Ushindi wa Dk. Slaa kuimarisha Bunge


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 August 2010

Printer-friendly version
Mahasimu waweza kuwa upinzani
Wakongwe waaga kwa msononeko
Dk. Willibrod Slaa

USHINDI wa Dk. Willibrod Slaa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, ndio pekee unaoweza kumaliza mivutano iliyokumba bunge lililopita, MwanaHALISI imebaini.

Kwa mujibu wa matokeo ya kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizopigwa Jumapili iliyopita nchi nzima, viongozi wakuu wa makundi mawili yaliyokuwa yakinyukana, wameshinda kwa kura nyingi katika machimbo yao.

“Mvutano umedumu katika mazingira ya utawala ambao hauchukui hatua; unaolea na kubembeleza mafisadi. Dk. Slaa hawezi kulea ufisadi hata kwa miezi miwili,” ameeleza kiongozi wa ngazi ya juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Dar es Salaam.

Dk. Slaa ambaye ameteuliwa na chama chake kuwa mgombea urais, ndiye mbunge wa upinzani aliyejitambulisha katika kuibua wizi na ufisadi ndani ya serikali.

“Lakini katika hali ya kuwajibika, huwezi kuacha wabunge walumbane juu ya suala linaloweza kumalizwa mara moja kwa kutema wanaonekana kuwa vikwazo,” ameeleza kiongozi huyo wa CHADEMA.

Malumbano ndani ya bunge yalichipuka katika kashfa ya mkataba wa uzalishaji umeme wa dharura kati ya serikali na kampuni ya Richmond.

Kashfa ya Richmond ilichunguzwa na Kamati Teule ya Bunge na kuwataja baadhi ya wabunge na maofisa wa serikali waliohusika nayo.

Kutokana na kashfa hiyo, Edward Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu alijiuzulu kufuatilia kushiriki kimalifu katikla mchakato wa mkataba huo.

Rais Kikwete alilazimika kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri akiwaacha nje mawaziri Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi ambao walitajwa kushiriki kikamilifu katika kashfa hiyo.

Katika kura za maoni za Jumapili iliyopita, wanaoitwa mahasimu wakuu katika sakata hili wameshinda kwa kisindo. Majimbo ambako wabunge hao wa CCM wameibukia yameelezwa kuwa na upinzani “mdogo sana.”

Wakati Spika aliyemaliza muda wake, Samweli Sitta ameshinda jimboni Urambo Mashariki, Edward Lowassa ambaye amekuwa akidai kuhujumiwa kisiasa ameibuka na ushindi jimboni Monduli.

Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kashfa ya Richmond, Harrison Mwakyembe ametikisa kwa kishindo jimboni Kyela na Rostam Aziz ameshinda jimboni Igunga.

Andrew Chenge wa Bariadi Mashariki ameshinda kwa kura nyingi huku Christopher ole Sendeka ameibuka kidedea huko Simanjiro.

Sitta, Mwakyembe, Sendeka, Anna Kilango wa Same Mashariki, Victor Mwambalaswa wa Lupa na wabunge wengine wamekuwa upande mmoja wa kupinga ufisadi; wakati Lowassa, Rostam na Chenge wamekuwa wakituhumiwa kuwa upande wa wanaotetea ufisadi.

Lakini malumbano na minyukano ndani ya bunge imekuwa ikiletwa kwenye ngazi ya watu binafsi badala ya wapinga ufisadi dhidi ya waungamkono mafisadi.

Katika hili Sitta na Dk. Mwakyembe wameeleweka kuongoza upande wa wapinga ufisadi, wakati Lowassa na Rostam wametajwa kupingana nao.

Majeruhi katika kambi ya Sitta na Mwakyembe ni Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii, mwenzake wa Bumbuli, William Shellukindo na James Lembeli wa Kahama ambao wamebwagwa.

Katika kambi ya Lowassa ni Nazir Karamagi wa Bukoba Vijijini aliyekumbwa na kimbunga cha kukataliwa katika kura za maoni.

Kura za maoni mwaka huu zilikuwa chungu kwa wanasiasa wakongwe ambao wengi wao walishindwa vibaya na wagombea wasiotarajiwa.

Mkoa ulioongoza kwa kuachana na wakongwe wa siasa ni Iringa ambapo zaidi ya nusu ya wabunge wa zamani wamebwagwa.

Wabunge hao ni Jackson Makwetta (Njombe Kusini), Joseph Mungai (Mufindi), Benito Malangalila (Mafinga), Profesa Raphael Mwalyosi (Ludewa) na Monica Mbega (Iringa Mjini).

Wabunge hao wamekuwa bungeni kwa takribani miaka 20 bila ya kukatizwa. Mbunge mwingine wa Iringa kwa muda mrefu ni Anne Makinda (Njombe Kusini).

Makinda ameshinda kura za maoni na iwapo atashinda katika uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, ndiye atakuwa mbunge wa muda mrefu kuliko wote katika bunge lijalo. Aliingia mwaka 1975 kupitia Umoja wa Vijana.

Wakongwe wengine waliodondoshwa ni John Malecela (Mtera), Juma Ngasongwa (Ulanga Magharibi) na William Shellukindo (Bumbuli).

Hata hivyo, kura za maoni za CCM zinadaiwa kutawaliwa na rushwa huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ikitangaza kila siku waliokamatwa na kuhojiwa kwa tendo hilo.

Katika sehemu mbalimbali nchini pia, ikiwemo Dar es Salaam, uchaguzi umeahirishwa kutokana na kutofuata taratibu na vitendo vilivyodaiwa kuwa vya upendeleo.

Jijiji Dar es Salaam, wanachama wa CCM wapatao 700 walirudisha kazi zao kwa chama wakidai kuwa majina yao yaliondolewa kwenye orodha ya wapiga kura ndani ya chama.

Baadhi ya wananchi wamedai kuwa wamekuta majina yao yamewekewa alama ya “ndiyo” ikiwa na maana kuwa tayari wamepiga kura.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: