Upo wakati walimu hunyenyekewa


Ramadhani Kingi's picture

Na Ramadhani Kingi - Imechapwa 09 December 2009

Printer-friendly version

NINAKUSIFU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe kwa ustadi wako na uthubutu wa kutoa kauli zinazovunja moyo walimu nchini.

Sijaelewa hasa kama ulikusudia kama Kiingereza ni elimu na elimu ni Kiingereza. Kweli Mswahili hakukosea kwa falsafa yake, “Shibe mwana malevya, njaa mwana malegeza.”

Umeitoa kauli wakati bado hatujasahau nyingine ya kuudhi aliyoitoa naibu waziri wako, Mwamtum Mahiza alipotamkia walimu kwamba “wale wanaoona wamechoka kazi ya ualimu basi bora watafute kazi nyingine ya kufanya.” Kisa, kuuliza mipango ya serikali kuinua maslahi ya walimu.

Si walimu wote wanaoweza kupata kazi ya ubunge maana asilimia 47 ya wafanyakazi wa serikali ni walimu. Isitoshe ubunge si taaluma aliyosomea hivyo pangapangua atabaki ni mwalimu mtaalam na mbobea taaluma ya vipofu, mabubu na viziwi.

Ila huko uliko waziri na naibu wako, ni kwa muda tu na hutegemea takrima kwa sisi walimu ili mkufike. Uwaziri hauhitaji digrii.

Lakini nieleze kwa sasa, ulionao si walimu safi bali wachafu. Umeshaaminisha Watanzania walimu ni watu ovyo wanaoghushi ili kujinufaisha kimalipo. Hivi kama umekuwa na walimu hao na hawajui Kiingereza, si ujiuzulu ili kuepuka kufedheheka.

Wizara unayoongoza imekuwa ikituhumiwa Aprili ililipa walimu hewa Sh. 3.4 bilioni. Sijaingiza zile Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, alizosema walimu wameghushi.

Haishangazi hamkushituka kwani watendaji wako wizarani ndio wanaoandaa na kulipa malipo hayo. Mwalimu gani anaandaa malipo? Yupi anayaidhinisha na kulipa?

Hatukumsikia CAG Utouh wakati huo akilalamikia kughushi kama afanyavyo sasa, kitendo kinachoporomosha morali wa kazi. Labda ndio aina nyingine ya mbinu na kampeni ya kupembeuka tatizo halisi la ufisadi kwa watendaji mnaowajua ili jamii wageuke sasa na kuanza kuwatuhumu wale unaowaongoza.

Mhariri wa MwanaHALISI (Toleo Na. 161) alionyesha njia aliposema, “…serikali zisizopenda kusikiliza maoni ya wananchi (public opinion) hutumia mbinu ya kuzua jambo katikati ya mjadala muhimu unaoendelea. Ni ulaghai kwa wananchi kutaka wageukie hilo na kusahau lile zito zaidi linalowahusu.”

Profesa umenukuliwa ukisema walimu watakaogoma utawafukuza kazi bila kujali uhaba utakaotokea nchini. Hakika ukitimiza hilo, utakuwa umepunguza ufisadi na kufuta hatia za kughushi kama CAG alivyoainisha ndani ya wizara yako.

Hapo utabaki peke yako kwani uprofesa haupatikani bila walimu. Vivyo hivyo elimu maalum, haipatikani Benki Kuu.

Mara kadhaa tumeisikia serikali ikiahidi kulipia wafanyakazi wa reli (TRL) wanapogoma; serikali hiyohiyo imelipa wakazi wa Kipawa waliposogelea mkate wa Ikulu; serikali ikalipa watu wa mgodi wa Kiwira walipomgusa mtu aliyesema Watanzania ni wavivu wa kufikiri.

Ni bahati mbaya sana hata mzee vijisenti hakuthubutu kuwafukuza watu wa gari moshi walipolikimbia gari Dodoma. Hakuwatuma watu wa Segerea wala Keko, wale walioacha gari Dar es Salaam. Mara zote tumeiona serikali ikisalimu amri, huku ikitingisha mkia mbele yao ikiahidi kuwalipia bila kuchelewa.

Profesa unamkumbuka yule aliyewafananisha Waingereza katikati ya miaka ya 1960 na mbwa kibogoyo aliyekuwa mahiri kwa kuchezeshachezesha mkia mbele ya meza yao wale?

Walimu si kitu ila ufike wakati wa uchaguzi. Licha ya kutojua kwao Kiingereza, wanakuwa lulu na dhahabu. Ni wao wanaosakamwa na wananchi kuwa wameiba kura kunufaisha wakubwa.

Hapa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali huwa hapamhusu. Hubaki wakipewa sifa kemkem za ukokwa. Huondolewa kada ya manokoa na kuogelea katika dimbwi la sifa za uheshimiwa.

Hudanganywa na pipi za mti, vifulana, vikofia na kubebwa tayari kuwaandalia ulaji wewe na waheshimiwa wenzako Profesa. Lugha za manyanyaso huzikwa, kebehi hupumzishwa na kiinimacho hubebwa kwa mbeleko za waheshimiwa.

0
No votes yet