Uongo wa Nape, Ridhiwani utamaduni wa CCM


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 18 May 2011

Printer-friendly version
Tafakuri
Ridhiwani Kikwete

DINI zote duniani hufundisha watu kutenda mema. Kwa mfano, hukataza kusema uongo, na wazazi wakati wote huwa na wajibu wa kuhakikisha wanawarithisha watoto wao maadili mema. Ni kwa kufanya hivyo tu jamii hukuza maadili mema na kuchukia uovu.

Taasisi nyingine zilizoundwa na wanadamu nazo hujengwa kwenye misingi ya kiuadilifu ili zistawi kwa nia ya kufikia malengo yake; taasisi yoyote inayokwepa uadilifu hata ikistawi kwa kiwango gani, mwisho wake ni kuporomoka tu.

Wiki iliyopita kulikuwa na malumbano makali katika vyombo vya habari, yakihusisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa upande mmoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa pili.

Hoja kubwa iliyokuwa inabishaniwa ni malipo ya ujira kwa makatibu wakuu wa vyama hivyo. CCM kupitia kwa Katibu wake wa  Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye, alikuwa akipaza sauti juu ya mshahara wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Willibroad Slaa, kwamba Sh. milioni 7.1 anazolipwa ni nyingi sana.

Nape alikanusha kwa mdomo mpana habari zilizokuwa zimetolewa na CHADEMA kuwa Katibu wao Mkuu, Wilson Mukama, alikuwa analipwa mshahara wa Sh. milioni 11.

Nape alisema Mukama analipwa Sh. 1. 5 milioni tu na posho ya kila mwezi ya Sh. 300,000, fedha ambazo kwa Nape ni kidogo sana ikilinganishwa na za Dk. Slaa na kwa maana hiyo Dk. Slaa anaonyesha hana uzalendo kwa wananchi wanaoishi maisha ya ufukara ilhlai yeye anayejiita mtetezi wao akilipwa mshahara mnono.

Nape kwa maana hiyo ametaka kuaminisha umma kwamba Mukama analipwa posho na mshahara wa Sh. 1,800,000 tu kwa mwezi. Habari hii inahitaji tafakuri ya kina juu ya ukweli wa kauli ya Nape. 

Kabla sijaenda mbali nikumbushe tu yapata wiki mbili au tatu hivi zilizopita, Ridhiwani Kikwete, kada wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) akiwa mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji na Baraza Kuu, naye alijitokeza hadharani akijibu tuhuma dhidi ya ukwasi wake baada ya kuitwa bilionea. Watu walitaka kujua ameupata katika njia gani ambazo zipo wazi.

Ridhiwani alisema hana utajiri wowote, ila anamiliki gari aina ya Toyota Camry ambalo ni la kawaida tu, wala si Hammer kama ilivyodaiwa. Halafu akasema ana akaunti yenye fedha kidogo tu, hakutaja kiasi halisi cha fedha zilizoko, na zipo katika benki zipi hasa; lakini pia akadai kuwa ana shamba la hekari moja kwao Bagamoyo.

Mtandao wa media ya kijamii wa Wanabidii wiki hiyo ulikuwa na jumbe nyingi juu ya suala la Ridhiwani, lakini nilivutika zaidi na mchangiaji mmoja aliyehoji: “hivi hilo shamba la hekari moja la Ridhiwani linajumuisha na kiwanja anachomiliki Burka, Arusha?”

Kiwanja hicho ni kati ya viwanja walivyomilikishwa vigogo mkoani Arusha na kuzua malalamiko ya wananchi wa kawaida ambao hawakupewa viwanja licha kuahidiwa kuwa wangemilikishwa. Jina la Ridhiwani lilikuwa miongoni mwa majina ya vigogo hao.

Nimechukua mifano hii miwili ya makada hawa vijana kujenga hoja moja muhimu ya ‘uadilifu’. Ridhiwani hadi leo hajawahi kukanusha kumilikia kiwanja Arusha, japokuwa binafsi sina ugomvi naye kumiliki kiwanja kokote atakako katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au kwenye sayari ya dunia, ni haki yake, lakini tatizo ni pale anapokwenda hadharani, mbele ya vyombo vya habari kutaja mali zake, huku akiacha nyingine ambazo kwa bahati nzuri jamii inazifahamu.

Kwa hiyo, jamii inapoona kuwa habari zenyewe za kukanusha na kuweka rekodi sawa ni za kutengenezwa, inajawa na maswali kuliko majibu kwamba hivi hawa vijana wabichi wakitazamwa kama viongozi wa kesho wa taifa hili wanapata wapi ujasiri wa kusema mambo ambayo hayana uhakika hadharani? Je, wakianza kuzungusha maneno leo na ujana wao wakiwa wazee itakuwaje?

Nape naye kasema kuhusu mapato ya bosi wake, sawa, lakini hajasema kwamba Mukama ana gari alilolipiwa na chama, linajazwa mafuta na chama; hajasema kuwa Mukama analipiwa nyumba na  chama; lakini pia hajasema kama analipiwa matibabu na wategemezi wake.

Kikubwa zaidi hajasema kama ana posho ya kukirimu wageni, posho ya simu na marupurupu mengine mengi yanayolingana na kufanana na nafasi yake kama mtendaji mkuu wa CCM.

Ni vigumu mno kusadiki kwamba kama makatibu wa CCM wa mikoa wanalipwa mshahara wa Sh. milioni moja baada ya kodi, na wale wa wilaya wakilipwa Sh. 700,000 baada ya kodi, na Katibu Mkuu wa UVCCM akilipwa Sh. milioni 1.7, inawezekanaje bosi wao wa juu kabisa kulipwa jumla ya Sh. 1,800,000 tu kwa maana ya mshahara na posho zote?

Nape anajua, na kama hajui hakutaka kutafuta taarifa sahihi kwamba Katibu Mkuu wa CCM hana kiwango maalum cha mshahara; inategemea mtu huyo katokea wapi. Kwa kawaida anahamishwa na mshahara wake kutoka alikokuwa, kwa maana kwamba analipwa sawa na huko alikokuwa na nyongeza ya posho kibao juu yake.

Nape atakuwa analifahamu hili, amekaa pale ofisi ndogo za makao makuu Lumumba kwa miaka kadhaa sasa, anajua vizuri habari hii. Lakini kwa makusudi tu ameamua kutokusema ukweli.

Kwa kauli za Nape na Ridhiwani katika muktadha tofauti, zinaeleza kitu kimoja kibaya ndani ya jumuiya za chama na katika chama kwa ujumla wake, kwamba kusema uongo ni sehemu ya utamaduni wa chama. Tena uongo huu unasemwa hadharani, mbele ya waandishi wa habari bila hata wahusika kuwa na chembe ya soni kwamba kauli zao zinaweza kuwageuka.

Kwa wenzetu wanaojali maadili, kusema uongo kwa kiongozi yeyote ni sababu tosha ya kumweka pembeni katika wajibu wa umma aliokabidhiwa, lakini kwa bahati mbaya sisi tunajenga mfumo wa kusema uongo, kutokuwajiba, yaani kiongozi anaweza tu kujisemea lolote na hakuna chochote kitakachompata hata kama alichosema ni uongo wa saa sita mchana.

Tatizo la viongozi kusema uongo ni kubwa. Lina madhara makubwa, ni janga la kiuongozi kwa sababu anayesema uongo akiwa amekalia ofisi ya umma anawasilisha taswira moja wazi, kwamba si mwaminifu, na asiye mwaminifu hawezi kusimamia ofisi ya umma. Inawezekana sana hili ndilo tatizo letu kama taifa, kuwa na viongozi wasiosema ukweli.

Ukiwatazama Nape na Ridhiwani katika kauli zao, mtu hatakuwa amekwenda pembeni kama akifikia hitimisho kwamba utamaduni wa kusema uongo umeruhusiwa kuwa sehemu ya kuendesha mambo ndani ya chama tawala, na kwa kuwa kuna ruhusa ya kusema uongo, ni lini basi wananchi wanaweza kuamini kwamba yasemwayo na viongozi wao ni ya kweli?

0
Your rating: None Average: 3.7 (7 votes)
Soma zaidi kuhusu: