UN kuongeza maafa Sudan


editor's picture

Na editor - Imechapwa 18 March 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MSIMAMO wa serikali ya Sudan, Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu amani ya Darfur, ni Rais Omar El Bashir kuachwa asaidie hatua za kupatikana amani nchini mwake.

Na Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na kile kiitwacho jumuiya ya kimataifa wanaelewa fika kwamba hakuna hatua za upatikanaji amani zinazoweza kufuzu popote pale iwapo kiongozi mhusika wa eneo lenye mgogoro ni sehemu ya mgogoro.

Bado UN inaendelea kusisitiza kwamba ni lazima Rais Bashir akubali kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) ambayo inataka afikishwe mbele yake.

Tunasema tunachokiona muhimu zaidi kwa sasa nchini Sudan, ni utulivu. Utulivu hauwezi kupatikana iwapo mkuu wa nchi anatakiwa kukamatwa na kufikishwa mahakama ya kimataifa.

Kinachotafutwa ni amani kwanza mengine yafuate baadaye. Tunataka wananchi wa Darfur wawe kwenye utulivu ili waendeshe shughuli zao za kujitafutia maendeleo.

Pili, tunataka amani ya jumla ya Sudan kulingana na mkataba wa ndani kati ya serikali na wapinzani wake.

Sasa haya yaende sambamba na upatikanaji wa huduma za misaada kwa mamilioni ya watu ambao wamekuwa wakiishi kama wakimbizi ndani ya nchi yao kutokana na migogoro.

Hatupingi kukamatwa kwa Rais Bashir iwapo kuna ushahidi wa kumtia hatiani kwa ukiukaji haki za binadamu kwa watu wake.

Hoja yetu ni wakati gani wa kutekeleza hilo. Kwa wakati huu, la muhimu zaidi ni kutekeleza yale yanayoelekea katika kuleta utulivu kamili jimboni Darfur na Sudan kwa ujumla.

Uamuzi wa Rais Bashir kufukuza mashirika ya misaada na kutishia vikosi vya kulinda amani Darfur, ni mwanzo wa athari mbaya za tangazo la ICC kumtaka kiongozi huyo akamatwe.

Bali kuna haja ya kupanua wigo. Iwapo mahakama ya kimataifa inataka kuonyesha ilivyo taasisi adili, basi ishughulikie hata viongozi wa mataifa ya magharibi waliosababisha mauaji ya raia wa Irak, Afghanistan, Somalia na kwingineko duniani.

Kama mahakama haitafanya hivyo, basi hatua zake zote zitabaki kuwa kituko na ishara tosha ya kutowajibika kimatarajio ya walimwengu.

0
No votes yet