Unabii wa Nyerere watimia


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 03 November 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Hayati Mwalimu Julius Nyerere

UCHAGUZI umemalizika. Kinyume na matarajio ya walioko madarakani, wananchi hawakusikiliza tambo za kampeni za chama kilichopo ikulu.

Badala yake wamechagua mabadiliko na sasa wanasubiri mrindimo wa matokeo yanayotoa picha moja tu: Kwamba katika kipindi cha miaka mitano ijayo, “wanataka mabadiliko.”

Kupitia sanduku la kura, wananchi wamesema kwa kauli moja, “Hatundanganyiki."

Kimsingi, uchaguzi huu ulikuwa ni kati ya watu au mtu mmoja mmoja. Bali, uchaguzi uliomalizika ulikuwa ni kati ya mawazo mapya yenye maono na mifumo tofauti.

Ni tofauti na yale ambayo tuliyazoea kwa miaka 49 au mawazo mapya na mfumo mpya kuelekea nusu karne ijayo. Katika sehemu mbalimbali nchini, sauti iliyosikika inasema “tunataka mabadiliko.”

Ni lazima basi kuelewa ni mabadiliko gani ambayo wananchi wanataka. Hili ni jukumu kwa uongozi wa mahali na hata wa taifa unapoingia madarakani. Ni lazima uongozi huo ukae chini na kujiuliza ili uweze kupata tafsiri ya kitu gani hasa Watanzania wamekisema kwenye sanduku la kura. Kwa upande wangu nina maoni.

Walichokisema wananchi hasa kinahusu Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea wake wa urais, Jakaya Kikwete. Kwamba, kwa muda mrefu chama hiki kimeendelea kutawala bila kufikiri matokeo yake kwenye sanduku la kura.

Hata dakika za mwisho za uchaguzi bado waliendelea kujiamini kana kwamba wamegeuka mbuni walioficha vichwa vyao kwenye mchanga huku miili yao mikubwa ikiwa wazi ikiwafichua.

Kwa muda mrefu hasa katika miaka hii mitano iliyopita, wana CCM toka ndani na wakosoaji kama mimi (kutoka nje) ambao bado walikuwa na mapenzi na CCM tulijaribu kukikosoa ili kitumie muda kujisahihisha.

Pamoja na kuandika tena na tena, tukisihi kuwa CCM ni lazima ijichunguze na kujisahihisha, lakini hakuna ambaye alisikiliza. Nilitarajia sana kuwa wakati fulani mwaka huu (mapema) kungekuwa na mkutano maalum wa CCM ambao ungetumika kujisafisha. Mkutano ungelenga kujenga upya chama hicho.

Siyo mimi tu, hata juhudi za ndani na za watu wenye nguvu zaidi kutaka chama chao kijisafishe zilishindikana. Ni kama watu waliotiwa pamba masikioni; chama hiki kinachojiita kikongwe, kiliingia katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kikiwa kimevurugika kutoka ndani.

Kwa mtu yeyote aliyefuatilia siasa nchini dalili za CCM kunyeshewa mvua mapema zilianza kuonekana kwenye kura za maoni. Ni katika kipindi hicho ambapo CCM ilitakiwa ichukue hatua za ziada kujisafisha. Lakini wapi! Imeshindwa kufanya hivyo.

Matokeo yake wakarudi kwa wananchi wakitegemea hazina mbili kubwa ya kwanza ni Kikwete na ya pili ni jina la CCM.

Kwa upande wa Kikwete hilo halikuwa na shaka. Kwamba angalau kidogo bado anaweza kuwa na mvuto hasa kwa baadhi ya makundi, , lakini CCM kama chama kimekuwa na jina lisilo safi mbele ya jamii.

Ninaamini kabisa kuwa kama CCM ingeonesha japo kidogo tu, kwamba inajitahidi kujisafisha, matokeo ya uchaguzi huu yasingekuwa kama yalivyo sasa. 

Wapiga kura wa Tanzania wasije kudharauliwa tena na mtu yeyote kuwa hawajui kuchagua au hawaoni. Wapiga kura nao kama binadamu wana kikomo chake.

Nilipoandika juu ya “kuanguka kwa CCM unabii utatimia,” nilikumbushia ukweli kwamba punda mnyama wa kazi unaweza kumtumikisha kwa muda fulani lakini naye ana kikomo.

Unaweza kumtwisha mizigo akabeba kila siku lakini kuna siku ukimuongezea ukubwa wa mzigo huo anagoma. Leo wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wamegoma.

Hivyo basi, fundisho kubwa lililopo mbele yetu kati ya mengi ni kuwa kura ina nguvu. Katika demokrasia ni wananchi wanaoamua nani atawale na ni vipi atawale.

Wananchi wameamua na kura yao lazima iheshimiwe na wanancho wote hata kama haitupendezi au kutuvutia. Ni lazima tukubali kauli yao waliyoitoa kwenye sanduku la kura kwa kuchagua mabadiliko.

Viongozi wetu wa kisiasa wawe tayari kukaa chini ili kuweza kuliponya taifa kutoka katika siasa ambazo siku za mwisho za kampeni zilipakana na kuanza kujenga uadui kati ya nafsi na nafsi.

Wala hakuna mashaka kwamba yote tuliyoyaona na siasa kama ilivyo michezo mingine, kuna kutambiana, kupigana mikwara na hata kuchokozana, lakini kama ilivyo katika michezo kuna kushinda na kushindwa.

Wapo walioshinda na wapo walioshindwa katika uchaguzi huu. Leo siyo mwisho wa dunia, taifa hili bado ipo, na bado kuna uchaguzi mwingine mwaka 2015 na kutakuwepo na chaguzi nyingine ndogo ndogo nyingi.

Ni lazima tujifunze kufanya mambo ya kisiasa kama siasa yakiisha tunayaacha na kurudi katika umoja wetu wa kuiweka nchi yetu juu na mbele zaidi kuliko vyama vyetu, itikadi zetu, urafiki wetu na hata hofu zetu.

Ninatoa pongezi kwa mshindi na kwa wote walioshindwa. Walioshindwa, hasa wale walioshindwa katika mazingira huru na haki, ni vema wakasubiri nafasi nyingine.

Lakini kwa wale ambao wameshindwa kwa hila, ni vema wakafuta mkondo wa kisheria kutafuta haki yao. Hata kama haki hiyo, haitapatikana leo, lakini itaweza kujengwa msingi imara huko tuendako.

Lakini nani alifikisha CCM hapa kilipo? Bila shaka kila mmoja anajua. Kwamba haya ni matokeo yaliosababishwa na Kikwete mwenyewe aliyechukua marafiki na kuwapa uongozi wa umma.

Kama wanachama na viongozi wa CCM wanataka kuokoa chama chao, waachane na Kikwete, badala yake wajipange na kuokoa chama chao, lakini kikiwa mbali na Kikwete.

Mwaka 1995, Baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwambia viongozi wa chama chake – Chama Cha Mapinduzi, kwamba “angalau ya CHADEMA – Chama cha Demokrasia na Maendeleo. Lakini walijifanya kichwa maji.

0
No votes yet