Usafiri wa reli nchini - Ndoto isiyotimilika


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 08 April 2008

Printer-friendly version

NI kama mwaka mmoja tu uliopita pale Watanzania walipotangaziwa kuwa Ubelgiji imekubali ombi la Tanzania la kutandika reli itakayounganisha nchi hii na nchi za Maziwa Makuu za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Wakati huo, ule mkataba wa kulibinafsisha (au kulikodisha) Shirika la Reli Tanzania kwa kampuni ya RITES ya India ulikuwa bado haujasainiwa.

Sijui suala la mpango wa ujenzi wa reli hii umefikia wapi lakini swali moja ambalo wengi walikuwa wanajiuliza ni hili:

Kama serikali ilikuwa imeshindwa kabisa kuendesha mfumo wa reli uliorithiwa kutoka kwa wakoloni, wapi itapata taaluma ya kuiendesha reli hii mpya?

Na hata lile wazo lililopendekezwa – kwamba reli hiyo mpya ingeendeshwa kwa ubia – yaani pamoja na nchi hizo za Maziwa Makuu, haliingii akilini kutokana na historia ya kushindwa katika medani hii.

Kuna reli moja ambayo tulikuwa tunaiendesha kwa pamoja na Zambia – TAZARA – lakini angalia sasa jinsi reli hiyo ilivyojikita katika chumba cha wagonjwa mahututi – ICU – na inapumua tu kwa "matibabu" kutoka kwa wafadhili.

Kumekuwa na utamaduni wa kubomoa tu, kwa maana ya kung'oa kabisa reli na mataruma yake. Hilo limetokea.

Baada ya kupata uhuru Reli ya Kusini (Southern Line) kutoka Lindi, Nachingea hadi Masasi iling'olewa. Leo hii serikali inafikiria kujenga reli hukohuko Kusini kwenye Ukanda wa Kusini, "The Mtwara Development Corridor."

Vilevile katika miaka ya 1960 serikali iling'oa reli kati ya Manyoni na Singida, ingawa ilijengwa tena miaka 30 baadaye kwa gharama kubwa.

Reli kati ya Kaliua hadi Mpanda nayo ilikuwa kwenye mpango wa kung'olewa kama hawangekuwapo viongozi wachache wenye vichwa vilivyotulia.

Sasa reli ya kuhudumia nchi za Maziwa Makuu ya nini wakati tayari kuna reli inayotoa huduma kwa nchi hizo tangu zamani – Reli ya Kati (Central Line). Kilichotokea ni kwamba kutokana na huduma mbovu, ilishindwa kabisa kutoa huduma kikamilifu.

La kujiuliza ni kwamba wakati kulikuwa na matatizo makubwa ya uendeshaji wa reli hii, kwa nini serikali haikuomba Burundi, Rwanda na DRC kushiriki uendeshaji wa pamoja wa reli hii badala ya kukodisha watu kutoka nje?

Hawa wa nje ni kama RITES kutoka India waliokodisha Shirika la Reli Tanzania. Wameanza kushindwa kulipa hata mishara ya wafanyakazi. Wawekezaji wasio na fedha?

Inawezekana vipi kukodisha shirika la umma kwa kampuni ya nje ambayo haina uwezo kifedha? Hii inakumbusha kashfa ya mkataba wa umeme wa Richmond.

Huu nao ni ufisadi. Ni mikataba hii inayoendelea kulemaza uchumi na wananchi wenyewe.

Inasemekana kwamba kuna makampuni yaliyotoka Canada na Afrika ya Kusini yaliyoomba kuendesha TRC sasa TRL. Hayakukubaliwa. Aliyekubaliwa hana fedha!

Ziko wapi tambo za serikali na kampuni ya RITES kwamba TRL itatoa huduma nzuri kuliko ilivyokuwa wakati wowote huko nyuma. Sasa abiria wanarejeshewa nauli na kuambiwa watakuwa wanakuja kuulizia usafiri.

Kinachosikitisha ni kwamba kuna taarifa kuwa mwekezaji kaleta mabehewa na injini zilizokuwa zimetumika huko India katika miaka ya 1960 na kupakwa rangi tu.

Wiki iliyopita huduma za TRL zilisimamishwa kutokana na mgomo wa wafanyakazi hadi serikali ilipoamua kuingilia kati kwa kuahidi kuwalipa mishahara wafanyakazi.

Serikali imekubali kutoa kiasi cha Sh. 3.7 bilioni kwa miezi ya Machi hadi Julai, kwa lengo la kukwamua mwekezaji asiyekuwa na fedha.

Ingawa serikali italipa wafanyakazi, fedha hizo ni hasara nyingine kwa taifa kutokana na sera na mipango mibovu ya serikali.

Hapa hakuna tofauti na hasara inayotokana na shughuli za Shirika la Umeme, ambalo sasa hivi Watanzania wanaligharamia kwa pua na kope zao kutokana na sera, mipango na uendeshaji wake mbovu.

Serikali hii haijali wananchi wake. Usafiri wa reli ndiyo rahisi kuliko usafiri wa aina nyingine yeyote. Huo ndiyo usafiri unaotegemewa na wananchi wa kipato cha chini walio wengi katika nchi zinazojali wananchi wake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: