Upinzani haujajijenga kuishinda CCM


John Kibasso's picture

Na John Kibasso - Imechapwa 01 September 2010

Printer-friendly version

KWAMBA Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitashiriki kumsukia zengwe mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) haiingii akilini mwangu.

Lakini ndivyo gazeti hili kipenzi cha wananchi lilivyoripoti katika moja ya makala zake kuu wiki mbili zilizopita.
Yawezekana yaliyosemwa yapo.

Lakini bado siamini kuwa viongozi wa CCM wangekuwa tayari kuacha kushughulikia maandalizi ya kufanikisha wanachama wao waliopitishwa kugombea pamoja na Mwenyekiti wao kurudisha fomu bali waanze kumhujumu Dk. Slaa.

Wafanye hivyo ili iweje? Kwa faida ya nani? Kwa uzoefu wangu wa uongozi, ingawa mimi si msemaji wa chama chetu, CCM hawawezi kujidhalilisha kwa mambo mepesi kama hayo.

Kwa muono wangu bila ya kuathiri fikra na mtizamo wa wadau wengine wenye mwelekeo chanya juu ya wapinzani, nasema washindani wa CCM bado hawajawa na mikakati madhubuti ya kuitoa kamasi.

Huwezi kuwa mpinzani wakati nyuma yako huna wafuasi wa kuaminika. Yawezekana ukawa nao, lakini wakawa si waaminifu. Ni heri kuwa na kundi dogo la wanachama wanaoaminika na kuheshimu itikadi ya chama chako, kuliko kuwa na kundi kubwa la watu wasiokuwa na maadili.

Tatizo kubwa la wapinzani wa CCM ni kukosa takwimu sahihi za wanachama wao waaminifu ambao wana uhakika kwamba hata chama kingine kikitumia hila au ulaghai wa aina yoyote hawatageuka na kusaliti chama.

Tuchukue mfano wa CCM, pamoja na ukubwa na ukomavu wake, mpaka leo wanayo idadi ndogo tu ya wanachama takribani milioni tano ambao kwayo wako tayari kufa kwa kutetea, kulinda na kusimamia itikadi ya chama hicho.

Chama chochote makini duniani kina aina mbili za makada. Kuna makada wa chama ndani ya chama na wapo makada wa kisiasa ndani ya chama. Kundi la kwanza, huwa ni watu wachache lakini tegemeo muhimu kwa chama.

Wanakuwa imara kiitikadi na kusimamia miiko na maadili ya wanachama kutetea, na kulinda uhai wa chama katika pilikapilika za ndani zinazoweza kufanya chama kisitawalike kiitikadi.

Makada hawa huwamo waasisi na vijana waliopikwa kwa madhumuni ya kuendeleza muongozo, dira na maslahi ya chama. Wamepevuka na wana wajibu wa kulinda heshima ya chama.

Kwa wale makada wa kisiasa ndani ya chama, kazi yao kuu ni propaganda, uenezi na utetezi wa chama dhidi ya mbinu za wapinzani wake wakati wa uchaguzi. Wanakuwa tayari kupika majungu, hujuma na hila zozote ili chama chao kishinde.

Bali hawa huwa hawadumu kwenye chama maana ni wepesi kurubuniwa na kuhamia chama kingine. Rahisi kuwaita wanachama mamluki.

Kwa bahati mbaya utafiti na uchambuzi wa weledi wa siasa umebaini kuwa vyama vya upinzani vinakosa makada wa aina ya kwanza kwani wote hawajalelewa katika misingi ya chama chao.

Hakuna wanaoguswa na itikadi ya chama. Hakuna walio tayari kufa kukifia chama chao. Wanachama wa upinzani wengi ni makada wa kisiasa ambao ikifika siku ya kupiga kura, wanakosa ujasiri na nguvu za ushawishi kwa chama chao.

Mara moja hurubuniwa na vyama vingine na hatimaye kugeuka misimamo. Hawa ndio wanachama mamluki.

Vyama vya upinzani vinaonekana visivyoaminiana. Hubaki kutupiana lawama. Hapo nani wa kulaumiwa kama siyo wenyewe vyama vya upinzani?

Kuna kosa gani wakitumia upungufu huo ili kuwazidi kete? Huwezi kulaumu viongozi wa CCM kwasababu hawajaajiriwa kufundisha wapinzani siri ya kushikamana.

Hata Mwalimu Nyerere alipotambua kuwa Chama cha TANU baada ya kupata uhuru kilikuwa hakijawa na viongozi waliopevuka na kusilimu kwa kutetea itikadi ya chama, aliamua kumuachia nafasi ya uwaziri mkuu mzee Rashid Mfaume Kawawa.

Alitaka kujipa nafasi ya kuunda na kujenga chama upya chenye viongozi wanaotii miiko na kufuata maadili ya uongozi. Mwalimu alijua kuongoza chama kisicho wanachama waaminifu na waadilifu kutakiondoa madarakani haraka.

Hali hii ya kuongoza chama kisichokuwa na dira wala mwelekeo kwa wanachama wake ndiyo iliyowafanya makada mashuhuri wa nchi nyingi barani Afrika kung’olewa mapema.

Baadhi yao ni Dk. Patrice Lumumba (wa iliyokuwa Zaire); Kwame Nkrumah (Ghana), Agostino Netto (Angola) na Sekou Ture (Guinea).
Hawakujali kuandaa wanachama wao mapema na matokeo yake, vyama vyao vikang’olewa au wao wenyewe kuuawa mapema.

Ingali vigumu vyama vya upinzani Tanzania kuing’oa CCM madarakani. Kikwazo ni kukosa mbinu za kujenga makada wao bali kilicho mbele kwao ni kufikiria tu kuikwapua CCM utawala.

CCM wana uhakika na ushindi ngazi ya urais kwasababu kiongozi wao hajakurupuka tu, aliandaliwa na chama. Jakaya Mrisho Kikwete anajua umuhimu wa nafasi yake kichama.

Aliandaliwa na UV-CCM akawa kada aliyepevuka, mwadilifu na mwaminifu. Ndio maana anaaminika kama mtaji wa chama.
Kwa vyama vya upinzani, ni nadra kuwapata waasisi wa aina ya Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa tayari kuacha nafasi kubwa ya uwaziri mkuu ili kwenda kuimarisha chama hata bila ya kuwa na uhakika wa maslahi yake.

Waasisi wa vyama hivi pamoja na viongozi wao, hawana damu ya chama miilini. Wote walikuwa CCM. Kwa mfano Dk. Slaa alikuwa mwanachama wa CCM hadi alipokatwa jina lake mwaka 1995 ndipo akahamia CHADEMA.

Kama yeye kama wenzake katika CHADEMA na vyama vingine. Sasa utategemea nini kwa viongozi wa vyama upinzani katika wakati wa uchaguzi zaidi ya kulalamika tu bila ya kutambua chanzo cha vyama vyao kushindwa?

Mwandishi wa makala hii ni mwanamageuzi anayepatikana kwa simu namba 0713/0767 399004.
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: