Umoja wa Sitta, Kilango, Sendeka na Lowassa


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version
Tafakuri

CHAGUZI ndogo zilizofanyika Aprili mosi mwaka huu kwa ngazi ya ubunge jimbo la Arumeru Mashariki na kwenye kata kadhaa nchini zimeacha taswira moja muhimu.

Hii ni mvuto wa makamanda wa vita dhidi ya ufisadi kwa upande mmoja na watuhumiwa kwa upande wa pili.

Ingawa ni mapema mno kueleza kwa kina kwamba matokeo ya chaguzi hizo ni kielelezo muhimu zaidi cha mwelekeo wa kisiasa kwa sasa nchini, bado ni suala nyeti  kisiasa kutafakari kwa mapana yake matokeo haya kwa kutazama nyuma na kujikumbusha makundi ya kisiasa ambayo yamekuwa yakivutana nchini kwa kitambo kirefu sasa.

Kwa vyovyote itakavyoangaliwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinazidi kujipambanua katika sura iliyojaa utata na mkanganyiko. Nitajitahidi kufafanua kauli hii.

Katika jimbo la uchaguzi la Arumeru Mashariki kulikuwa na ushindani wa vyama viwili, CCM na CHADEMA. Kila chama kilipeleka watu wake, makada na wasaidizi wake ambao kwa hisia na imani za mioyo yao walisadiki kabisa kwamba wangesaidia kuvuna kura.

Kwa mara ya kwanza katika harakati za kuomba kura kwenye chaguzi ndogo, tuliona muungano wa mashaka wa makundi hasimu ndani ya CCM, yaani wale wanaojiita makamanda wa kupambana dhidi ya ufisadi kwa upande mmoja na wale ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa ufisadi wenyewe.

Katika kambi ya CCM ilionekana kuwa makada kama Mbunge wa Simanjiro Christopher ole Sendeka ni miongoni mwa watu waliojipambanua kuwa hawataki ufisadi na kimsingi wanaupiga vita kwa nguvu zote.

Ni sura kama hiyo ya makamanda wa ufisadi ndiyo ilimpeleka Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta katika kata ya Kirumba, Mwanza kuomba kura ili CCM ishinde.

Arumeru na kata ya Kirumba vilikamiwa vilivyo na CCM, si kwa bahati mbaya, ila ni kwa mkakati. Arumeru ilikuwa lazima kupata ushindi, kwa sababu lilikuwa jimbo la CCM ambalo liliongozwa na hayati Jeremiah Sumari, baba yake na aliyekuwa mgombea wa CCM, Sioi.

Kwa maana hiyo, Arumeru ilikuwa kulinda heshima ya CCM, kwamba bado ni chaguo la wananchi, lakini kubwa zaidi kuwasilisha ujumbe kwamba pamoja na kelele za upinzani kwamba serikali na chama tawala wamepotea njia katika kuendesha nchi, bado walikuwa chaguo la wananchi.

Kwa hiyo kuonekana kwa Sitta Kirumba, Sendeka Arumeru Mashariki na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela kujichimbia kata ya Kiwira, Mbeya, hazikuwa hatua za bahati mbaya. Ulikuwa mkakati wa kutumia karata ya ‘ukamanda dhidi ufisadi’ kupata kura.

Hali imeifunua CCM kuwa ina imani mbili; moja ya kutaka kuonekana wanapambana dhidi ya ufisadi, lakini pia hawataki kumuudhi yeyote. Wote ni abiria kwake. Haipigi vita ufisadi kwa nia ya kweli ndiyo maana haiwezi kuchukua hatua za kweli na za dhati dhidi ya ufisadi. Imebakia maneno tu!

Kwa bahati mbaya, karata ya vita dhidi ya ufisadi haikuisaidia CCM kupitia Sendeka Arumeru Mashariki, pia haikuisaidia CCM Kirumba kupitia kinywa cha Sitta na mbaya zaidi hata Kiwira ambako ilikuwa kata ya CCM pia mbwembwe za Kilango hazikusaidia chama hicho kuvuna chochote cha maana kiasi kuendelea kuongoza wananchi wa Kiwira.

Lakini pia CCM, ikijua kwamba haina ujasiri wa kweli wa kupambana na ufisadi, na ndani ya nafasi ya makada wake wakijua vilivyo kuwa hata hoja ya ufisadi si yao, ila waliipora kutoka CHADEMA, haikushangaza kuona mseto wa timu mbili hasimu; moja ya wanaoandamwa kuwa ni mafisadi, akiwamo Waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, nay a pili ya wanaowaandama, wakiwamo kina Sitta, Sendeka, na Kilango.

Wote kwa ujumla wao, hawakuwakuna wananchi wa Arumeru Mashariki, Kiwira na Kirumba. Mbele ya wananchi wamewaona kuwa ni wale wale.

Kwa hiyo, mseto wa makamanda na watuhumiwa wa ufisadi haukusaidia CCM kuvuna chochote cha maana ya Arumeru Mashariki, Kirumba na Kiwira. Katika mazingira kama haya, umma unaelekea kuanza kutambua kuwa ndani ya chama hiki hakika hakuna mwenye usafi wa kutosha kiasi cha kumpa nafasi ya kunyanyua kidole na kumnyooshea kidole mwingine. Wote ni wamoja, wanawaza na kunuia mamoja, hawa ni ndege wafananao daima huruka pamoja!

Kupoteza kwa CCM kwa kiwango hiki pia kumeelezwa kumechangiwa eti na mgawanyiko wa ndani kwa ndani. Inasemekana kuwa kule Arumeru Mashariki, baadhi ya makada waliokuwa kwenye kampeni ya Sioi, walikuwa na sifa ya “akumulikaye mchana, usiku akuchoma”.

Kwa maneno mengine, waliuzana wenyewe kwa wenyewe. Yaani CCM wamebobea katika siasa za umamluki. Ubaya wa siasa hizi za kimamluki hazifanywi dhidi ya chama kingine, ila wanafanyiana humo humo ndani, ndiyo maana haikushangaza basi watu kama Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, kuamua kuporomosha matusi yasioandikika dhidi ya viongozi wa CHADEMA badala ya kujenga hoja za kumwombea kura Sioi.

Lusinde ambaye anaonekana kuwa kijana, aliushangaza umma alipoamua kumwaga matusi katika wiki ya mwisho ya kampeni za kusaka kura, katika kipindi ambacho waomba kura wanapaswa kuonyesha unyenyekevu mkubwa kwa wapiga kura, yeye aliamua kuendesha siasa za mwituni, siasa ambazo zimekosa hata chembe ya ustaarabu na kumwaga matusi.

Hali hii haikushangaza Lowassa alipofanya kampeni zake akiweka sharti la kutokuruhusiwa kwa matusi katika mikutano ambayo angemnadi Sioi. Pia, haikushangaza kwa akina Lusinde aka Kibajaj kutokutia mguu katika mkutano wa Lowassa wa Kikatiti.

Tukirejea Kirumba, CCM ilikuwa imepania kwa udi na uvumba kunyakua kata hiyo, si kwa kubahatisha ila kwa kuwa waliiona kama upenyo wa kuipora CHADEMA nafasi ya kuongoza Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Akihutubia moja ya mikutano ya kampeni Kirumba Jumamosi Machi 24, mwaka huu, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema kuwa amepata taarifa kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza alikuwa amepewa maelekezo na Rais Jakaya Kikwete kuwa ampatie zawadi ya kata ya Kirumba.

Hii haikumaanisha kuwa ni kuimega na kumpa hati ya kuimiliki, ila ni kusaidia diwani wa CCM ashinde kwenye uchaguzi wa kata hiyo. Hesabu iliyokuwa inapigwa ni kuleta mageuzi ya kuongoza halmashauri kama CHADEMA ingelishindwa.

Kwa hiyo, Sitta kuteuliwa na chama chake kwenda Kirumba, kwanza kuzindua kampeni na kisha kuzifunga katika harakati za kusaka kura, haikuwa kazi nyepesi, aliaminiwa kwa kudhaniwa kuwa katika ile taswira waliyoijenga kuwa wao wanauchukia ufisadi basi wananchi wangelishawishika na hivyo kuipa CCM ushindi. Hata hivyo, matamanio yao  hayakutokea.

Kwa pamoja matokeo ya Kiwira, Kirumba na Arumeru Mashariki, yameacha somo moja muhimu, kwamba wale waliojitangaza kuwa ni wapambanaji dhidi ya ufisadi kimsingi hawana tofauti na hao wanaowapinga; ndiyo maana makundi yote haya mbele ya wananchi wameonekana kuwa ni sawa tu. Adhabu yao imekuwa ya kufanana, hakuna kura.

0
Your rating: None Average: 4.3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: