Usafiri baharini roho mkononi


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version
Miundombinu ya usalama dhaifu

“IKIZAMA hatuizamui. Ikiungua hatuizimi. Serikali yetu ipoipo. Inaangalia tu, haina cha kufanya…”

Ni maneno 12 ya Idi Makame, mkazi wa Mikunguni, mjini Zanzibar, akielezea jinsi serikali inavyoshindwa kukabiliana na ajali za vyombo vya baharini.

Mfanyakazi huyu wa sekta ya fedha, ametoa kilio siku tatu tu tangu meli ya mizigo iliyokuwa imetia nanga mdomoni mwa bandari kuu Zanzibar – Malindi, iteketee kwa moto.

Moto ulioteketeza meli hiyo iitwayo m.v Ya Razaak, inayomilikiwa na kampuni ya Green Island Enterprises, ulizimwa saa nne baadaye.

Ni hapa ambapo meli ya m.v. Fatih ilizama, Juni 2009 na kuua watu wote 10 waliokuwemo.

Meli hiyo ilisajiliwa Zanzibar 29 Juni, 2004 na ilikuwa na uwezo wa kubeba tani 675 za mizigo ambapo ilipoanza kuwaka, ilikuwa imeshateremesha mizigo yote.

Kikosi cha Zimamoto na Uokozi cha Zanzibar (KZU) kiliwasili mapema bandarini, lakini ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kuifikia meli, pamoja na wataalamu, uliwanyima wafanyakazi wake nafasi ya kuzima moto huo haraka.

Ajali hii inarudisha kumbukumbu ya 10 Septemba 2011, wakati m.v Spice Islander I, ilipozama kwenye eneo la Matumbilini, katika Bahari ya Hindi, kilomita kadhaa kutoka Bandari ya Mkoani, Kusini Pemba.

Kwa mujibu wa serikali ya Zanzibar, watu 203 walipoteza maisha na wengine 1,370 “kupotea.” Mpaka sasa hawajaonekana.

Shughuli za uokoaji wasafiri na wafanyakazi zilikuwa duni. Meli hiyo ilizama saa 7 usiku, lakini chombo cha kwanza cha kuokoa kilifika hapo saa 12.30 asubuhi, kwa mujibu wa simulizi za mabaharia na walionusurika.

Ingawa Zanzibar ni nchi ya visiwa viwili vikubwa na vidogo vingi, inakabiliwa na ukosefu mkubwa wa zana na wataalamu wa shughuli za ukaguzi, uchunguzi na uokozi.

Ofisa mwandamizi serikalini ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini anasema, “Hili ni tatizo sugu. Ufumbuzi wake utachukua miaka mingi.”

Hali hii inatokea miaka 18 tangu Ali Ibrahim Muhina, aliyekuwa Mkurugenzi wa Bandari na Usafiri Baharini, idara mahsusi iliyokuwa ikisimamia bandari na usafiri wa baharini, apaze kilio chake.

Kupitia mada aliyoiita “Maandalizi ya kukabiliana na majanga ya baharini, shughuli za utafutaji na uokozi Zanzibar; ” aliyoitoa kwenye warsha iliyofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Muhina alitambua umuhimu wa kuiwezesha idara yake kwa kuipa zana na wataalamu.

Alisema kwa kuwa Zanzibar ni nchi ya visiwa, suala la kukinga maafa na kuratibu shughuli za utafutaji na uokozi, pamoja na ujenzi wa miundombinu imara ya kuwezesha hayo kufanywa kwa ufanisi, haliepukiki.

“…Lakini ni ukweli ulio wazi kuwa idara haiwezi kutoa huduma zake kwa ufanisi. Haina zana na vifaa muhimu. Wafanyakazi wake nao wanahitaji mafunzo ya kisasa.”

Ilikuwa Septemba 1994 Muhina aliposema ajali 16 zilikuwa zimetokea katika kipindi cha miaka mine tu tangu 1990. Watu 127 walikufa. Mwaka 1990 pekee alisema, watu 108 walikufa kwa ajali za majini.

Ajali aliyoitaja kama kubwa ni iliyohusisha meli ya m.v Qabul, iliyotokea 14 Septemba, eneo la Nungwi, Kaskazini mwa kisiwa cha Unguja. Watu 68 walikufa; wawili tu ndio walinusurika.

Uchunguzi mpya umebaini hata sasa ambapo kumeanzishwa mamlaka maalum ya kusimamia sekta ndogo hiyo ya usafiri wa majini, bado mamlaka “ipoipo tu” – haina nyenzo wala wataalamu.

Mamlaka inao wakaguzi wawili na mchunguzi mmoja tu wa meli. Wanaohitajika ni angalau wanane. Pia, haina zana na vifaa vya kisasa vikiwemo vya mawasiliano kama redio.

“Panahitajika wakaguzi angalau wanane. Wanne wawepo Unguja na wanne Pemba. Kwa sasa yupo mchunguzi mmoja tu,” anasema ofisa mwandamizi, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano ya Zanzibar.

Ofisa huyo anasema wakaguzi wapo wawili lakini mmoja ni mgonjwa kwa zaidi ya mwaka sasa.

Ofisa huyo aliyeshurutisha kutotajwa jina, anasema mchunguzi wa meli huangalia kanuni za usalama wakati mkaguzi huangalia masuala ya kiufundi katika meli.

Mamlaka (Zanzibar Marine Authority – ZMA) ilianzishwa mwaka 2009 kutokana na Sheria Na. 5 ya mwaka 2006 iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi.

Nchi yenye bandari inahitaji, pamoja na mambo mengine, kituo cha kisasa cha mawasiliano cha kupokea taarifa za matatizo ya vyombo baharini.

“Hapa uzungumze kituo chenye vifaa kinachoweza kufanya kazi sambamba na kile kilichopo Feri, Dar es Salaam . Kile kinatosheleza eneo la Bahari ya Hindi hadi Shelisheli.

“Lakini ili kuweza kupokea taarifa vizuri, lazima nasi tuwe na kituo japo kidogo kilichoshiba vifaa vya kisasa. Hili ni moja ya mahitaji yetu  makubwa,” anasema ofisa huyo wa serikali.

Kuna kasoro nyingine kubwa upande wa wazamiaji na waokoaji. Wanaotegemewa kwa kazi hii ni askari wachache wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) wasiokuwa na uzoefu.

Aidha, hakuna helikopta kwa ajili ya utafutaji na uokoaji wakati wa maafa; wala vifaa vya huduma ya kwanza.

Kikosi kina boti mbili zisizo na vifaa vya kisasa. Boti hizo ndizo zinategemewa kukimbiza vyombo vilivyohofiwa kubeba karafuu za magendo.

Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Gavu anasema, wanaelewa matatizo hayo na wamekuwa wakielezea, kila wakati, ili hatimaye serikali itoe, “japo kwa awamu, fedha za kununulia zana muhimu. Zana zenyewe ni ghali sana.”

Alichotabiri Muhina miaka 18 iliyopita, ndicho kilitokea 10 Septemba na ndicho kinaeekea kuendelea kutokea.

0
No votes yet