Uspika unamzuzua Job Ndugai


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Tafakuri

UONGOZI haujawahi kuwa kitu rahisi. Wanafalsafa wengi wamejadili sifa za uongozi au kiongozi, lakini kila mmoja alifikia hitimisho lake kulingana na alichotaka kulenga.

Hata hivyo, katika historia ya mwanadamu, tawala zote, ziwe za kiimla au za kidemokrasia, yapo mambo ya kimsingi sana ambayo hutazamwa kwa kila ayebahatika kuwa kiongozi. Sifa hizi ni lazima ijulikane kuwa ni ziada juu ya zile ambazo zimeandikwa au kukubalika katika kuendesha mambo.

Mwalimu Nyerere ni aina ya viongozi ambayo huenda Tanzania haitashuhudia tena katika uhai wake; hii ni kutokana na Nyerere kuwa na sifa nyingi za ziada za uongozi.

Nyerere anaweza kutazamwa kama mwanasiasa kiongozi, lakini pia kama kiongozi mwanafalsafa. Ni wakati gani alikuwa anatumia kipi, wapi na kwa nini ni suala la mjadala tofauti na wa leo.

Hata hivyo, tunapojitazama kama taifa kujitawala kwetu kunaakisiwa zaidi na jinsi Bunge linavyojiendesha kwa sababu ni katika chombo hicho wale waliopewa ridhaa na wananchi kuongoza, huwa wanatazamwa na kuhojiwa kama kweli wanakwenda sawasawa na matarajio ya wananchi.

Katika mfumo wa Bunge la Tanzania kujiendesha kwa uwazi, unawafanya wabunge kuwa na changamoto kubwa sana, moja kujipima wenyewe katika uwajibikaji wao ndani ya chombo hicho, lakini pia uwajibikaji huo hujidhihirisha katika kukidhi matakwa makuu matatu ya uwakilishi.

Mosi, uwakilishi wa wapigakura; pili, uwakilishi wa chama chake kwa kuwa ndicho kimemdhamini; tatu, utetezi wa maslahi yake kama mwanasiasa na binadamu mwenye mahitaji kadha wa kadha.

Kwa bahati mbaya, katika utekelezaji wa majukumu haya, siku baada ya siku, umma umeshuhudia mikwaruzano miongoni mwa wabunge (wabunge wenyewe kwa wenyewe), na kwa bahati mbaya zaidi baina ya wabunge na kiti (Spika, Naibu Spika au Wenyeviti wa Bunge).

Katika mikwaruzo hii, kwa kiasi kikubwa sana kiti mara nyingi kimekuwa sababu ya mparaganyiko wa mambo.

Katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma kwa sasa, maamuzi mengi ambayo ama yamelalamikiwa au kuamsha mijadala ndani na nje ya Bunge ambayo yametolewa na viti, yamethibitisha kitu kimoja kikubwa; nia ya kiti kutaka kujijengea uhalali wa kuwako sasa na kuamini zaidi na kundi moja kwa nia manufaa ya mbele ya safari.

Katika kundi la wabunge wanaokalia kiti cha spika, mbali na Spika Anne Makinda, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa kujua au kutokujua wamekuwa wakidhihirisha rangi mbili kuu zinazoashiria kuwa uongozi siyo kitu chepesi sana.

Nitafafanua. Katika mkutano wa bajeti wa mwaka jana yaani Juni –Agosti 2011, ulitokea mgogoro kati ya serikaki na Bunge kuhusu kitendo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, kuchangisha fedha kutoka taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo, kisha aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kuingilia kati na kumsafisha Jairo chapchap.

Ndugai alikuwa mbogo bungeni akiendesha kikao cha Bunge. Alisema, “Kama wamezoea kuchezeana ni huko huko (serikalini) lakini siyo bungeni”.

Ndugai alisema hayo wakati ilipoundwa kamati ya Bunge kuchunguza kadhia ya Jairo. Kwa hakika kauli ya Ndugai kwa muhimili mwingine wa dola ‘kwamba kama wamezoea kuchezeana ni huko huko’ ilikusudia kujitafutia uhalali wa kuwaongoza wabunge kwamba yeye ndiye nguzo yao hasa ya sasa na huko tuendako.

Nimekuwa namtazama na kutafakari sana maamuzi mbalimbali ya Ndugai katika mkutano wa Bunge wa sasa unaoendelea Dodoma, lakini ninachokiona kwa hakika, siyo juhudi ya kutekeleza kazi za unaibu spika ila ni kama yuko kwenye kampeni kali ya kujipanga kwa ajili ya nafasi kubwa zaidi mbele ya safari.

Kila nikimtazama sana ninajifikisha kwenye hitimisho kwamba Ndugai ameanza kutafuta uspika mapema.

Tunajua Makinda hana mpango wa kurudi kwenye ubunge na pia hana mpango wa kutetea kiti cha uspika mwaka 2015 baada ya uchaguzi mkuu, kwa maana hiyo Ndugai anajaribu kujenga njia yake hasa kwa wabunge wa CCM kuwa yeye ni wao na kwa maana hiyo atakuwa wao.

Wiki iliyopita, Ndugai aliwapeleka wabunge wawili wa CHADEMA, John Mnyika (Ubungo) na Tundu Lissu (Singida Mashariki) kwenye kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka kwa maelezo kuwa walikuwa wamesema  uongo bungeni.

Ni wiki hiyo hiyo, Ndugai alikuwa amemtimua bungeni Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk. Faustine Ndungulile, siku ambayo pia alimtukana Mbunge wa Kawe (CHADEMA), Halima Mdee, kwa kumwita kituko.

Ndugai amekuwa mwepesi wa kupandwa na hasira, amekosa uvumilivu mara nyingi na husema maneno ambayo kwa hakika yanaudhi sana wengine.

Ni jambo la bahati mbaya, kwamba Ndugai tofauti na wenyeviti wa Bunge ambao japo nao wameonyesha kuyumba kwa kiwango cha juu kabisa kama Sylvester Mabumba, ana uzoefu zaidi wa kuongoza Bunge tangu zama za Spika wa Kasi na Viwango, Samuel Sitta.

Alipokuwa mwenyekiti wa Bunge wakati wa Sitta, alikuwa ‘mnazi’ kupita kiasi na ‘unazi’ huu siyo wa bure tu. Kuna kitu anawinda.

Nilifuatilia mjadala ulioendeshwa na kituo cha Star Tv Jumapili iliyopita ambao uliwakutanisha Ndugai, Lissu na Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali.

Katika mjadala ule, Ndugai alionekana dhahiri anahamisha nguzo za magoli kwa faida yake. Suala la je, magazeti ni miongoni mwa vyanzo vya habari vinavyokubalika kuwasilishwa au kunukuliwa bungeni kama ushahidi wa kile anachosema mbunge, Ndugai alisema siyo.

Ndugai alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa ushahidi wa bungeni ni sawa na wa mahakamani, kwa mawazo yake magazeti hayakubaliki.

Baada ya kauli ya Ndugai, Lissu alifungua kitabu cha kanuni za Bunge ambacho alikuwa nacho pale pale, na kurejea kanuni ya 63 kifungu kinachoeleza wazi kwamba magazeti yanaruhusiwa.

Lakini wakati Lisu akisoma kanuni hiyo, Ndugai kwa kejeli akasema “MwanaHalisi ?” hilo ni tabloid. Sikumwelewa alikusudia nini.

Kwa haraka nikafikiri, kwa Ndugai, MwanaHalisi siyo gazeti la kuaminika, ingawaje katika Bunge hilo hilo magazeti mengine mengi tu yamekuwa yakiwasilishwa kama ushahidi.

Siyo hayo tu, katika historia ya Bunge zipo kamati teule nyingi zimekwisha kuundwa kuchunguza sakata nyingi ambazo zilianza kufichuliwa na magazeti.

Lakini ukipiga hatua kubwa mbele, juu ya Ndugai kukataa kuamini taarifa za kwenye vyombo vya habari, ninashindwa kujua kwa yakini nini maana ya kurusha vikao vya Bunge moja kwa moja kwenye televisheni kama vyombo vya habari haviaminiki kiasi hicho.

Kitu ambacho Ndugai hajui ni kwamba hata katika mjadala huo uliokuwa unaendelea kwenye Star Tv, ni chombo cha habari kilichomsaidia kuufikisha ujumbe huo kwa umma.

Najua kinachomsumbua ni kitu kimoja, kujiandalia njia kuelekea kwenye uspika huku akikanyaga wengine na kutumia vibaya kiti.

Mwalimu Nyerere alipata kusema kuwa katiba ya Tanzania ilikuwa imempa madaraka makubwa sana ya kuweza kuwa dikteta, lakini hakuyatumia.

Ndugai ameonja Unaibu Spika kwa miaka miwili na ushei, sasa anajitazama anatamani uspika kwa kasi kubwa, lakini kwa staili yake ya kukanyanga wenzake na kuibeba kambi moja ndani ya Bunge dhidi ya nyingine, kwa mwendo huu ninashindwa kujizui kuhitimisha kwamba namuona Ndugai kama kiongozi hatari, akiwa na madaraka makubwa zaidi itakuwaje?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: