Urais ngoma nzito kwa Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 29 April 2008

Printer-friendly version
Wabia wake wamekuwa na nguvu kuliko yeye
Ameendelea kuwabeba mawaziri wenye tuhuma
Rais Jakaya Kikwete

SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete imechukuliwa na msukule. Wananchi wanajiuliza: "Mbona urais kwa Kikwete umekuwa mgumu kinyume cha matarajio yao?"

Ni miaka miwili na nusu imepita tangu Kikwete aingie madarakani, lakini hakuna mwenye uhakika Kikwete anaelekea wapi!

Inavyoonekana ni kama vile Kikwete anatembea gizani kwa kupapasa njia. Wengine wanasema hajui hata aendako.

Ukiangalia matendo ya serikali yake, huwezi kupata jibu kwa haraka juu ya uwezo wa Kikwete wa kustahamili vishindo vya urais.

Kila mara Kikwete amekuwa akishindwa kuuleza umma hali ya 'uhovyo' inayojitokeza ndani ya serikali yake. Hali hiyo huzidishwa zaidi na maamuzi yake yasiyokuwa makini na hatua anazochukua kukabiliana nayo.

Kila kukicha, utasikia kadhia hii au ile imeibuka ndani ya serikali yake, huku msemaji wake, Salva Rweyemamu, akijitahidi kupotosha umma.

Kwa mfano, wakati Andrew Chenge anajiuzulu uwaziri wa miundombinu majuzi, Salva alisema hatua hiyo ya Chenge ni kitendo cha kijasiri na kinaonyesha serikali ilivyo makini katika kutenda kazi zake.

Nilipomsikia Salva akizungumza maneno hayo, mara moja nilimkumbuka aliyekuwa Waziri wa Habari katika utawala wa Saddam Hussein, Mohammed Al-Sahaf.

Huyu anakumbukwa jinsi alivyokuwa bingwa wa propaganda ndani ya serikali ya Saddam Hussein. Hata pale ilipofahamika na kila mmoja kwamba majeshi ya Marekani na washirika wake tayari yameuzingira mji wa Baghadad, bado Al-Sahaf aliendelea kung'ang'ana kukana jambo hilo.

Kwa upande wa Salva, pamoja na kwamba kila mmoja anajua kuwa Chenge hakustahili kuwamo katika Baraza la Mawaziri, bado analeta porojo za "umakini wa serikali."

Kuwa taaluma aliyo nayo, na kwa umahiri tunaoujua kwa Salva, ni dhahiri kwamba naye anajua kwamba utetezi anaoipa serikali unaitokomeza.

Hii inatokana na ukweli kwamba maamuzi ya hovyo ya Kikwete ndiyo yaliyochangia kutokea hali hiyo.

Maana kama Kikwete angekuwa makini katika kutenda kazi zake, asingewafikiria watu kama Chenge tangu mwanzo. Na alipopata fursa ya kuunda upya baraza hilo, asingemrejesha.

Tuhuma za Chenge zinajulikana hata kwa watoto wa darasa la sita. Ni yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, aliyesimamia, au kushauri serikali katika kuingia mikataba karibu yote nchini.

Kuanzia mikataba ya madini, migodi, mashamba, viwanda, ununuzi wa rada ya kijeshi, ndege mbovu ya rais, uuzaji wa benki ya taifa (NBC), na hata ule wa ugawanyaji nyumba za serikali.

Yote haya yalifanywa kwa baraka za Chenge na watendaji wengine wa serikali ambao baadhi yao Kikwete amewakumbatia mpaka sasa. Kama mwanasheria mkuu alipaswa kuishauri serikali isijiingize kwenye mikataba isiyo na maslahi. Hakufanya hivyo. Ni dhahiri Salva analijua jambo hili.

Ukiacha tatizo la uhalifu wa kutumia silaha, ambao lilitikisa serikali ya Kikwete katika siku zake za kwanza, hakuna jingine ambalo Kikwete anaweza kujivunia kuwa imelishughulikia kikamilifu.

Kwa mfano, Kikwete hawezi kujitapa kuwa ameshughulikia tatizo la njaa nchini lililotokea mara baada ya yeye kuingia madarakani.

Hii ni kwa sababu Kikwete anajua, kama sote tujuavyo, kwamba tatizo la uhaba wa chakula katika taifa hili, halikusababishwa na ukame pekee yake.

Lilichochewa zaidi na kukosekana kwa uadilifu na uaminifu kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara na watumishi wa serikali.

Baadhi ya makampuni yaliyopewa kazi ya kusambaza chakula cha njaa, hayakufanya kazi hiyo kama ilivyokusudiwa.

Hata hivyo, pamoja na matatizo hayo, hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi wa serikali wala makampuni husika.

Hii ni kwa sababu, miongoni mwa makampuni yaliyopewa kazi hiyo, baadhi yao yanatajwa kuwa yanamilikiwa na marafiki wa rais. Mengine yanadaiwa yalifadhili kampeni za uchaguzi za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Matokeo yake, badala ya serikali kuleta chakula cha njaa ili kuokoa maisha ya wananchi wake, imeishia kutoa "sadaka" fedha za umma na zile za wafadhili.

Hata Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Chakula nchini (FACF), Dk. Lorri Willibard, anathibitisha hilo.

Anasema baadhi ya wafanyabiashara waliochotewa fedha kwa lengo la kusambaza chakula cha njaa, hawakufanya kazi waliyotumwa.

Ukiacha uhaba wa chakula, tatizo la ukame, lilikausha pia mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kihansi, Mtera na Kidatu.

Hapo ndipo wasaidizi na marafiki wa rais walipopata nafasi ya kuotesha kama uyoga makampuni ya kitapeli, ikiwamo Richmond Development Company.

Kwa makusudi, huku wakijua kwamba Richmond ni kampuni ya kitapeli, watendaji wa serikali waliikingua kifua kampuni hiyo na kuipa kazi.

Ndiyo chanzo, au kichocheo cha serikali kushikwa na kigugumizi na kushindwa kusitisha mkataba wake na Richmond na dada yake Dowans.

Serikali inafanya hivyo huku ikiwa na uhakika usio na shaka, kwamba Richmond si kampuni, bali kundi la matapeli waliojikusanya kukamua uchumi wa nchi kwa maslahi yao binafsi.

Na hili linathibitishwa na kauli na matendo ya Kikwete mwenyewe. Kwa mfano, mpaka sasa Kikwete hajasema kinagaubaga kwa nini alibadilisha hotuba yake aliyotaka kuitoa siku ya UKIMWI duniani, mjini Musoma, mkoani Mara.

Katika hotuba hiyo, ambayo tayari ilikuwa imesambazwa kwenye vyombo vya habari, Kikwete aliishutumu Richmond na kueleza jinsi asivyoridhishwa na utendaji wake.

Lakini badala ya kuifikisha kwa wananchi kama alivyoiandaa na kuisambaza kwa vyombo vya habari, Kikwete akachonga kitu kingine na kukipeleka kwa wananchi.

Katika "mchongo huo mpya" rais hakugusia hata chembe mkataba kati ya serikali na Richmond. Hii ni kutokana na kile wengi walichosema, "ameshindwa kushambulia marafiki zake waliojipachika utatu mchafu ndani ya serikali yake."

Ni utatu huu, ambao unadaiwa kuwa ulikuwa unaundwa na Edward Lowassa, Rostam Aziz na Nazir Karamagi.

Hakika, mungu anawapenda Watanzania. Maana bila ya kupinduliwa aliyekuwa waziri mkuu wa Thailand, Thaksin Shinawatra, mwishoni mwa mwaka jana, Lowassa alikuwa tayari analeta "Richmond" nyingine.

Hii ni ile iliyotokana na mpango wake wa kuleta wataalam wa kutengeneza mvua ambapo Watanzania waliupachika jina la "mvua za Sumbawanga."

Kutokana na hali hiyo, haikutarajiwa kwa Rais Kikwete, kumpeleka Karamagi katika wizara ya Nishati na Madini, baada ya kufanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri mwisho mwa mwaka juzi.

Maana kama ilivyo kwa Lowassa, Karamagi hana ubavu wa kupindisha maamuzi ya serikali, ama kuamua vinginevyo kwa maslahi ya Rostam.

Lakini ukweli unabaki pale pale, kwamba tatizo kubwa alilonalo Kikwete, ni kushindwa kutumia fursa anazozipata kurekebisha serikali yake.

Mifano ipo mingi. Ni Kikwete aliyemrudisha Chenge katika nafasi yake. Baada ya miezi miwili, hatimaye Chenge akalazimika kuondoka ili, kama alivyosema baadaye, "kumsaidia rais."

Bila shaka wapo wengine, watamfuata Chenge. Na kama Kikwete hakufunua shuka na kutoka usingizini, atalazimika kubadili baraza la mawaziri kila mwezi.

Na hili linathibitishwa na hatua ya Kikwete ya kumuacha katika baraza lake, Lawrence Masha, ambaye naye kama Chenge analalamikiwa kwa mengi.

Naye anasemwa yumo katika kapu la Richmond. Ndiye aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, wakati mkataba wa Richmond unasainiwa.

Ni huyu ambaye anatajwa kuwa aliwahi kuwa mkurugenzi wa kampuni ya Tanzanite One inayochimba madini mkoani Arusha.

Amekuwa mkurugenzi katika kampuni yake ya uwakili ya IMMA Advocates iliyotumiwa na wajanja kusajili na hatimaye kufilisi kampuni ya kitapeli ya Deep Green Finance Limited.

Hii ni moja ya kampuni zilizochotewa na serikali kutoka Hazina kupitia Benki Kuu (BoT) mabilioni ya shilingi.

Ni Deep Green hii, ambayo imeweka historia katika mambo ya benki baada ya kufungua akaunti yake siku ya Mei mosi.

Lakini badala ya Kikwete kumwondoa, amempandisha na kumfanya waziri kamili katika wizara nyeti ambayo inatakiwa kusimamia usalama, sheria na haki za wananchi.

Sasa swali la kujiuliza: Masha atapata wapi uwezo na ujasiri wa kukemea polisi wanaotuhumiwa kufanya mauaji katika maeneo ya migodi?

Ataanzia wapi wakati yeye ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni inayopambana na wachimbaji wadogo maarufu kama Wana-Apolo, wanaolalamika kudhulumiwa maeneo yao?

Hali inayomkumba ya mgongano wa kimaslahi, ni kama ile inayompata Karamagi katika sakata la kampuni yake ya upakuaji na upakiaji wa mizigo bandarini (TICTS).

Haijulikani wazi Kikwete "amelishwa" nini na Masha hadi kuendelea kumng'ang'ania. Lakini kinachofahamika ni "uhusiano wa kindugu" kati ya mtoto wa Kikwete, Ridhiwani na Masha.

Ni wazi kwamba yote haya yanatokea kutokana na Kikwete kutoangalia mbali na kujua hisia za wananchi wake.

Kama angekuwa anapima alama za nyakati, kamwe rais Kikwete asingeweza kuwaingiza katika baraza lake la mawaziri wanasiasa kama vile, Basil Mramba, Bakari Mwapachu, Joseph Mungai, Athumani Kapuya na Kingunge Ngombale-Mwiru.

Ndiyo maana kwa udhaifu huo wa Kikwete, Chenge mara aliporudishwa katika baraza la mawaziri, Februari mwaka huu, mara moja alisema, "muulizeni rais aliyeniteua."

Wapo wanaosema kwamba sababu ya mambo haya ni Kikwete kufadhiliwa na wafanyabiashara ambao sasa ndiyo wanaomharibia.

Wakati wa kinyang'anyiro cha urais, wapambe wa Kikwete waliweza hata kubadilisha utaratibu wa kampeni ndani ya chama chake.

Badala ya kampeni hizo kufanywa na chama, Kikwete na kundi lake walijikusanya na kuratibu wenyewe shughuli nzima za kampeni. Inafahamika hata ofisi ya uratibu wa kampeni hizi haikuwa ya CCM makao makuu.

Matokeo yake, lawama na tuhuma kutoka ndani na nje ya chama, kwamba Kikwete inawezekana ameingia madarakani kwa fedha chafu, zinapamba moto kila kona.

Ndiyo maana dira na mwelekeo wa serikali yake umepotea. Maana wengi wanaoteuliwa, hawana uwezo wa uongozi na kutetea serikali, badala yake wamekuwa mabingwa wa hadaa na mikakati ya kujitajirisha.

Si hivyo tu, uteuzi wake wa sasa umeiongezea serikali mzigo wa gharama baada ya zoezi hilo kufanywa kwa pupa.

Mpaka sasa ikiwa ni zaidi ya miezi miwili, haijulikani nafasi ya baadhi ya makatibu wakuu, manaibu, wakurugenzi na makamishina katika wizara zilizounganishwa.

Kwa mfano, bado watu wanahoji nafasi ya katibu mkuu katika iliyokuwa wizara ya Usalama wa Raia, ambayo sasa imeunganishwa na kuitwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi.

Pamoja na kwamba watumishi hawa wa umma wanaendelea kulipwa mishahara, lakini haijulikani wanafanya kazi gani. Ni dhahiri wananchi hawakosei wamaposema Kikwete hajui aendako.

Siku wanahabari walipomuuliza kama ana habari kwamba urais wake una wabia wengi, alikana akasema hana ubia na mtu isipokuwa Dk. Ali Mohammed Shein.

Hata hivyo, utendaji wa Kikwete unatuonyesha wabia wake ni kina nani. Shein analazimika tu kuwa mbia wa rais kwa mujibu wa katiba, lakini hawezi kuwa kigingi cha maamuzi ya rais kama hawa watu wake wa karibu, wafadhili na wawezeshaji wa chama walivyo.

Licha ya hizi propaganda tunazosikia watu wake wakisukuma kwenye vyombo vya habari kumsafishia njia, hakuna dalili kwamba Kkwete atarejea mstarini. Urais umekuwa mzigo mzito kwake, na sisi ndio tunaoumia.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: