UNITA washangilia uamuzi wa korti


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 June 2012

Printer-friendly version

MAELFU ya wafuasi wa chama cha upinzani cha Unita Jumamosi iliyopita walifanya maandamano makubwa kusherehekea uamuzi cha mahakama kumsimamisha kazi msimamizi wa uchaguzi nchini ikiwa ni miezi michache kabla ya kuelekea katika uchaguzi mkuu.

Wakiwa wamevaa fulana zenye picha ya mwenyekiti wa chama hicho cha upinzani, Isaias Samakuva, pamoja na kofia nyingi zenye nembo ya chama hicho zenye rangi nyekundu na kijani, maelfu ya watu hao walikuwa wakiimba na kucheza katika mji mkuu wa Angola, Luanda.

"Uchaguzi huru, haki na uwazi, unaoheshimu sheria," ilikuwa kauli mbiu ya watu hao waliokusanyika kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu.

"Tupo hapa ili kumshinikiza rais kuhakikisha kuwa taratibu zote za uchaguzi zinatekelezwa ipasavyo," Samakuva aliuambia umati wa watu.

"Ili uchaguzi huu uende vizuri, ni lazima kwa kila mmoja kujiandaa kupiga kura lakini pia kulinda kura zenu," alisema Samakuva.

Unita ilikusanya idadi ya watu wanaokadiriwa kufikia 10,000, lakini hakukuwa na kiwango maalum kilichokadiriwa na polisi. Samakuva alisema kuwa maandamano zaidi yatafanyika wakati wa kukaribia kwa uchaguzi.

Chama hicho cha upinzani kiliandaa maandamano ili kuwasilisha shinikizo lake la kutaka msimamizi wa uchaguzi, Suzana Ingles kuacha kazi, kikidai kuwa hajatimiza vigezo vya kisheria katika kufanya kazi hiyo.

Alhamisi iliyopita, Mahakama Kuu ilikubali na kuamua kuwa Suzana aachie nafasi yake ya kuongoza tume ya uchaguzi.

Hata hivyo, chama tawala nchini humo, MPLA ambacho kimekuwa madarakani tangu kupatikana kwa uhuru kutoka kwa Wareno mwaka 1975 kimekuwa kikikabiliwa na changamoto chache katika utawala wake.

Unita, chama ambacho kilikuwa kikipigana vita na Serikali ya Angola kwa miongo kadhaa iliyopita kiliamua kuendelea na maandamano hayo katika kusherehekea uamuzi wa mahakama.

Kwa mwaka huu, uchaguzi huo utakuwa ni wa tatu katika historia ya Angola. Uchaguzi wa kwanza ulifanyika mwaka 1992, japokuwa haukukamilizika kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, na uchaguzi wa pili ulifanyika mwaka 2008, miaka sita baada ya kumalizika kwa vita.

Katika uchaguzi wa mwisho, chama cha MPLA kilishinda kwa zaidi ya asilimia 81 na kilitumia wingi wa wabunge wake katika kupitisha muswada wa sheria mpya ikiwemo katiba mpya, ambayo imeondoa moja kwa moja uchaguzi wa rais.

Hivyo, Rais atakuwa akichaguliwa kutoka katika orodha ya juu ya chama kitakachoshinda katika uchaguzi wa mwaka huu, na hivyo ukitarajiwa kumpatia kirahisi muda mwingine wa kuendelea kukaa madarakani rais Jose Eduardo dos Santos.

0
No votes yet