeme likishindikana kupata ufumbuzi wa kudumu kwa miaka yote hii tangu kuingia milenia.

0
No votes yet