Unyama wa polisi Arusha na maigizo kwenye TV


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 19 January 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki
Polisi imetumia nguvu iliyopitiliza Arusha

MKANDA wa picha unaotumiwa na polisi kuonyesha kile ambacho inadai kilitokea Arusha, hauwezi kulibakizia heshima jeshi hilo.

Mjini Arusha, tarehe 5 Januari 2011, polisi walifyatua risasi za moto na kuua na kujeruhi waandamanji – wanachana, wafuasi,mashabiki wa Chama cha demokrasia na Maendeleo na wananchi wengine.

Ijumaa iliyopita, kupitia vituo vitatu vya televisheni nchini – TBC, ITV na Channel Ten, polisi walionyesha mkanda wa video uliojaaa matukio yaliyokatwakatwa.

Katika mkanda huo ambao baadhi ya wananchi wameita “wa kuchonga,” polisi hawaonyeshi matukio ya mapema siku hiyo yaliyosheheni ukatili uliokithiri dhidi ya raia wasio na silaha.

Hawaonyeshi kwa mfano, jinsi walivyofyatulia raia risasi za moto, walivyowashambulia kwa virungu, mabomu ya machozi na maji ya washawasha.

Hauonyeshi jinsi walivyokuwa wanavamia na kupasua vioo vya magari ya raia; walivyowapiga kama nyoka wabunge wa CHADEMA, mashabiki na wafuasi wengine wa mageuzi jijini Arusha.

Mkanda wa polisi hauonyeshi jinsi watu ambao kabla ya kuguswa na polisi walikuwa wakiandamana kwa utulivu, wakiimba na kusindikizana wakienda uwanja wa mkutano.

Mkanda wa polisi hauonyeshi jinsi maandamano yalivyoanza kwa amani kuelekea uwanja wa mkutano na jinsi ambavyo, kama si kuvamiwa na polisi, yangemalizika kwa amani kama ambavyo ilitokea siku saba baadaye katika mazishi ya waliouawa na polisi.

Mkanda unaacha matukio yote ya mapema siku hiyo na badala yake unawapeleka watazamaji katika matukio ya jioni kwenye mkutano wa hadhara ambako pia wananchi walichokozwa.

Mkanda unaonyesha viongozi wa CHADEMA wakitoa matamko makali dhidi ya polisi na serikali. Hapa unalenga kusisitiza hoja ya “uchochezi” bila kuonyesha kiini cha hoja hizo.

Polisi wanatumia kanda iliyochakachuliwa, lakini wananchi wa Arusha walikuwepo na wanajua kilichotendeka.

Hata wananchi wa mikoa mingine, walishaona matukio ya asubuhi yaliyosheheni manyanyaso ya polisi dhidi ya raia.

Polisi wanasahau kuwa vyombo vilevile walivyotumiwa kurusha matangazo yao ya propaganda, ndivyo vilitumika tarehe 5 Januari 2011, kurusha picha zilizoonyesha kilichotokea Arusha.

Ilitarajiwa polisi waombe radhi wananchi kwa waliyotenda. Hawakufanya hivyo. Sasa jeshi linatumia fedha za wananchi kununua muda wa matangazo yenye lengo la kuficha ukweli.

Bila shaka wanaendelea kushikamana na CCM, ambapo kupitia katibu mkuu wake, Yusuph Makamba wameshangilia mauaji yaliyotokea Arusha.

Polisi wanashindwa kujua kuwa nguvu ya umma haiwezi kunyamazishwa kwa risasi. Mfano hai ni nchini Tunisia. Hivi sasa haina rais. Hakufukuzwa ikulu na risasi za polisi, amefukuzwa na nguvu ya umma; si kwamba polisi hawakuwapo.

Walikuwapo. Wamepiga na kuua sana raia. Lakini mwisho wa siku, nguvu ya umma ilishinda; rais amekimbia nchi yake.

Ni vema polisi wakafahamu kuwa kuzungumzia lugha za uchochezi wa viongozi wa CHADEMA, bila kutaja kilichosababisha, kunazidisha shaka kwa wananchi juu ya uadilifu wa jeshi hilo kwa mwajiri – wananchi.

Walichofanya CHADEMA Arusha ni harakati za kujitetea na kujinasua kutoka kwenye unyanyasaji wa serikali na polisi.

Kama msimamizi wa uchaguzi angegoma kumwapisha mbunge wa Viti Maalumu kutoka Tanga ili awe diwani Arusha, wala CHADEMA wasingekuwa na nafasi ya kuitisha maandamano.

Kama msimamizi wa uchaguzi, asingewahujumu kwa kukataa kuwatumia barua za mwaliko wa uchaguzi wa meya, na badala yake akawaita madiwani wa CCM kwa siri, wakafanya uchaguzi peke yao na diwani mmoja wa TLP, CHADEMA wasingelalamika.

Kama CHADEMA wangeshirikishwa, wakapiga kura zisitoshe, wasingekataa uchaguzi wala matokeo yake. Na kwa sababu hiyo, wasingeitisha maandamano ya kupinga kile kilichotokea.

Kama polisi isingeingia katika mtego wa kuruhusu na kuzuia maandamano yao, isingelazimika kuwafuata na kuwapiga waandamanaji, maana wasingekuwapo.

Makosa ya jeshi la polisi katika hili yamejikita katika maeneno matano. Kwanza, ni kukubali kukaa upande wa mkurugenzi wa jiji, Estomi Chang’a aliyesimamia uchaguzi feki.

Hili linathibitishwa na kitendo cha polisi kuingia ndani ya ukumbi wa manispaa na kumshambulia kwa virungu hadi kumuumiza vibaya, mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema aliyekuwa anapinga uchaguzi feki wa meya.

Pili, kuingilia maandamano ya CHADEMA yaliyokuwa yamefanyika kwa amani kwa takribani kilomita mbili.

Tatu, kuwafuata mkutanoni na kuwapiga mabomu wafuasi wa CHADEMA, jambo lililopandisha hasira na chuki za wafuasi wa chama hicho.

Nne, hatua ya polisi kutumia nguvu iliyopitiliza, kurusha risasi za moto na kuua raia, na sasa kuamua kuchakachua mkanda wa matukio ya Arusha na kuurusha ili kuwaghilibu wananchi.

Tano, mkuu wa jeshi hilo, Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP), Saidi Mwema alikiuka mipaka ya kazi yake kwa hatua yake ya kufuta maandamano ya CHADEMA.

Kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 na ile ya jeshi la polisi, mkuu wa jeshi hilo hana mamlaka yoyote ya kisheria, kuzuia au kuruhusu maandamano na mikutano ya hadhara iliyoitishwa na vyama vya siasa.

Mtu pekee mwenye mamlaka hayo chini ya sheria ya polisi na sheria ya vyama vya siasa, ni “ofisa polisi mwenye mamlaka ya eneo la mkutano.”

Anayetajwa hapa, kwa maana ya neno eneo la mkutano, ni mkuu wa wa polisi wa wilaya.

Lakini hata katiba ya Jamhuri inalinda uhuru wa wananchi kufanya maandamano na mikutano ya hadhara. Haki hiyo ya kikatiba, haiwezi kupokonywa kwa visingizio vyovyote vile, kikiwamo hicho kinachoitwa na polisi, “Taarifa za kiintelijensia.”

Sasa swali la kujiuliza: Mkanda huu utawasaidia vipi polisi kuficha ukweli, wakati wameshakiri kuwa walitumia risasi za moto kutawanya waandamanaji?

Hivyo basi, katika hili polisi hawawezi kukwepa lawama kwamba walikuwa wanafanya siasa – tena siasa za CCM.

Lakini ukiacha yote hayo, kuna swali jingine kubwa la ziada. Hivi wanapojiweka katika mizani, wanaona wao nao ni kundi lililoneemeka kiasi cha kuwaua wanyonge wenzao?

Hivi baada ya tukio la 12 Januari 2011, siku ambayo CHADEMA na wananchi wa Arusha walikuwa wanatoa heshima za mwisho na mazishi kwa waliouawa; hawaoni kwamba wao ndio waliosababisha ghasia zilizoleta sokomoko na vurugu Arusha?

Siku ambayo wananchi wa Arusha waliandamana kwa amani na bila kulindwa na polisi hata mmoja, kutoka chumba cha maiti hadi viwanja vya NMC, ndiyo iliyodhihirisha kuwa tatizo lote la Arusha chanzo chake ni polisi.

Hivi kwa nini polisi hawataki hata kuheshimu kauli ya kiongozi wao, Shamsi Vuai Nahodha, kwamba makosa yamefanyika mgogoro huu wa Ausha unahitaji kumalizwa kwa njia ya majadiliano?

0
Your rating: None Average: 3.9 (13 votes)
Soma zaidi kuhusu: