Urais mchezo wa karata tatu


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 10 November 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

MCHEZO wa karata tatu huwa haumaliziki salama. Wachezeshaji, wanapoona wanazidi kuliwa hulazimisha ushindi.

Kama aliyecheza ni wakuja yaani hausigeli au shambaboi, basi ataishia kulia, lakini kama ni mtoto wa mjini, utazuka ugomvi na wachezeshaji hutoroka na fedha. Ole wako uwafuate vichochoroni.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imegeuza uchaguzi mkuu mwaka huu kuwa mchezo wa kamari ya karata tatu. Kilichotokea ni hiki NEC ilitoroka na matokeo hadi Karimjee ikamtangaza mshindwa kuwa mshindi. Ole aliyeshindwa apinge matokeo!

NEC ilianza kutengeneza mazingira hayo katika Datfari la Kudumu la Wapigakura ikidai waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 20,137,303.

Ukweli wa kihistoria hakuna mwaka wa uchaguzi mkuu ambapo kulikuwa na ongezeko la watu milioni tano, maajabu ni mwaka 2005 na 2010.

Kabla ya uchaguzi mwaka 1965, Mwalimu Nyerere akafuta mfumo wa vyama vingi ikabaki Tanganyika African National Union (TANU). Waliojiandikisha walikuwa 3,373,089; watu 2,600,040 (77.1%) walipiga kura. Nyerere alipata kura 2,410,903 (96.46%), watu 88,600 (03.54%) walimkataa na kura 100,537 ziliharibika.

Mwaka 1970 wapigakura walikuwa 5,051,938. Nyerere alishinda kwa kura 3,465,573 (72.2%), kura 109,828 (03.07%) zilimkataa na 74,388 ziliharibika.

Mwaka 1975 wapigakura walikuwa 5,577,566. Kati ya hao waliomchagua walikuwa 4,172,267 (93.25%), kura 302,005 (06.75%) zilimkataa na kura 83,323 ziliharibika.

Mwaka 1980 wapigakura walikuwa 6,969,803 na kati ya hao 5,570,883 (95.56%) walimpigia Nyerere kura za ndiyo na chama chake Chama cha Mapinduzi (CCM), kura 259,040 (04.44%) zilimkataa na kura 157,019 ziliharibika.

Mwaka 1985 Alhaji Ali Hassan Mwinyi aliteuliwa kuwa mgombea urais baada ya Nyerere kustaafu. Mwaka huo watu 6,910,555 walijiandikisha.

Watu 4,778,114 (95.68%) walimpa ushindi, 215,626 (04.32%) walimkataa huku kura 188,259 zikiharibika.

Mwaka 1990, waliojiandikisha walikuwa 7,296,553 na kati ya hao 5,198,120 (97.79%) walipiga kura za ndiyo, kura 117,366 (02.21%) zilimkataa na 109,796 ziliharibika.

Mwaka 1995 kulikuwa na hamasa kubwa nchini baada ya kurejeshwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Hata hivyo, waliojiandikisha walikuwa 8,929,969.

CCM ilipata ushindani kutoka vyama vipya vya siasa vilivyoanzishwa kama NCCR-Mageuzi, CHADEMA, CUF, TLP, NLD, Tadea, UMD.

Benjamin Mkapa wa CCM alishinda kwa kura 4,026,422 (61.82%), Augustine Mrema wa NCCR- Mageuzi kura 1,808,616 (27.77%) na Ibrahim Lipumba wa CUF kura 418,973 (6.43%) huku John Cheyo wa UDP akipata 258,734 (3.97%). Kura 333,936 ziliharibika.

Mwaka 2000 waliojiandikisha walikuwa 10,088,484 ongezeko likiwa watu karibu 1.2 milioni ikilinganishwa na mwaka 1995.

Mkapa alirejeshwa madarakani kwa kura 5,863,201 (71.74%), Lipumba akapata kura 1,329,077 (16.26%), Mrema wa TLP alipata kura 637,115 (7.80%) na Cheyo kura 342,891 (4.20%), kura 345,314 ziliharibika.

Maajabu NEC ilidai mwaka 2005 walijiandikisha watu 16,401,694 yaani eti waliongezeka wapigakura milioni sita.

Walilotaka likawa. Jakaya Kikwete wa CCM akashinda kwa kura 9,123,952 (80.28%)! Lipumba aliishia na kura 1,327,125 (11.68%), Freeman Mbowe wa CHADEMA kura 668,756 (5.88%), Mrema kura 84,901 (0.75%).

Waliopigakura walikuwa 11,875,927 (72.4%), kura 510,460 ziliharibika huku watu wapatao milioni tano wakikosa kupigakura.

Wakati idadi ya mwaka 2005 ikitiliwa shaka, mwaka huu NEC wakaja na idadi inayotatanisha. Awali walidai kuwa walikuwepo wapigakura zaidi ya milioni 21 lakini baada ya kurekebisha kwa kuondoa waliokufa na wale waliojiandikisha mara mbili, idadi ilibaki 19.6milioni.

Kwa hiyo Watanzania waliingia kwenye uchaguzi mkuu wakijua wapigakura wako 19.6milioni. Nini kimetokea NEC idai wapigakura walikuwa 20,137,303? Idadi hii mpya imetoka wapi? Hivi hakukuwa na ulazima wa kuwaeleza wagombea kwamba idadi kamili ni hiyo?

Kwa kuwa NEC inasema wapigakura 8,626,283 (42.8%) ndio waliojitokeza, watu 11,511,020 (57.2) ambao inataka watu waamini hawakujitokeza kupiga kura ni usanii; kwa kufuata mtiririko huo tangu mwaka 1965 wapigakura hawakufika milioni ishirini.

Je, Rais Kikwete atapita akijiamini kuwa ni mjenzi wa demokrasia? Kwamba mchezo wa kuomba kura kwa helkopta tatu, kuweka sura kila kona, kujitangaza kwenye luninga na opena zikiimba sifa zake unaishia kuwa wa kamari ya karata tatu?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: