Usafir wa TRL: Kama binadamu, kama mnyama


Issa Katoba's picture

Na Issa Katoba - Imechapwa 11 March 2009

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

NI saa 10:30 alasiri. Nipo Stesheni Kuu ya Reli Dar es Salaam. Ndio kituo kikuu cha kuanzia safari za treni kwa njia ya reli ya kati iendayo Mwanza na Kigoma kupitia Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga.

Safari inaanza saa 11 jioni na abiria tunapungia mikono ndugu na jamaa zetu kuwaaga kwamba safari ndio imeanza; nao wanatupungia kujibu; ikiashiria kututakia safari njema.

Nimekaa behewa la Daraja la Tatu. Niliamini kwamba kutokana na serikali kukaribisha kampuni ya kigeni kuendesha menejimenti ya lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), basi safari itakuwa nzuri, tofauti na nilivyosafiri miaka minne iliyopita.

Niliamini menejimenti mpya iitwayo RITES kutoka India, wanaofanya kazi chini ya shirika jipya la TRL (Tanzania Railways Limited) wameleta mabehewa mapya.

Nilikosea. Nikiwa nimejitayarisha kukalia sofa katika kiti nilichoandikiwa namba kwenye tiketi yangu, nikakumbana na kiti cha bati. “Ah, nikalie kiti cha bati leo?”

Nakalia kwa kujipa moyo labda mambo mengine yaweza kuwa bora. Naanza kuhisi joto. Nainua macho kutazama juu kwa matumaini ya kuona feni ili niiwashe na kupunguza joto.

Lahaula! Ni mabati chakavu ya zilizokuwa feni za TRC; mifuniko yake imekatikakatika kutokana na kutu. Mapanga yamejaa vumbi na kwa hali ilivyo feni lile haliwezi kuzunguka. Na sehemu nyingine ninaona misumari zilipokuwa zimefungwa feni.

Natulia na hali ile ya joto. Najiuliza maswali sipati majibu yake. Narudi kukumbuka maneno ya viongozi kwamba tukikaribisha wawekezaji wataimarisha huduma za reli. Si hawa waliopata kusema “mabehewa yamefanyiwa ukarabati na mengine ni mapya yaliyotoka India?”

Sasa kama ndio hayo niliyoyakuta daraja la tatu, labda macho yalinidanganya. Hapana. Macho yangu yangali mazima. Nilichokiona ndio hali iliyopo.

Kutafuta ahueni, sasa angalau nipate maji nijimwagie. Mahala pekee ninapoweza kuyapata ndani ya treni ni kwenye vyoo.

Nasikia sauti za watoto wadogo wakilia, “Joto kali!” Watu wazima wanavumilia ila wanalalamikia hali hii. Baadhi walioshindwa uzalendo, wanaanza kusema “Ah ndio serikali ya CCM hii. Haitaki kusaidia wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na hasa Tabora na Kigoma.” Navuta pumzi taratibu.

Nakwenda chooni ili kujimwagia maji. Ebo! Huku balaa tupu. Kumejaa glasi ndogo za plastiki ambazo wasafiri wanakwenda nazo zikiwa na maji lakini sasa hazina maji. Zimetupwa ovyo.

Ninabaini kuwa hakuna maji vyooni. Nashindwa kuvumilia. Namuuliza mfanyakazi anayehusika na usafi wa behewa hili la Daraja la Tatu, “Ndugu yangu, hali hii vipi?”

Sikiliza majibu yake, “Unashangaa nini sasa kaka, hii ndiyo hali halisi ya usafiri wetu; wewe vumilia tu.” Hakika, hali ya vyoo inasikitisha maana hata mabeseni ya kuoshea mikono unaogopa kuyagusa kwa jinsi yalivyo machafu.

Saa 1:30 usiku tunafika stesheni ya SOGA, mbele kidogo kutoka Pugu. Nilitaraji kuwa tutaondoka hapo ndani ya muda wa kawaida. Tulilala hapo hadi saa 11:45 asubuhi bila ya kupewa taarifa yoyote.

Hata hivyo tulianza safari. Njiani tulisimama mara kwa mara kwa zaidi ya dakika 15 hadi 20 katika sehemu ambazo kwa kawaida treni hutakiwa kusimama kwa dakika tatu hadi tano. Tuliambiwa kuwa hiyo ni kwa sababu huko mbele kuna matengenezo ya reli iliyoharibika.

Hilo halishangazi. Ni kwa kuwa baadhi ya vituo vya uangalizi wa reli (gengi) ambako walikuwa wakikaa mafunzi wa TRC walioshughulikia ukarabati wa njia kila siku, vimefungwa kwa madai ya “kubana matumizi.”

Zamani njia ilikuwa safi. Nyasi zilizokuwa maeneo jirani na reli zilikuwa zikifyekwa vizuri na mafundi walioitwa kwa jina la “pigilia.” Hiyo ilisaidia kuwa na reli imara. Siku hizi hakuna kitu kama hicho kwa sehemu kubwa ya reli.

Ni kawaida wasafiri kukumbwa na kila aina ya adha safarini. Wale wanaopandia vituo vya njiani wanalazimika kuingia kwenye treni bila ya tiketi. Wakiuliza wanambiwa na wahusika kuwa tiketi zimekwisha.

Huwezi kuamini. Hata katika treni kumbe kuna wapiga debe! Treni ikifika kituoni, utasikia wasafiri wanaitwa, “We una shilingi ngapi na unakwenda wapi?” Hawa utakuta wengi kwenye vichochoro vya behewa wakiwa na stuli na viti vya marimba. Wala si wafanyakazi wa TRL bali wanakupa tiketi.

Nilipouliza baadhi ya abiria wazoefu, inakuaje ndani ya treni kuna watu wamebeba vistuli na viti vya marimba, wakanishangaa, “We bwana vipi? Hawa ukiongea nao vizuri waweza kusafiri kwa nauli ya chini kabisa – mwanzo hadi mwisho.”

Wakati nikiwa bado natafakari hayo, mkaguzi wa tiketi kwenye treni (TTE) anaingia katika behewa nililomo. Anakagua tiketi, kiti changu, namba 8, kilikuwa mwanzoni kabisa karibu na uchochoro ambapo hukaa watu wasiokuwa na tiketi.

Abiria mmoja alipoulizwa tiketi, haraka akainuka mpiga debe mwenye kistuli na kumuonyesha TTE orodha ya aliowaita “watu wangu.” Mkaguzi anaangalia na kuondoka kuendelea na ukaguzi mbele.

Katika treni huduma za vinywaji baridi hutolewa na vijana waliovalia sare – shati jeupe na suruali nyeusi. Hawa hupita wamebeba makreti ya soda begani na inakuwa hatari kutokana na msongamano mkubwa wa abiria kwenye mabehewa.

Sasa ni saa 4:30 usiku. Treni inaingia stesheni ya Kigoma. Tunaanza kuteremka na kila mmoja anaanza pilikapilika za kutafuta usafiri wa kwenda usawa wa anakofikia.

Stesheni ya Kigoma imefurika abiria. Mamia wamekwama hapo kwa siku mbili wakisubiri treni. “Hivi mmeshuka labda tutachukua hili; tupo hapa tokea juzi (siku mbili zilizopita),” ananieleza kijana mmoja ninayemfahamu.

Wakati wa kurejea Dar es Salaam nilitaka kusafiri kwa Daraja la Pili ili kubadilisha mazingira. Ninaulizia tiketi ya daraja hili. “Itabidi usubiri hadi baada ya wiki mbili,” najibiwa.

Nikaona balaa inanirudia. Kwamba nitalazimika kusafiria lilelile daraja la tatu. Nilipoulizia tiketi nikaambiwa, “Tiketi hupatikana siku ya safari na ili upate lazima uwepo hapa kuanzia saa 11 alfajiri.”

Nilishindwa. Nikajiandaa kukata tiketi ndani ya treni nikijua nitalipishwa faini. Nikakata tiketi ndani kwa kutoa ziada ya Sh. 5,000 kutoka nauli ya kawaida ya Sh. 39,700.

Adha, Daraja la Pili kutokea Kigoma ni nyingine. Behewa nililopanda, Na. 2203 Chumba F, lilikuwa chakavu na chafu. Ilionekana halijatumika kwa muda mrefu.

Feni lake ni msumari mtupu uliozungushiwa sufuria la kipenyo kipatacho futi moja na kupakwa rangi. Hili limetobolewa tundu ili kusaidia kupitisha hewa, ingawa halizunguki. Hakuna mashuka kwenye vitanda na vitanda vyenyewe ni chakavu.

Nilipomuuliza TTE kuhusu hali hiyo, alijibu haraka, “Hii ndiyo TRL.” Nami niliona, hiyo ndiyo TRL.

*Mwandishi ni Ofisa Matangazo wa MwanaHALISI aliyekuwa likizo nyumbani kwao, Kigoma, Februari mwaka huu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: