UN ni ndumilakuwili


editor's picture

Na editor - Imechapwa 23 March 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

UMOJA wa Mataifa (UN), kwa kufuata mapendekezo ya mataifa yenye nguvu kiuchumi na kijeshi, wiki iliyopita, ulipitisha azimio tata la kuzuia ndege za serikali ya Libya kuruka nchini kwake.

Hatua ya umoja ulioanzishwa mwaka 1945 kwa lengo la kusaidia kuimarisha amani na utengemano wa mataifa baada ya vita vya dunia, ililenga kuzuia ndege za kivita za serikali kupiga maeneo yanayoshikiliwa na wapinzani wa Rais Muamar Gaddafi.

UN wakaenda mbali zaidi kusema kuwa ndege zozote zinazotaka kwenda Libya au kuruka kupitia anga ya nchi hiyo, lazima ziombe idhini kwake.

Lakini katika hali ya kushangaza umoja huohuo unaozuia serikali ya Gaddafi kutumia anga yake kurusha ndege kupambana na waasi, umeruhusu ndege za Marekani, Ufaransa na Uingereza kuishambulia Libya.

Ndege za mataifa hayo zimeruka zitakavyo, eneo waliloliita ‘ukanda wa kutorusha ndege’ za serikali, na kuhujumu makazi ya Gaddafi na kuvunja miundombinu ya kijeshi ya serikali yake. Wameshambulia maeneo mengine ya nchi ikiwemo vitongoji vya mji wa Benghazi ambako vikosi vya Gaddafi vilijiandaa kusambaratisha waasi wanaoshikilia mji huo.

Kwa hali hiyo, majeshi ya serikali yameshambuliwa na waasi kwa msaada wa mataifa ambayo macho yao yako kwenye mafuta ya Libya.

Hapa UN imeonyesha undumilakuwili katika suala hilo moja maana haiwezekani serikali ‘ifungwe mikono’ kutumia anga yake kulinda utawala wake, lakini iruhusu ndege za mataifa ya magharibi kuishambulia serikali halali.

UN imepotoka. Tulidhani kuwa baada ya wananchi wa Libya kushindwa kutumia nguvu ya umma kumtoa madarakani Gaddafi kama wenzao wa Tunisia na Misri, umoja huo ulipaswa kufanya usuluhishi kama Umoja wa Afrika (AU) ulivyopendekeza.

Marekani haikuipiga Kenya yalipotokea mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ila ilisaidia kuratibu usuluhishi. Vilevile haikuipiga Zimbabwe ila ilisaidia AU kupata suluhu. Hata sasa haijapanga kuingia Ivory Coast ili kumtoa Laurent Gbagbo anayeng’ang’ania madaraka japokuwa ameshindwa uchaguzi wa kidemokrasia.

Kinachofanyika sasa Libya, kwa kibali ya UN, si kuzuia machafuko bali ni kuingilia utawala wa ndani wa nchi hiyo na kuhujumu uchumi. Mambo haya mawili si lengo la UN.

Kwa viwango vyovyote vile huo ni uonevu, dhuluma, ukandamizaji, undumilakuwili na ni kielelezo tosha kuwa umoja huo unatumika kutekeleza matakwa ya Marekani na washirika wake ya kuhakikisha Gaddafi anaondolewa madarakani iwe iwavyo.

Wakati tunaunga mkono matumizi ya nguvu ya umma inayoratibiwa na wananchi wenyewe bila ya ushawishi wa vyama vya siasa, tunapinga hatua ya UN kuruhusu nchi za Magharibi kuvamia nchi huru ya Libya na kusaidia waasi waipindue serikali halali.

Tunataka UN irudi kwenye mstari sasa. Izuie vitendo vyovyote, na popote pale duniani, vya kuvuruga amani kama ilivyoidhinisha nchini Libya.

0
Your rating: None Average: 3 (2 votes)