Urithi wa Nyerere ni Muungano tu?


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 04 May 2011

Printer-friendly version
Mwalimu Julius Nyerere

KINGUNGE Ngombale-Mwiru, mmoja wa makada wakuu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ametoa wito.

Anawataka Watanzania kupuuza watu “wanaobeza” Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Amesema watu hao ni wabinafsi na waroho wa madaraka.

Ameliambia kongamano la Umoja wa Vijana wa CCM wa Shirikisho la Vyuo Vikuu lililofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, kwamba wanaobeza Muungano wa Tanzania wanapingana na dhana ya wapigania uhuru ambao walikuwa na uzalendo wa kudai uhuru na heshima ya taifa lao.

Kwenye kongamano hilo, Kingunge alizungumzia jinsi Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume walivyojadili na “kushirikisha wananchi” kufikia aina ya muungano uliopo sasa.

Alisema Karume alitaka iwepo serikali moja ya Jamhuri ya Muungano, lakini baadaye akakubali wazo la Nyerere kuwa na serikali mbili – Muungano na Zanzibar – ili kulinda utaifa wa Zanzibar.

Hapa Kingunge anataka kuwaambia Watanzania kuwa kile kilichojadiliwa na kuafikiwa na marais wawili hao ni “msahafu” usioweza kubadilishwa; hivyo pasiwepo wa kulalamika.

Muungano ni kitu kizuri. Unafaa kuenziwa na watu wa pande zote mbili. Hapo ni kama hakuna matatizo. Kukiwa na matatizo sharti wananchi wapewe fursa kuujadili; kupata uamuzi wenye maslahi – kuuvunja au kuuendeleza.

Historia ya malalamiko ya Wazanzibari ni ndefu; sawa na Muungano wenyewe. Mathalani, malalamiko hayo ndiyo chimbuko la kile kilichoitwa “kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar” mwaka 1984.

CCM iliminya haki ya Wazanzibari kwa kumwadhibu Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Aboud Jumbe kwa kumfuta urais. Bado Wazanzibari wameendelea kusisitiza kuwa muundo wa Muungano urekebishwe.

Miongoni mwa wanaolalamikia muundo wa Muungano ni wafanyabiashara ambao hawataki madaraka ya kisiasa bali kuondolewa kwa utaratibu wa kulipa ushuru mara mbili – Zanzibar na Dar es Salaam au Tanga.

Ni ufinyu wa mawazo basi kufikiri kwamba kila anayetaka muundo tofauti wa Muungano, anafikiria nafasi za uongozi. 

Tujiulize, wabunge wa kundi la G55 lililodai, mwaka 1994, kuwepo kwa Tanganyika na serikai yake, walitaka ubalozi au uwaziri?

Kingunge ni shahidi kwamba kuna mambo mengi ya urithi waliyoacha Nyerere na Karume; siyo Muungano tu yamevunjwa, yamepuuzwa, yamesahauliwa na yamekiukwa.

Wananchi walishapokea ushauri mwingi kutoka kwa akina Kingunge, lakini sasa wamegundua kuwa si kila linalosemwa na wao ni kwa maslahi ya taifa.

Tuchukue Azimio la Arusha. Mwaka 1967 TANU ilianzisha Azimio lililoweka miiko ya uongozi, misingi ya utawala bora na siasa ya ujamaa na kujitegemea.

CCM ilirithi Azimio. Hii ni pale vyama viwili – TANU na Afro Shirazi – vilipoungana na kuzaa CCM, hapo 5 Februari 1977.

Kina Kingunge ndio walikuwa machampioni wa kuelezea na kufafanua azimio, ikiwa ni pamoja na kutekeleza azimio hilo chini ya Mwalimu Nyerere.

Kuna vilivyotaifishwa na kuwa chini ya serikali. Kuna vilivyojengwa na kuwa vya umma chini ya serikali – viwanda, mashirika na makampuni.

Mwaka 1985 baada ya Nyerere kung’atuka madarakani, serikali ikapagawa na kuanza kuvunja misingi yote chini ya kilichoitwa Azimio la Zanzibar.

Viongozi waliua Azimio la Arusha. Wakavunja miiko ya uongozi. Wakatengua misingi ya usawa katika kipato, umilikaji ardhi na uongozi bora.

