Undumila kuwili wa Marekani unazidi kila siku


Zakaria Malangalila's picture

Na Zakaria Malangalila - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version

KATIKA siasa za nje (na za ndani pia) kwa Marekani, unafiki na undumilakuwili ni vitu vya kawaida na vimekuwa mtindo katika uendeshaji wa sera zake kwa miaka mingi – hadi kufikia usemi kwamba Marekani huwa haina rafiki au adui wa kudumu, bali ina maslahi ya kudumu.

Angalia tu: Marekani, nchi tajiri, yenye nguvu na kustaarabika (sifa hii ya mwisho ina mjadala) kuliko zote duniani ilifikia kuwaua Sadam Hussein na Osama bin Laden kwa njia ya ukatili mkubwa, licha ya wawili hawa kuwahi kuwa maswahiba wake.

Katika miaka ya mwanzoni ya 1980, Marekani, chini ya Rais Ronald Reagan, ilimtumia Saddam kuishambulia Iran. Hii ilitokea mara tu baada ya Mfalme Shah (mshirika mkubwa wa Washington enzi zile na nchi inayotoa mafuta mengi) kupinduliwa na wananchi walioongozwa na Ayatollah Rohullah Khomeini na kutangaza Jamhuri ya Kiislamu.

Marekani iliona mapinduzi ya Iran lazima yazimwe kwani yangeweza kuenea na kuambukiza nchi nyingine jirani, hasa Saudi Arabia, mshirika wake mkubwa mwingine, nayo ikiwa inatoa mafuta mengi.

Vita baina ya Iraq na Iran vilichukuwa miaka minane na Marekani walidiriki hata kumpa Saddam silaha za sumu ili azitumie dhidi ya majeshi ya Iran hasa ilipofika mwaka 1984 wakati majeshi yake yalipokuwa yanazidiwa nguvu na kutishia kuingia nchini mwake.

Hivyo basi miaka 20 baadaye, wakati Marekani inakazania kwamba Saddam anamiliki silaha za maangamizi pamoja na za sumu, ilikuwa inajua kile ilichokuwa inakisema.

Marekani walimtumia Osama nchini Afghanistan, katika miaka ya 1980 pia katika jitihada za kuwaondoa Warusi wa Kisovieti waliokuwa wanakalia nchi hiyo. Walimtuma kwenda kuwasaidia wapiganaji (baadhi yao ni wanaoitwa sasa Taliban) katika kuwachimbia mahandaki n.k., ya kujihami, kwani yeye kitaaluma alikuwa ni mhandisi.

Sasa, utawala wa Barack Obama nao unafuata nyayo hizohizo za siasa za undumilakuwili za kina Reagan. Obama amekuwa akipuliza tarumbeta kunadi maadili mema ya nchi yake kwa kuzitaka nchi nyingine zijiheshimu na zifuate maadili hayo, kudumisha uhuru na demokrasia.

Swali: Nchi hizo zitafuataje maadili mema iwapo Obama, wakati yumo katika harakati za maandalizi ya uchaguzi mwaka ujao, anatuma vikosi vya mauaji katika nchi za mbali –Abbotabad ndani ya Pakistan – kuua? Anatuma ndege zisizo na rubani kuua raia wa nchi nyingine – hasa wale wasio na hatia – wakiwemo wanawake na watoto? Wakishaua wanasema “samahani, hatukudhamiria kulenga raia.”

Marekani kweli inaweza kukaa kimya iwapo Ahmedinejad atatuma kikosi cha mauaji kuwaua wapinzani wake waliojichimbia mjini New York?

Na wiki mbili zilizopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton aliushambulia utawala wa China kwa madai ya kuminya demokrasia na haki za kibinadamu – wakati nchi yake imekuwa ikiaibishwa na waandamanaji wa nchi zilizokuwa swahiba zake hadi kufikia kuwang’oa viongozi wake kutokana na tuhuma kama hizo zilizoelekezwa China. Nchi hizo ni Tunisia, Misri na sasa Yemen.

Aidha mapema mwezi uliopita, Obama alitia saini mkataba wa kupanua biashara baina ya nchi yake na Colombia, nchi ambayo mwaka jana iliua viongozi 51 wa vyama vya wafanyakazi na vikundi vya mauaji vilivyodhaminiwa na serikali.

Tukiacha huko Marekani ya Kusini, tuangalie Bahrain, nchi ya kisiwa ambayo inahifadhi wanajeshi wa Marekani waliojenga kituo kikubwa cha jeshi la wanamaji (US 5th Fleet).

Wakati Clinton akiwashutumu watawala wa China, habari za kuhuzunisha zilikuwa zinasikika kuhusu ukandamizaji wa raia nchini Bahrain wa madhehebu ya Shia kutoka kwa utawala wa kifalme wa Kisunni. Idadi ya Mashia nchini humo ni zaidi ya asilimia 80.

Habari zilisema askari kutoka vikosi vya serikali vya usalama waliofunika nyuso zao walikuwa wakivamia vijiji vya Mashia ifikapo usiku. Zaidi ya misikiti 27 ilivunjwa kwa mabuldoza kwa kushukiwa kuwa ni vituo vya viongozi wa waandamanaji wanaoipinga serikali.

Kama hii ingekuwa ni Libya, Clinton haraka angetamka kwamba mashambulizi hayo dhidi ya raia yalipaswa kujibiwa na mashambulizi ya vikosi vya Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO). Lakini siyo Bahrain.

Kukosekana kwa karipio lolote kutoka Marekani kuhusu uminywaji wa haki za binadamu unaofanywa na watawala wa Bahrain ni kwa sababu makaripio yote yalikuwa yanaelekezwa kwa utawala wa Kanali Muammar Ghaddafi wa Libya. Hali hii imetoa mwanya kwa utawala wa Kifalme wa Wasunni ukiongozwa na familia ya Al-Khalifa, kuendeleza uovu dhidi ya raia wake.

Lakini pengine hakuna suala ambalo Obama amelivurunda kama mgogoro wa Palestina. Msimamo wake wa kutaka kuwepo taifa la Wapalestina na mazuri mengine kuhusu Wapalestina ulivurugwa vibaya na kauli yake kwamba yuko tayari kuzuia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kulitambua taifa la Palestina ifikapo Septemba mwaka huu.

Kuyumba huku ambako kumempotezea Obama nyenzo ya kumkabili Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, unatokana na nguvu za ushawishi za Wayahudi (Jewish lobby) dhidi ya serikali ya Obama. Hii ilisababisha mwanahabari mmoja maarufu wa Kiyahudi, Uri Avnery, kutamka katika makala yake wiki iliyopita: “Obama atajifanya kwamba kilichotua kwenye shavu lake siyo mate, bali tone tu la mvua.”

Na tukija katika sera zake za ndani: Yale mambo mazuri ambayo Marekani imekuwa ikiyasisitiza yafanyike kwa nchi nyingine, yenyewe hainayo na ni onyesho tosha la undumilakuwili wa nchi hii.

Marekani ina wafungwa 2.3 milioni katika magereza yake. Idadi hii ni wastani wa wafungwa 743 kwa kila raia 100,000 ikilinganishwa na Russia yenye wastani wa wafungwa 580 kwa idadi hiyo; China wafungwa 186; Uingereza inao 154 na India ina wafungwa 32 kwa idadi hiyo ya watu 100,000.

Nusu ya wafungwa hao 2.3 milioni waliopo Marekani, ni watu wa asili ya Afrika, ingawa idadi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika nchini humo ni asilimia 20 tu ya Wamarekani wote.

Hali hii iliifanya Mahakama Kuu ya Marekani kuiamuru serikali ya jimbo la California kupunguza idadi ya wafungwa katika magereza yake. Kwa sasa jimbo hilo tu lina wafungwa 143,335 – yaani wamezidi kwa watu 30,000.

Inavyotakiwa katika kuonyesha kuwa magerezani kuna utu, angalau idadi ya wafungwa wasizidi 80,000.

zakmalang@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 4 (2 votes)