Unafiki wa CHADEMA, ulafi wa CCM


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version
Zitto Kabwe akataa posho za wabunge

TAKRIBANI majuma mawili sasa, Bunge la Jamhuri na baadhi ya vyombo vya habari nchini vimetawaliwa na mjadala wa posho za wabunge na watumishi wa serikali.

Kwa hali ilivyo haielekei kama kuna mwenyekiti wa kweli wa mjadala huu unaovutia na kuamsha hisia kali miongoni mwa wananchi.

Mwangwi wa mjadala huu katika masikio ya watu wengi unaashiria hali mbaya ya mustakabali wa taifa letu. Wapo wanaowaona wabunge na viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambao kimsingi ndiyo waasisi wa kufutwa au kupunguzwa kwa posho, kama “wanafiki” wakubwa, wanaojifanya kutopenda posho wakati wanazitaka.

Viongozi wa chama hicho wanatuhumiwa kutumia suala la posho kujitafutia umaarufu kwa wapigakura. Wabunge wa CCM na watendaji serikalini wanaonufaika na posho wanawaona CHADEMA kama maadui wakubwa wasiofaa kuvumiliwa.

Upande wa pili unawalaumu wabunge na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwaona ni “walafi, mafisadi na wenye tamaa.”

Wabunge hawa wana mishahara mikubwa ikilinganishwa na watumishi wengine serikalini na wana utitiri mkubwa wa posho, ikiwamo mfuko wa jimbo, mikopo ya magari, posho ya mafuta na madereva – ambayo  wengi wanaitumia kuwapunja madereva wao.

Aidha, wana posho kubwa za kamati mbalimbali za bodi katika taasisi za umma na mashirika ya fedha, pamoja na lundo la marupurupu mengine ambayo hayatajwi  hadharani.

Wabunge hawa wana hali nzuri sana kulinganisha na hali za wananchi waliowachagua. Kitendo cha kung’ang’ania posho ya vikao, kinawaonyesha walivyo walafi na wakosaji wa shukrani.

Kwangu mimi, ni bora “unafiki” wa CHADEMA kuliko “ulafi” wa CCM. Nasema hivi kwa sababu, hoja za CHADEMA kupitia kiongozi wao wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe hazikuishia kwenye posho pekee. Zimeenda mbali.

Kama ni unafiki basi utakuwa ni unafiki wa kujitesa sana. CHADEMA wametamka hadharani posho zao wanazotaka zifutwe na sababu ya kuzifuta.

Wameelekeza zipelekwe kwenye kusaidia wananchi wanaoishi maisha ya shida zaidi. CHADEMA wamependekeza magari ya kifahari yafutwe na yaliyopo yauzwe. Anayetaka gari la kifahari akope na kununua lake.

Kimsingi CHADEMA katika suala la magari, wamekomesha ngojera za waziri mkuu Mizengo Pinda asiyependa hata kuumiza sisimizi katika maamuzi yake.

CHADEMA wapependekeza usafiri wa ndege kwa daraja la kawaida badala ya daraja la kwanza. Wamependekeza magari ya kifahari yauzwe ili akina mama wajawazito wanunuliwe magari ya maana kuliko vibajaji ambavyo Rais Jakaya Kikwete amewataka wajawazito watumie. Tayari Mbowe amerejesha serikalini gari alilokabidhiwa ili lipigwe mnada.

CHADEMA wamependekeza marekebisho muhimu katika suala la elimu, afya, usalama wa chakula na mengine mengi. Wanataka viongozi wachukue maamuzi mazito yanayoleta mateso kwa viongozi na unafuu wa maisha ya wananchi wa kawaida. Huu ni uongozi wa kujitoa mhanga badala ya uongozi wa kufaidi marupurupu.

Msimamo huu wa CHADEMA utaleta nafuu kubwa kwa watu wa kawaida lakini pia utaleta mtizamo mpya kuhusu utumishi wa umma. Huu si ukombozi wa wananchi wenye shida, bali hata ukombozi kwa viongozi wenyewe.

Viongozi wengi wa umma wanaishi kama wako peponi katika nchi yenye shida nyingi. Imefikia wakati viongozi wetu hawaamini kama wanaishi Tanzania yetu na kuamua kuwekeza hata mitaji yao nje ya nchi na kusomesha watoto wao Ulaya na Marekani kwa sababu wanaona hapa nchini hakuna usalama wowote kwa mtindo wao wa maisha wanayoishi.

Hii ikibadilika, wanaweza kugundua kuwa wamekombolewa katika gereza la kuona nchi yao haifai.

Kimsingi CHADEMA wanalenga kutibu gonjwa kuu la kitaifa kwa sasa linaloitwa “mradi siasa.” Watu wengi wasomi wamekimbilia mradi huu kwa sababu unalipa na hauna kodi nyingi.

Ukiishakuwa mbunge, hununui mafuta, hununui chakula cha bei ghali, hutibiwi katika hospitali zetu labda ukianguka ghafla bungeni; watoto wako watasoma nje, Mamlaka ya Mapato (TRA) watapita biashara yako kama wanavyopita kituo cha polisi.

Nazo benki zitakupa mikopo na mkataba utasaini baadaye utakapopata muda; utachelewesha ndege kuondoka uwanjani, utasafiria daraja la kwanza na vimada wako wawili wasiojuana katika ndege moja; makatibu wakuu wa wizara watakupa mafungu na kukukarimu wizarani ili usikwamishe bajeti zao.

Hata wakuu wa mashirika ya umma wataomba kukukarimu badala ya wewe kuwaomba. Kuna mengi mengine utayapata. Ni kwa sababu, mradi huu unalipa na ndiyo maana wengi wanaukimbilia.

Msimamo wa CHADEMA ukikubaliwa, utakisaidia chama chetu – CCM, kuondokana na minyukano ya ndani kwa ndani kwa sababu minyukano hiyo inahusu ulaji wa raslimali za nchi na ulinzi wa pato dhalimu lililokwishakusanywa na baadhi ya wanasiasa.

Haiwezekani mtu mwenye mabilioni ya shilingi kuanza kugombana na kuraruana na wenzake ili kuchaguliwa nafasi yenye mshahara wa Sh. 2 milioni! Kinachowafanya wararuane ni zaidi ya mshahara wa ubunge na urais.

Wanaruana kwa sababu wanashtakiwa nyoyoni mwao; ni jinsi gani watajibu siku wakiulizwa walipataje utajiri huo kwa mshahara wa Sh. 2 milioni kwa mwezi? Njia pekee ya kuwahakikishia usalama ni kupambana kubakia madarakani.

Kama uongozi ungekuwa ni mzigo na msalaba, wala tusingesikia wanamalizana kama wanavyofanya sasa. Hakuna anayemalizana na wenzake ili kuwatumikia wananchi kwa njia ya kukabiliana na shida.

Ndiyo maana hatujawasikia wabunge wa chama chetu wakisema watajiuzuru ubunge endapo serikali haitapitisha bajeti yenye kuhakikisha wazee wote nchini wanapata pensheni ya Sh. 5,000 kwa mwezi.

Badala yake tumemsikia waziri mkuu akitetea posho kwa madai kuwa zinatumika kuwasaidia wenye shida wanaofika viwanja vya Bunge kuwaomba wabunge.

Hii si njia rasmi ya kutumia posho za wabunge. Kwanza tunawajua wabunge ambao hata soda hawawezi kumnunulia mtu, badala yake hata wao huwategemea wapigakura wao wawanunulie soda baada ya uchaguzi. Wabunge hununua soda wakati wa uchaguzi.

Ni vema wabunge wa CCM, kama wanakipenda chama chao na wanataka kuendelea kutuongoza, wakubali msimamo wa CHADEMA. Ni hatari na hasara kwao wenyewe wakiendelea kudhani kila jambo la CHADEMA lina kasoro. Maslahi ya taifa ni muhimu yatangulizwe mbele ili uongozi uonekane kuwa na maana kwa wananchi.

Kuongoza ni kuonyesha mfano na kama serikali inataka wananchi waielewe, haina budi kuwaunga mkono CHADEMA. Hivi sasa katika mabaraza ya majumba ya wahisani wa serikali yetu, ndani na nje ya nchi, malalamiko juu ya posho za vikao yanaongezeka.

Ukipitia maandiko yote ya miradi katika wizara zetu, utaona yamejaa orodha ndefu ya posho za vikao. Imefikia mahali hata kuwatibu watu malaria inabidi kwanza uwalipe posho.

0
Your rating: None Average: 3 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: