Uranium kufuta historia, Bahi, Manyoni na Kondoa


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 14 July 2010

Printer-friendly version
Gumzo

SIYO siri tena kwamba mji na sehemu kubwa ya wilaya ya Bahi vitafutika kwa maana ya wakazi wake wote kuhama ili kupisha uchimbaji madini ya uranium.

Taarifa zilizosambazwa wilayani humo zinaonyesha kuwa wasio na shughuli zozote za uchimbaji na uchenjuaji uranium watatakiwa kuishi umbali wa zaidi ya kilomita 50 kutoka eneo lililotengwa kwa ajili ya mradi huu.

Makao makuu ya wilaya ya Bahi yaliyoko kilomita mbili na nusu kutoka kilima cha Kisalalo ambako ndiko yamegundulika madini ya uranium, yatafutika. Vivyo hivyo miji ya Manyoni na Kondoa iliyomo ndani ya kilomita 50 kutoka yalikogunduliwa madini.

Jiji la Dodoma nalo limo hatarini ingawa inasemekana linaweza kuponea chupuchupu kwa kilometa sita tu; kwani umbali kutoka Bahi hadi Dodoma ni kilomita 56.

Hii ina maana wakazi wa vijiji zaidi ya 86 vilivyo katika Bonde la Bahi lenye mbuga za Sulungai – kutoka wilaya ya Bahi mkoani Dodoma hadi Manyoni mkoani Singida – watahamishwa kutoka makazi yao ya miaka nendarudi.

Madini ya uranium hutumika kuzalisha umeme, kutoa matibabu kwa kutumia mionzi ya nyuklia, kufanyia utafiti wa kisayansi na katika kutengeneza silaha za nyuklia.

Kiwewe kilichokumba wengi kinatokana na taarifa rasmi kwamba serikali imetoa kibali kwa kampuni ya Uranex (ASX) ya Australia kufanya uchimbaji na uchenjuaji madini ya uranium katika Bonde la Bahi/Sulungai.

Eneo lote litakalohusishwa na uchimbaji madini kuanzia mwaka 2012 lina ukubwa wa kilomita 2,365 za mraba katika wilaya mbili za Bahi na Manyoni.

Makazi, mashamba, maeneo ya asili ya matambiko na vielelezo vingine vya kihistoria kama kanisa la Bahi lililojengwa mwaka 1912, vyote vitavunjwa na kufutwa kwenye uso wa dunia miaka miwili ijayo.

Hadi sasa hakuna mtawala aliyezungumzia umilikishaji kisheria mali za wananchi na tathmini ya mali hizo kwa ajili ya fidia halali kwa kilichopo kwenye uso wa ardhi na ardhini kabla ya kuanza uchimbaji.

Ilivyo sasa serikali, kama kawaida yake – machimbo ya dhahabu ya Buzwagi na North Mara – yaweza kunawa mikono na kuwatelekeza wananchi kwa kampuni itakayochimba madini kuwa ndiyo itashughulikia tathmini na fidia.

Katika taarifa yake ya 19 Julai 2009 iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, serikali inasema wananchi wanaoishi kwenye maeneo yenye hazina ya madini ya uranium wasiwe na wasiwasi kuhusu mionzi hatari ya metali ya madini hayo.

“Waendelee kama walivyozoea kwa karne nyingi, kuishi kwenye mashapo yenye madini ya uranium bila kudhurika hadi pale watakaposhauriwa na serikali kupisha shughuli za uchimbaji zitakapoanza,” alisema Ngeleja.

“Hadi watakaposhauriwa na serikali kupisha shughuli za uchimbaji…” na siyo wakati serikali itakapotathmini mali zao na kutoa fidia stahili. Hapo ndio kiama, kwani kinachoitwa “ushauri wa serikali” mara zote kimekuwa lazima au shuruti.

Aidha, serikali haitoi hata elimu juu ya athari za uranium. Kuna wanaharakati wa mazingira kutoka asasi za kiraia za Al-Mallid, Femapo na Cesope ndio pekee walijitokeza kuelimisha wananchi kuhusu uranium na mazingira.

Ni wanaharakati hawa ambao wameeleza umuhimu wa raia asiyejihusisha na uchimbaji madini kuishi umbali wa kilomita 50 kutoka eneo la mgodi ili asiweze kudhurika.

Taarifa ya serikali ya 2009 inakiri kuwa madini ya uranium yakichenjuliwa na kutoa metali ya uranium, basi metali hiyo huwa hatari kwa maisha ya watu, viumbe wengine na mazingira kwa vile hutoa mionzi yenye nguvu nyingi.

Padri Patrick Safari wa parokia ya Bahi anasema uchimbaji madini ya uranium katika wilaya ya Bahi, utakaoandamana na uhamishaji, hata kwa nguvu, maelfu ya wananchi, utakuwa na athari mbaya kwa binadamu, viumbe hai na mazingira kwa ujumla.

“Sisi katika nafasi ya kanisa tunaona kuondosha watu ni kufuta historia,” anasema Padri Safari.

Kanisa la parokia ya Bahi ndilo la kwanza kujengwa katika eneo hilo. Lilijengwa mwaka 1912 na kufuatiwa na makanisa ya Kigwe, Kintinku, Manyoni, Itigi na Chibumagwa.

Woga uliopo ni kwamba kuondoshwa kwa wananchi katika eneo hili, ili kupisha shughuli za uchimbaji na uchenjuaji uranium, kutakuwa njia maalum ya kufuta kazi ya kanisa katika kaya ambazo zimekuwa zikiishi karibu, katika vigango, makanisa na parokia nzima na jimbo kwa jumla.

“Kanisa linajali mazingira; uhai unahusisha watu, wanyama, wadudu, samaki na ardhi kwa uzalishaji. Sisi ni sauti ya watu wasiosikika ambao wanaona eneo kubwa la ardhi yao litahusika katika uchimbaji madini ya uranium,” anasema.

Familia ya Rashid Nzwili, moja ya familia za wafugaji zilizohamia Bahi baada ya kuondolewa kwa nguvu, Ihefu, wilayani Mbarali katika mkoa wa Mbeya, inajuta kuhamia Bahi katika Bonde la Sulungai.

Kwa familia hii, huo ni msiba wa pili. Msiba wa kwanza ulimkumba Ihefu, mwaka 1988 akiwa bado mdogo. Ilianza hivi: Familia nzima ya Nzwili Massanja iliondoka Shinyanga na mifugo hadi eneo lenye uwanda mpana na wa kijanikibichi wa Ihefu.

Waliishi hapo raha mstarehe na kwa kuwa eneo hilo lina maji ya kutosha, wafugaji waliligeuza pia kuwa makazi yao ya kudumu. Lakini mwanzoni mwa miaka ya 2000 serikali ilitangaza eneo hilo kuwa hifadhi, hivyo wafugaji wakaamuriwa kuhama.

Wapo waliohamia Songea na maeneo mengine ya mkoa wa Mbeya lakini familia ya Nzwili, akiwemo Rashid, baba yake Nzwili Massanja na ndugu zake, waliamua kusafiri hadi Bonde la Bahi/Sulungai, Bahi, mkoani Dodoma.

Leo familia hii inajilaumu kuchagua Bahi kuwa makazi ya kudumu kwani wanatakiwa kuhama kwenda kusikojulikana, ili kupisha mradi mkubwa wa uchimbaji madini ya uranium.

Rashid ana kumbukumbu ya yaliyowapata. “Nikiwa na wazazi wangu tulifika Ihefu tukiwa na ng’ombe 2000. Sikumbuki idadi ya mbuzi na kondoo. Lakini katika sekeseke lile la kuhamishwa kwa nguvu kutoka Ihefu, tuliondoka na ng’ombe 80 tu,” anasimulia Rashid.

“Baba alinipa ng’ombe 20 nikaja kuishi hapa Bahisokoni. Mdogo wangu alipewa ng’ombe 10. Kwa vile nilishuhudia sekeseke la Ihefu, katika Bonde la Usangu, nashindwa kueleza woga na masikitiko yangu kuhusu kuhamishwa, tena bila kujua ninakopaswa kwenda,” anasema Rashid kwa sauti ya kusononeka.

Rashid ana eka sita anamolima mpunga katika eneo la Lionii na mahindi lakini sasa akiwa na wake wawili na watoto tisa, anatafakari atakavyotupwa nje ya makazi yake kama ilivyotokea Ihefu.

Padri Safari anasema haafiki uchimbaji na uchenjuaji uranium katika mazingira ya sasa. Anasema kanisa linahudumia binadamu kiroho, “hivyo lazima tujali mwili wake, afya yake, mali zake na mazingira yanayomwezesha kuishi.”

“Hatuamini kama serikali ina uwezo wa kulipa fidia watu wote watakaoathirika kutokana na uhamishaji mkubwa kama huu katika historia. Inasikitisha kwamba hata viongozi hawashiriki katika kutoa elimu juu ya madhara ya uranium,” analalamika padri.

Kuhusu umbali, Samwel Galulet Mlugu, ambaye ni mkazi wa Bahimwanachugu anasema mwaka jana, katika mkutano wa wanaharakati wa mazingira ulioshirikisha wanaharakati wa kimataifa, waliambiwa wananchi wawe umbali wa kilomita 45 unakotokea upepo na kilomita 60 unakoelekea.

Samwel anasema waliambiwa na wanaharakati kuwa kemikali zinazotoka kwenye uranium huweza kuendelea kuwa na nguvu katika maji ya mto na kuathiri hata watu na viumbe vingine hai vilivyoko kilomita 250 kutoka pale kemikali zilipoingia majini.

Wakati mashirika yasiyo ya kiserikali yakifanya kazi ya kuwaelimisha wananchi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima anadaiwa kutoa “kauli ya maumivu” kwa wananchi katika mkutano wa hadhara.

Katika ziara yake wilayani Bahi mwaka jana, Malima anadaiwa kusema, “Suala la kuhamishwa halitakuwepo na kama mtahamishwa itabidi mfanye makubaliano na hizo kampuni (na hapa ni Uranex ASX),” anasimulia Athumani Makolokolo akikariri alichosema waziri Malima.

Malima aliwaacha njiapanda wananchi alipojiondoa yeye na serikali yake katika kusimamia fidia pale alipoonya kuwa isije ikatokea mtu akataka pesa nyingi katika eneo dogo.

“Kwanza alisema madini hayatachimbwa lakini baada ya kubanwa kwa maswali, akatoa majibu hayo. Serikali inataka kutushtukiza kama walivyofanya katika upimaji viwanja. Walipima na kugawa hadi kwenye maeneo ya watu, hadi wenye maeneo wakakosa,” anakumbuka Makolokolo.

Anapopima kauli ya Malima, mzee Mussa Chizumi, aliyekariri simulizi za “Ukoloni mpya uliotabiriwa” katika mfululizo wa makala juu ya uranium wilayani Bahi, anasema haoni uwezekano wa kuigomea serikali isipokuwa anatoa ushauri.

“Serikali itupe hatimiliki ya makazi na mashamba ili tusidhurumiwe wakati wa kulipwa fidia kupisha mradi huo wenye faida kwa serikali,” anapendekeza.

Wito huo anao pia Rashid kwamba wananchi hawana ujanja isipokuwa kuhama ili kupisha mradi huo, “…bali tumilikishwe ardhi ili wakija wachimbaji tulipwe fidia halali kwa maeneo tunamoishi,” anasema kwa kuzingatia kauli ya waziri Malima kuhusu serikali kutoweza kulipa fidia.

Mbwana Omari Shomito, mkazi wa Bahisokoni, anasikitikia kukosekana kwa mwamko wa wananchi; kwamba ingawa yanafanyika makongamano mengi yanayoandaliwa na asasi za kiraia, mahudhurio ni kidogo.

“Tatizo suala hili linataka kuchukua mkondo wa siasa; CCM (Chama Cha Mapinduzi) wanakubali mradi huo na wanaokataa wanadaiwa kuwa wapinzani,” anaeleza.

Aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Bahi, Omari Badwel aliondolewa kwenye nafasi hiyo kwa madai ya “kufungua mkutano wa asasi za kiraia” uliokuwa na ajenda ya mazingira na suala la uranium.

Jacob Mwamatepe, mkazi wa Kyela anayefanya kazi ya uvuvi katika Bwawa la Sulungai/Bahi, anasema uranium itasababisha wavuvi na wafanyabiashara wapatao 600 katika kambi ya Bahinagulo kukosa kazi.

“Uvuvi ni kazi yetu kubwa; kwa kipindi cha miezi mitatu huwa tunaondoka na zaidi ya shilingi milioni moja – hapo ni mbali ya vifaa tunavyokuwa tumenunua. Tukiondolewa hapa kupisha uchimbaji wa madini, basi na ajira yetu itakuwa imesitishwa,” alisema.

Mwanaharakati wa mazingira wa asasi ya Al-Mallid, Menasi Venance Muhumpa anasema kwa kuwa serikali haijajiandaa kuchimba madini, ingekuwa busara kuacha kufanya hivyo.

“Serikali itoe elimu ya kutosha, iandae eneo la kuwahamishia watu, itengeneze vizuri miundombinu ya barabara na maji, badala ya kuwaacha wananchi kuendelea kujiimarisha hapo walipo,” anasema.

Anasema pia, kwa vile eneo litakalotumika ni kubwa na litaathiri viumbe wengi, serikali itoe elimu kwa wananchi juu ya uranium ni nini, faida na athari zake; na kuhakikisha watu wa maeneo hayo wananufaika na uchimbaji huo.

Kwa sasa siyo rahisi kutamani kuwekeza Bahi kwa kujenga mahoteli, kuwa na shughuli nyingine za huduma na hata kufanya biashara nyingine wakati wananchi waliopo wanajua kuwa watashurutishwa kuhama.

Upinzani ni mkubwa. Katika mkutano mmoja wa viongozi wa vijiji mjini Dodoma, kati ya wajumbe 96 waliohudhuria, watu 68 walipinga na 28 walikataa kupiga kura ili kuiruhusu serikali ichimbe madini ya uranium.

Suala la uranium linatarajiwa kuwa kete ya kisiasa kwa wote walioonyesha nia ya kuwania ubunge na udiwani Bahi. Hata mgombea urais atalazimika kulifafanua kwa kina.

0
No votes yet