Ushindi wa mbeleko aibu Yanga, Simba


Elius Kambili's picture

Na Elius Kambili - Imechapwa 11 January 2012

Printer-friendly version

FUNUNU na malalamiko juu ya upangaji matokeo katika mechi za Ligi Kuu ya Bara huwa yanapuuzwa kwa madai ya kukosekana ushahidi. Klabu ndogo za soka zimekuwa zikilalamika kwamba Yanga na Simba zinabebwa, lakini hazisikilizwi.

Leo, hiki kilichotokea katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Zanzibar kinathibitisha klabu hizo kongwe katika soka nchini zinabebwa. Wakati kila shabiki ameona na amesikia, waandaaji michuano wameamua kufumba macho.

Mashahidi ni makocha Salum Bausi wa Miembeni na Stewart Hall wa Azam FC, na kiongozi wa klabu ya Miembeni. Hao wote wanathibitisha upangaji matokeo katika michuano hiyo inayomalizika kesho mjini Zanzibar.

Bausi, kutokana na kukerwa na upangaji matokeo,  alitangaza kuachia ngazi. Kisa ni bosi wake kuingilia kazi yake eti akitaka Miembeni ifungwe na Simba, ili timu hiyo kongwe isonge mbele.

Kwa upande wake, Mwingereza Stewart amefungua mdomo baada ya kusikitishwa na tabia ya upangaji matokeo katika baadhi ya mechi zinazokikabili kikosi chake.

Stewart amelalamikia wazi mamlaka zinazosimamia michuano na waamuzi kwamba wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha timu fulani zinashinda hata kama hazina uwezo wa kufanya hivyo. Kocha huyo anazilenga Simba na Yanga, bila shaka.

Mwingereza huyo alitoa kauli hiyo wikiendi iliyopita baada ya kukerwa na namna michuano ya Kombe la Mapinduzi inavyoendeshwa. Anasema inaelekea michuano ilikuwa na lengo moja tu, kuhakikisha Simba na Yanga zinazonga mbele.

Mfano, katika mchezo kati ya Simba na Miembeni ambao ulionekana kuwa muhimu kwa Wekundu wa Msimbazi kushinda ili wasonge mbele, kiongozi wa Miembeni alikwenda katika benchi la wachezaji kutoa maelekezo – kisha Simba ikashinda.

Katika mchezo dhidi ya Azam, Yanga iliyopaswa kushinda ili isonge mbele, ilizidiwa katika kila idara na haikuwa ajabu ilipobamizwa mabao 3-0. Lakini katika hali ya kushangaza, waandaaji wa michuano wakaamua kumsimamisha mwamuzi wa mchezo ule Ramadhan Kibo, kwa madai ya uchezeshaji mbovu.

Hapo ndipo Stewart aling’aka, “Uchezeshaji mbovu upi?” Inawezekana hakufuata maelezo ya mabosi wake; chumbani aliwasikiliza wakitakacho lakini alipoingia uwanjani alifuata kanuni za soka.

Hiki kinachotokea sasa cha kutaka Simba na Yanga zisonge mbele katika kila michuano iwe ya ndani au ile ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati zaidi hulenga mapato, lakini si kuinua kiwango cha soka.

Kwa maneno mengine upangaji matokeo kama huu ndio unadumaza soka yetu. Ushindi wa kubebwa nyumbani ndio unazifanya klabu mbili hizi zenye utani wa jadi kushindwa kutamba kimataifa.

Tazama Yanga imewahi kufika robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1969 na ikatolewa na Asante Kotoko ya Ghana kwa shilingi na mara ya pili kufikia tena ni mwaka 1998 ilipobadilishwa na kuitwa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mafanikio ya Simba; mwaka 1974 ilifika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika ikatolewa kwa penalti 3-0 na Mehla Al Kubra ya Misri, halafu mwaka 2003. Mwaka 1993 ilifika fainali ya Kombe la CAF ikachapwa 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast. Ajabu ni kwamba katika Kombe la Kagame, Simba imeshinda mara sita na mara zote michuano ikifanyika nchini.

Zaidi ya miaka 15 sasa, hakuna timu iliyofika hatua ya fainali ya michuano yoyote ya Caf. Sababu kubwa ni ukiritimba, ulimbukeni na ubabaishaji uliojaa midomoni mwa wanaojifanya Simba na Yanga ni timu zao. Hao hupenda kujiita watu wa mpira.

Wiki iliyopita niliandika makala “Kitakachoziponza Simba, Yanga” katika Kombe la Mapinduzi na mechi za kimataifa kutokana na maandalizi duni. Nguvu nyingi zinawekwa katika kuhakikisha timu hizo zinasonga mbele kwa mbinu zisizo za ndani ya uwanja.

Kabla ya Kombe la Mapinduzi, Simba na Yanga hazikuwa na mazoezi ya kutosha kuweza kuhimili mikikimikiki ya timu zilizojiandaa vizuri kama Azam, Miembeni, KMKM, Kikwajuni na Mafunzo.

Kwa kujua udhaifu wa timu hizi, watendaji wa soka ambao hawazitakii mema Simba na Yanga, ndipo wakalazimisha zishinde katika michezo ambayo zimezidiwa kiuwezo. Zitatamba ndani ya mipaka ya Tanzania na Afrika Mashariki pekee, lakini hazina uwezo kwingineko.

Simba na Yanga zina bahati kwamba mfumo wa soka unazipendelea hivyo zinaweza kulazimisha ushindi na zisiadhibiwe. Lakini mfano mzuri wa madhara ya kubwebwa uko kwa Olympique de Marseille ya Ufaransa. Mwaka 1993 ilitwaa kwa mara ya kwanza ubingwa wa Ulaya, lakini ilipogundulika Rais wake, Bernard Tapie alikuwa anahonga, timu ilishushwa daraja.

Kwa Simba na Yanga yaonekana wazi watu wa benchi la ufundi wenye uelewa na mapenzi ya kweli katika soka ni wachache, wengi ni wababaishaji na wabakaji wa mpira wa miguu. Hata hivyo wajue kwamba ushindi wa mbeleko ni aibu kwao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: