Uongozi shupavu umetoweka nchini


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version

TAIFA linakabiliwa na ombwe kuu la ushupavu wa uongozi hasa wakati wa matatizo.

Nchi inapokwa katika hali ya amani na furaha, kila mtu anaweza kuwa kiongozi. Lakini taifa linapokabiliwa na matatizo, kunahitajika kiongozi makini wa kuliongoza na kulivusha kutoka lilipo.

Kwa sasa, taifa linakabiliwa na orodha ndefu ya matatizo na bado wananchi hawaoni hatua madhubuti ambazo zinachukuliwa na watawala; ndiyo maana tunasema, “Taifa linakabiliwa na ombwe la uongozi.”

Ombwe likiachwa bila kushughulikiwa, mambo mawili yaweza kutokea.

Kwanza, anaweza kujitokeza kiongozi wa dharula, mwenye ushawishi, lakini usiopimwa wala kuaminika, akaliongoza taifa katika mwelekeo wa hatari.

Kiongozi wa namna hiyo anaweza kutumia shida na mkanganyiko kama vilivyopo sasa, kuvuna wafuasi na akaonekana machoni mwa wengi kuwa amesheheni busara.

Haya yamewahi kutokea katika mataifa kadhaa duniani, ikiwamo Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Msumbiji. Bila shaka, yanaweza kutokea hapa pia.

Pili, obwe la uongozi linaweza kujenga hofu kwa watawala na kuamua kuanza kushughulikiana wao kwa wao, na ndani kwa ndani. Lengo ni kuzuia matatizo yanayolikabili taifa kutoka nje.

Kwamba, badala ya kuruhusu matatizo kutoka nje ili kupata fursa ya kueleza wananchi kiini cha chake, wanaweza kutumia muda wao mwingi kumalizana.

Hata mahubiri ya viongozi wa dini ya kikristo katika mkesha wa Krismasi, yamejikita katika kukemea na kuonya hatari inayokabili taifa.

Mimbari za makanisa kila kona ya nchi, zilipambwa kwa mahubiri yanayoashiria kuwapo kwa ombwe la uongozi katika taifa.

Tuangalie tatizo kubwa la kuwapo kwa mgawo wa umeme, katika kipindi ambapo shirika la umeme la taifa (Tanesco) linakabiliwa na deni la mabilioni ya shilingi kutoka kampuni tata ya Dowans Holding Limited.

Tayari bei ya nishati hiyo imepanda hata kama haipatikani kwa walio wengi. Kuna taarifa kwamba ni asilimia kumi ya wananchi wanaotumia umeme nchini.

Hii ina maana kwamba hawa watumiaji wachache, ndiyo wanaobeba mzigo wa kuendesha shirika na ufisadi wake.

Kupanda kwa bei ya nishati ni ruksa rasmi ya kuendelea kukata miti ili kukidhi mahitaji ya nishati ya walio wengi. Hatua hii itaongeza kasi ya kuharibu mazingira na kuchangia mabadiliko ya tabia nchi.

Ombwe la uongozi kitaifa linaonekana wazi katika namna ya kutatua tatizo hili la kukosekana kwa umeme na adha ya mgawo usioisha. 

Hata madai ya katiba mpya, chimbuko lake ni kuwapo kwa ombwe la uongozi.

Wakati wananchi mbalimbali, wakiwamo viongozi wa kidini wakisisitiza kuwa suala la katiba mpya haliwezi kuepukika, mshauri mkuu wa rais – Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema – anaibuka katikati ya mjadala na kusema, “Hakuna haja ya kuwapo kwa katiba mpya.”

Baadhi ya wale wasiopenda kumuudhi “bwana mkubwa” kwa kumwambia ukweli, wanapenda kusingizia kuwa ombwe hili la uongozi linatokana na wasaidizi wa rais kumuangusha katika utendaji wake.

Watu hawa wanashindwa kutambua kuwa mfumo wa uteuzi kwa mujibu wa katiba ya sasa, unampa rais mamlaka yasiyochujwa na chombo chochote kile.

Ili kumpa rais umakini wa kutosha katika kuteua wasaidizi wake, katiba inatakiwa ichinje mamlaka hii ili lawama kwa wasaidizi na wateule wa rais ziende kwa mgawo kati yake, Bunge na wasaidizi wenyewe.

Hata suala la mfumuko wa bei ambao tayari unadhalilisha thamani ya shilingi, unaweza kuwa umesababishwa kwa kiasi kikubwa na ombwe la uongozi lililopo.

Kila unapopita, bei za vitu kadhaa imepanda. Gharama za elimu zimepanda, matibabu ziko juu, usafiri nao haushikiki, huku umaskini kwa wananchi ukizidi kuongezeka.

Imefikia hatua baadhi ya wananchi wanaona shilingi yetu haina thamani yoyote hali iliyofanya Gavana wa Benki Kuu, Beno Ndullu kutoa tamko la kusisitiza kuwa sarafu ni fedha halali.

Baadhi ya makanisa yamediriki kupiga marufuku utoaji wa sadaka kwa njia ya sarafu kwa sababu ni usumbufu kuhesabu fedha hiyo isiyo na thamani katika mzunguko.

Mpaka sasa, kutokana na ombwe la uongozi kushamiri, wananchi hawajapata maelezo yeyote kuhusu mfumuko huu wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi.

Ombwe pia limeonekana wazi katika medani za siasa. Baada ya uchaguzi, Rais Jakaya Kikwete aliasisi fikra potofu za kuaminisha watu kuwa CCM, kilipata ushindi mdogo kuliko mategemeo yake kutokana na udini ulioendeshwa na viongozi wa madhehebu.

Lakini tumesikia baadhi ya viongozi wa dini wakikemea fikra hizi katika mahubiri yao. Kuanzia Iringa, Arusha, Morogoro na Mbeya, wote waliozungumza wameeleza kuwa kiongozi anayeendekeza fikra za udini anajitangazia kushindwa uongozi.

Viongozi hao wamesema haiwezekani udini ambao haukuonekana katika awamu tatu zilizopita, uje kuibuka ghafla katika awamu hii ya nne na mwishoni mwa uchaguzi.

Kushughulikia matatizo ya kisiasa kwa kuongozwa na fikra za udini, ni kujaribu kuwapumbaza watu ili wasione ukweli wa matatizo yao. Bahati njema wananchi wanaona na wanaelewa.

0
No votes yet