Uswahiba kati ya Waasia na CCM


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

SINA nia ya kuzungumzia Watanzania wenye asili ya Kiasia kwa lengo la kuibua hisia za kibaguzi, la hasha, bali ni kwa sababu ya historia yake na umuhimu wa nafasi yao katika uchumi wa nchi hii.

Raia hawa ninaowazungumzia ni wale wenye asili ya India na Pakistan.

Kwa kiasi kikubwa hawa ndio wanashikilia sekta ya biashara na pia viwanda, na hivyo ni jamii muhimu katika maendeleo ya uchumi, na pia kama waajiri wakuu hapa nchini.

Hivyo, lengo langu ni kuufahamisha umma mwelekeo wake katika masuala ya siasa za vyama vingi hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi, na mahusiano yao na viongozi waliopo madarakani sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) .

Tangu uanzishwaji wa mfumo wa vyama vingi raia hawa wamekuwa wanajihusisha sana na siasa, huku wakiendelea kushikilia shughuli zao za kibiashara.

Aidha, nitakuwa sisemi ukweli iwapo nitapuuzia jinsi baadhi yao ambavyo wamekuwa wakitajwa katika tuhuma mbali mbali kuhusu ufisadi wakishirikiana na raia wengine wazalendo. 

Jamii ya Kiasia nchini Tanzania ina historia kubwa na ya kipekee. Kamusi huru ya Wikipedia (kuhusu Tanzania) inataja idadi ya jamii ya Kiasia nchini kuwa 50,000 kwa makadirio ya mwaka 1994. Hii ni kufuatana na ripoti ya Idara ya Nchi za Nje ya Marekani (US Department of State) ya mwaka 2008/09.

Historia yao kwa ufupi sana ni kwamba waliingia nchini (Tanganyika wakati huo) wakati wa ukoloni wa Kiingereza katika miaka ya 1920 baada ya Vita Vikuu ya Kwanza iliyoisha 1918.

Wengi wao waliletwa na Waingereza nchini Kenya kutoka Bara Hindi (iliyokuwa inatawaliwa na Waingereza) mwishoni mwa karne ya 19 kama vibarua katika ujenzi wa reli ya Kenya hadi Uganda. Kipindi hicho nchi za Kenya na Uganda zilikuwa makoloni ya Uingereza.

Baada ya ujenzi wa reli hiyo, baadhi yao waliamua kulowea katika nchi hizo (Kenya na Uganda) na wengine kuja Tanganyika baada ya Waingereza kuikamata nchi kutoka kwa wakoloni wenzao wa Kijerumani.

Chini ya utawala wa kikoloni, watu wa jamii hii ya Kiasia waliwekwa katika tabaka la pili– la kwanza likiwa la wakoloni wenyewe, na la tatu wazalendo weusi.

Harakati za kudai uhuru zilipoanza wengi wao waliingiwa na wasiwasi kuhusu hatma yao, na hivyo waliamua kuchukua uraia wa Uingereza na kupewa hati maalum za kusafiria za nchi hiyo. Wengine wachache waliamua kuwa raia wa Tanganyika huru kufuatana na masharti ya Sheria ya Uraia iliyowekwa baada ya uhuru.

Baada ya uhuru, Waasia waliochukua uraia wa Uingereza walijikuta wageni katika nchi yao na lilikuwa jukumu la serikali ya Uingereza kuwachukua. Matukio mawili muhimu yalibadilisha hali hii.

Mwezi Januari 1971 serikali ya Milton Obote nchini Uganda ilipinduliwa na Jenerali Idi Amin. Baada ya mapinduzi, Idi Amin alitangaza kuwafukuza nchini humo wakazi wote wa asili ya Kiasia waliokwa raia wa Uingereza, akiwarushia tuhuma mbali mbali, ufisadi, kutolipa kodi na kuficha bidhaa.

Miezi minne tu ya mapinduzi ya kijeshi ya Uganda, yaani Aprili 1971, serikali ya Tanzania ilitaifisha majumba, mengi yalikuwa yanamilikiwa na watu wa asili ya Kiasia. Utaifishaji wa majumba hayo ulifuatia Sheria ya Utaifishaji Majumba iliyopitishwa na Bunge kwa spidi ya zimamoto.

Ingawa haikuwekwa wazi, lakini kutaifishwa kwa majumba kulikuwa na uhusiano na matukio ya Uganda. Katika sera ya kuziweka njia kuu za uchumi mikononi mwa umma chini ya Azimio la Arusha lililotangazwa mwaka 1967, utaifishaji wa majumba haukuorodheshwa, kwani haukuonekana kama ni njia kuu.

Mengi ya majumba hayo yalikuwa yanamilikiwa na mtu mmoja mmoja, na siyo makampuni. Hatua ya Idi Amin ya kuwapa wazalendo biashara zilizokuwa zinamilikiwa na Waasia ilikuwa inaisuta serikali ya Nyerere na sera yake ya ujamaaa ambaye naye aliamua kuyataifisha majumba na kuyaweka chini ya umma.

Aidha, Nyerere pia alihofu naye kupinduliwa pia – huku kukiwa na kumbukumbu ya jaribio la kwanza la kutaka kumpindua mwaka uliotangulia tu – la akina Oscar Kambona na Bibi Titi.

Lakini tofauti na Uganda, majumba yaliyotaifishwa hapa Tanzania yaliendelea kukaliwa na hao hao wamiliki wa zamani na jamaa zao kwa kupanga na kufanyia biashara pia hadi leo hii.

Wazalendo wachache tu ndio wamebahatika kupanga katika majengo hayo, huku wengi wamekuwa wakiyaingia kama wafanyakazi tu wa madukani au watumishi wa ndani.

Aidha, (sintakosea nikisema) wananchi wengi hawajui iwapo serikali yao inamiliki majumba hayo.

Si siri kwamba wengi wa watu wa jamii hiyo ya Kiasia wanaishi katika dunia ya peke yao – ya hali nzuri na utajiri mkubwa – tofauti na mamilioni ya wazalendo.

Pamoja na athari walizopata kiuchumi, na pengine kisaikolojia kutokana na kutaifishwa kwa majumba yao hali kadhalika makampuni na baadhi ya biashara zao kufuatia ule utekelezaji wa sera ya Ujamaa, hadi leo hii jamii hiyo ni waumini na wafuasi wakubwa wa chama tawala – CCM.

Uchunguzi unaonyesha katika uchaguzi wa kesho karibu asilimia 98 wa raia wenye asili ya kiasia wataipigia CCM bila wasiwasi wowote.

Tofauti na mamilioni ya Watanzania wengi wenye hali duni na ambao wangependa kuona mabadiliko, jamii ya Kiasia haipendi kuona mabadiliko yoyote ya kisiasa au ya kiuchumi kwa hofu ya kuathiri biashara zao na namna ya maisha yao ya anasa. Na katika kuhakikisha hilo, wale matajiri wakubwa wamekuwa wakikichangia chama hicho hasa katika chaguzi.

Baadhi yao wameingia katika siasa, wengi wao katika chama tawala na kufanikiwa kuingia bungeni na katika nyadhifa za juu ya chama.

Lakini kikubwa ambacho kimekuwa kinajitokeza katika miaka ya karibuni ni kwa baadhi yao kutajwa sana kwa kujihusisha na ufisadi katika ngazi za juu wakishirikiana na maafisa wakuu wa chama tawala na serikali.

Wametajwa katika kashfa kadha za kifisadi kama vile Richmond, EPA, rada na nyinginezo. Wachunguzi wa masuala haya wanasema, katika ufisadi hasa mkubwa, viongozi wa juu wa serikali wanawaamini sana watu wa jamii hii katika kuweka siri kuliko wazalendo wenzao.

Na siyo hilo tu, kikundi kimoja kidogo cha watu watano katika jamii hii kinachojumuisha baadhi ya watajwa wa kashfa za ufisadi chenye uwezo mkubwa wa kifedha, kina ushawishi mkubwa sana katika masuala ya siasa ya nchi hii.

0
No votes yet