Wakaanza kuuza viwanda na mashirika yote ya umma. Walipokosa mali za kuuza, wakajiuzia nyumba za serikali kwa “bei ya kutupa.” Kingunge hakusikika akisema “tutajuta.”

Viongozi wakaanza kuwa na hisa katika makampuni na mashirika binafsi, ikiwa ni pamoja na kuwa wakurugenzi. Hakuna aliyesema tutajuta.

Hata pale Kingunge alipopewa mradi wa kukusanya ushuru kituo cha mabasi Ubungo na maegesho ya magari jijini Dar es Salaam, hakujuta kutelekeza ujamaa huku akiwa mmoja wa makada wakuu wa chama.

Ngombale atakuwa alijuta tu pale alipopokonywa mradi huo, kutokana na madai ya kuwasilisha mapato kiduchu kuliko makusanyo halisi.

Ni utuki ulioje, kwamba Kingunge – mwana-ideolojia na kada mkuu wa CCM – “alishinda” zabuni ya kuendesha kituo na maegesho ya magari wakati Wilson Mukama akiwa mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam.

Leo hii, Mukama ndiye katibu mkuu wa CCM. Anajua yote ya Kingunge; yale ya mapato yake na hata lawama kwamba “mwekezaji Kingunge” alikuwa akichukua kingi kuliko ilivyostahili. Hakuna anayesema tutajuta.

Ilikuwa tume ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda iliyobaini uozo uliofanywa. Makada hawa hawakujuta.

Hapa, suala la uadilifu liliwekwa kando na utekelezaji siasa ya ujamaa na kujitegemea kama ilivyo kwenye katiba yake, ama vilitupiliwa mbali au vilisahaulika. Hakuna aliyesema tutajuta.

Ibara ya 107 ya Katiba ya CCM toleo la mwaka 2010 inasema, pamoja na mambo mengine, kuwa kazi za Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC) ni pamoja na “kuongoza na kusimamia ujezi wa Ujamaa na Kujitegemea nchini.”

Kingunge, ambaye ni mwandaaji wa Dira ya CCM, ana nini la kusema kuhusu utekelezaji wa hayo katika mfumo wa sasa ambamo CCM inauza vipande vya ardhi kwa makabaila, mabwanyenye, na mabepari? Hakuna anayesema tutajuta.

Mbona hawajuti kupotosha wananchi na hasa wana CCM, kwamba nchi hii bado inafuata siasa za ujamaa wakati waliitupa tangu walipoanzisha Azimio la Zanzibar na kukumbatia ubepari?

Wamebaki wameshikilia Muungano kwa matendo yao yanayofunikwa na kauli zao za ulaghai, watabomoa Muungano – jiwe la mwisho la msingi wa taifa hili.

Huwezi kupenda Muungano bila kupenda kushirikisha wananchi kuujadili, kuukosoa na kuurekebisha na kuuimarisha au hata kuukataa kama hauna manufaa tena.

Mwaka 1995, katika kinyang’anyiro cha urais kupitia CCM, Mwalimu Nyerere aliwakataa baadhi ya wagombea dakika za mwisho wakati wa mchujo mjini Dodoma.

Tena alisema kwamba “bila CCM imara nchi itayumba;” akiwasihi watafute kiongozi madhubuti wa kusimamia chama na serikali.

Mbona hawaelezi walivyopuuza ushauri wa mwasisi huyo wa Tanzania na sasa nchi imetekwa na ufisadi? Hakuna anayesema tutajuta.

Mwalimu Nyerere na Karume walichukia na walipinga rushwa kwa vitendo. Historia ya wapigania uhuru hao inaonyesha nini katika vita dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi? Hakuna anayesema tutajuta.

Nini kimetokea baada ya viongozi hao kufariki dunia hadi kina Kingunge hawajutii chama chao sasa kulea walarushwa na mafisadi?

Je, kukosa uzalendo ni katika Muungano tu? Kutupa au kubadili mambo mengine ya waasisi siyo usaliti? Hakika Nyerere hakurithisha Muungano peke yake.

Kingunge na wenzake sharti wajute kwa kuua karibu “kila kitu cha Nyerere” na kubakiza Muungano; tena Muungano wenye nyufa, matundu na nondo zilizopinda.

0658 383979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: