Urais Zanzibar waitafuna CUF


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 04 January 2012

Printer-friendly version

MGOGORO unaofukuta kati ya katibu mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad na mbunge wa Wawi, kisiwani Pemba, Hamad Rashid Mohamed, chimbuko lake, ni mbio za urais wa Zanzibar mwaka 2015, imefahamika.

Taarifa za ndani ya chama na serikali mjini Zanzibar, zinasema Hamad Rashid anataka kugombea nafasi hiyo baada ya kuelezwa kuwa Maalim Seif hatogombea tena urais wa visiwa hivyo.

Mtoa taarifa wa MwanaHALISI anasema, wakati Hamad Rashid akijizatiti kutaka kuwania nafasi hiyo, Maalim Seif kwa ushirikiano wa Ismail Jussa Ladhu, naibu katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar, wamejizatiti kuweka mtu wao.

“Nakuhakikishia ugomvi wote huu, ni urais wa Zanzibar mwaka 2015. Hamad Rashid anataka kujitosa kuwania urais, lakini Maalim na Jussa tayari wameandaa mtu wao. Hii ndiyo sababu ya mvutano ulioibuka,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi wa CUF ambaye hakutaka kutajwa gazetini.

Haijafahamika mara moja, iwapo Maalim Seif atagombea urais wa Muungano au atastaafu siasa za ushindani.

Anayetajwa kuwa chaguo la Maalim Seif na Jussa kwenye urais wa Zanzibar, ni kiongozi mmoja mwandamizi visiwani humo anayefanya kazi kwenye serikali ya Muungano. Gazeti hili linalihifadhi jina lake kwa sasa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu waliokaribu na Maalim Seif, Jussa, Hamad Rashid na viongozi waandamizi kwenye serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar, kinachowasukuma wanasiasa hao wawili waliokuwa marafiki wa karibu, waliojitoa kuijenga CUF, ni urais wa visiwa hivyo.

Wakati Hamad Rashid amekuwa akifikiria kupata idhini ya chama hicho ili kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao, akianzia na kukamata nafasi ya katibu mkuu anayoishikilia Maalim Seif, nafasi hiyo inaonekana ametengewa “mtu mahsusi.”

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja wiki moja baada ya gazeti hili kuanika mawasiliano kati Maalim Seif na Profesa Ibrahim Lipumba juu ya umuhimu wa “chama kufanya uamuzi mgumu wa kumfukuza uwanachama Hamad.”

Mawasiliano kati ya viongozi hao, yalinakiliwa kwa Julius Mtatiro, naibu katibu mkuu Tanzania Bara na Jussa.

Katika moja ya andishi lake, Maalim Seif anasema, “Tayari ushahidi wa kutosha umekusanywa na idara ya usalama dhidi ya Hamad, Doyo na Shoka na kwamba sharti Hamad afukuzwe ndani ya chama… Jamaa yako kama anataka kwenda CHADEMA (Chama cha Demokrasia na Maendeleo) ili akawe mgombea mwenza mwache aende…”

Anasema, “KUT ichukue uamuzi mgumu wa kuwasimamisha uongozi vinara wao na wengine kupewa karipio,” anaeleza Maalim katika mawasiliano yake na Profesa Lipumba.

Vyanzo vya taarifa vimesema Maalim Seif amekuwa akimtumia Jussa, kuhakikisha hakuna mtu anayekaribia mazingira ya kuteuliwa na chama hicho, isipokuwa “mtu wao.”

“Pengine huyu mheshimiwa HR (Hamad Rashid) anaposema Maalim Seif kwa kumpa nafasi kubwa Jussa inayoweza kumpeleka mpaka kuwa katibu mkuu wa chama, hakika hajakosea. Ameshajua kuna mtu ameandaliwa kuja kugombea urais kupitia CUF. Naye anataka nafasi hiyo, hivyo ameamua kupambana mapema kuhakisha analinda maslahi yake,” amesema mtoa habari mmoja.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa kauli hiyo, mtoa taarifa alisema, “Haya mambo yanafahamika vizuri serikalini na kwa watu waliokaribu na Jussa.”

Habari zinaeleza hatua ya Maalim kuacha kugombea tena nafasi hiyo inatokana na kile wachambuzi wanaita, “kukamilisha ajenda ya kuleta umoja na mshikamano visiwani,” na kwamba anataka kuachia madaraka kwa heshima.

“Maalim bado anakubalika. Pamoja na umri wake kuwa mkubwa, lakini bado ana nguvu. Ukakamavu wake kama mwanasiasa bado haujabadilika sana, ingawa kwa sasa, si yule wa miaka mitatu iliyopita, ambaye alikuwa anaweza kuikosoa serikali na kuitisha,” ameeleza.

Hamad Rashid ni mmoja wa viongozi 14 wa chama hicho wanaosubiri hatima yao baada ya kutuhumiwa kuendesha kampeni za kumg’oa Maalim Seif kwenye nafasi yake ya katibu mkuu.

Wengine wanaosubiri hatima yao, ni Doyo Khassani Doyo, Amir Kirungi na mbunge wa zamani wa Micheweni Pemba, Shoka Khamisi Juma.

Wengine, ni Juma Said Saanani, Yasin Mrotwa, Mohamed Albadawi, Doni Waziri, Mohamed Masaga, Yusuf Mungiro, Ahmed Issa, Tamim Omar, Ayub Kimangale na Haji Nanjase.

Mashitaka ya Hamad Rashid na wenzake yaliwasilishwa kwenye kikao cha kamati ya utekelezaji kilichofanyika mjini Uguja, 30 na 31 Desemba 2011. Mashitaka yote ambayo Hamad Rashid ameshitakiwa yaliandaliwa na kamati ya nidhamu na maadili ya chama, ambapo mwanasiasa huyo aligoma kuhojiwa.

Inaelezwa kuwa Hamad Rashid alitoa sababu tatu za kugoma kuhojiwa. Kwanza, Hamad ananukuliwa akieleza ndani ya kikao hicho kuwa kamati ya nidhamu imeundwa kinyume na katiba ya chama.

Pili, mkuu wa kamati hiyo (Khamisi Khassan) ndiye aliyeandaa alichokiita mashitaka bandia dhidi yake; na tatu, makamu mwenyekiti wa chama hicho, Khamisi Machano Ali, pamoja na wajumbe wengine watano ni sehemu ya wale wanaomtuhumu.

Ndani ya kikao cha kamati ya nidhamu, taarifa zinasema baadhi ya watuhumiwa waliokubali kuhojiwa, pamoja na kujibu tuhuma zilizokuwa zinawakabili, walieleza tuhuma moja baada ya nyingine kuhusu Maalim Seif, Jussa, Mtatiro na Machano mwenyewe.

Kwa mfano, taarifa zinaeleza, mmoja wa watuhumiwa Kirungi, alimtuhumu Mtatiro kuwadanganya viongozi wa chama kwamba yeye (Kirungi) alikuwa miongoni mwa wanachama wa chama hicho waliokuwa mkoani Tabora kumchafua mwenyekiti Lipumba na kufitinisha wanachama na viongozi.

“Mle ndani…Kirungi alitoa ushahidi wa kutosha kuonyesha hakuwa Tabora kwa muda wa wiki mbili. Alitoa hati ya kusafiria na tiketi ya safari kuthibitisha kuwa alikuwa nchini Comoro. Nakuambia ndugu yangu, ilikuwa aibu ya mwaka,” ameeleza mjumbe mmoja wa kamati ya nidhamu kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Kirungi amenukuliwa na mtoa taarifa akisema, “Anayeleta yote haya ni Mtatiro. Huyu ndiye aliyeniambia kuwa Maalim Seif ndiye aliyezuia maandamano yetu ya kupeleka rasimu ya katiba serikalini baada ya kuongea na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.”

Anasema, “Nikamwambia Mtatiro, hiki chama mnakiua. Inaonekana Maalim Seif na wenzake wametimiza malengo yao ya kuingia serikalini, lakini sisi huku Bara hatujapata tunachokitaka.”

Akiongea kwa kujiamini, Kirungi amenukuliwa akisema, “Acheni unafiki. Nendeni mikoani mkajenge chama. Msikae hapa kuleta majungu.”

Naye Hamad Rashid, taarifa zinasema alisema yeye na makamu wake Machano Khamis, walikutana mjini Zanzibar na kukubaliana kuwa Maalim Seif anakidhoofisha chama chao.

“Wewe makamu, si tulikutana Zanzibar; tukazungumza na ukaniambia kuwa Maalim Seif anadhoofisha chama kwa hatua yake ya kuingia serikalini? Sasa leo umepewa vipesa kidogo, tayari umebadilika,” alieleza Hamad Rashid kwa njia ya kusuta.

Mkutano wa baraza kuu unaotarajiwa kufanyika leo mjini Zanzibar, ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo utakaoamua hatima ya Hamad Rashid na wenzake, unatarajiwa kuwa na mjadala mpana, hasa kuhusiana na hatua ya uhusiano wenye shaka kati ya Jussa,  January Makamba (Mbunge wa Bumbuli – CCM) na Rostam Aziz.

Imeelezwa kuwa baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa tayari wamekusanya ushahidi wanaodai kuwa unaoenyesha Jussa akiwasiliana na mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, akiomba amtetee Rostam kwenye sakata la Richmond.

Ushahidi mwingine ambao wanaodaiwa kukivuruga chama wamekusanya, ni pamoja na mawasiliano ya imeili kati ya Jussa na Makamba, yakiwamo inayodaiwa kuwa kauli ya Makamba akihoji, “Utakumbuka yale makubaliano yetu; imekuwaje mwafaka wa kutoenda personal (kushambulia mtu binafsi)?

Naye Jussa akijibu Makamba alisema, “January, maelewano yetu yako palepale. Kosa lilikuwa langu kumsubiri (Lipumba) hadi tuonane uso kwa uso ili nimpe briefing (taarifa). Bahati leo amekuja Zanzibar na tumeelewana…”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: