Utabiri wa Sumaye umeanza kutimia


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 14 December 2011

Printer-friendly version

BAADA ya kuandamwa vilivyo akiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano katika serikali ya awamu ya tatu kuanzia mwaka 1995-2005, Frederick Sumaye, alitoa angalizo wakati wa joto kusaka mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2005 lilipokuwa limepanda sana.

Sumaye ambaye hakika alikuwa ametwishwa tuhuma nyingi chini ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa, alikutana na waandishi wa habari pamoja na mambo mengine kutangaza hadharani nia ya kuwania kiti cha urais, alionya kwamba alikuwa amechoshwa na tuhuma dhidi yake na kwamba alikuwa amejitoa kueleza kwamba asingevumilia tena upakaziaji dhidi yake.

Hata hivyo, alitoa angalizo muhimu ambalo katika miaka ya hivi karibuni ni kama linatimia kwa kasi kubwa. Alisema: “Waogopeni wanaotumia magazeti kuingia madarakani, kwa kuwa wakishayapata watatumia risasi kusalia madarakani.”

Sumaye hakumtaja mtu mahususi, ila alionyesha kuwa tuhuma alizokuwa anashushiwa zilikuwa zimetengenezwa na watu ndani ya chama chake (CCM) kwa kutumia magazeti ili wampiku na kutwaa urais.

Ukitazama mlolongo wa mambo ndani ya nchi kwa sasa, kuna kila dalili kwamba kile alichosema Sumaye kinaanza kutimia kwa kasi, matumizi ya nguvu za kipolisi na njama za kutengenezeana kesi kwa wale wote wanaoonekana kuikosoa serikali ni vitendo ambavyo havina hesabu.

Waathirika wakuu wa vitendo hivi vya kulinda utawala kwa gharama zote, ikiwamo matumizi ya risasi, ni wabunge. Imeonekena kuwa idadi ya kesi zilizofunguliwa dhidi ya wabunge wa kambi ya upinzani ni sehemu ya mkakati huo. Zipo kesi nyingi mno. Polisi wametumika mara kadhaa kuwadhalilisha na kuwasumbua wabunge wa vyama vya upinzani pale wanapozungumza au kushiriki katika mikutano na maandamano ambayo ni haki yao.

Wapo waliofunguliwa kesi za kijinga sana kama vile kuzidisha muda wa kuhutubia wananchi kwa dakika 15 hivi; wapo waliokamatwa na kufikishwa polisi, mabomu ya machozi kutumika na hata risasi za moto kurindima kwa kuwa tu wabunge hao walisimama mahali na kuzungumza na wananchi.

Baada ya kampeni kali dhidi ya wabunge na wanasiasa kwa ujumla kupamba moto, sasa moto unaelekezwa kwa vyombo vya habari. Serikali inaonekana kila siku iendayo kwa Muumba ikikosa uvumilivu juu ya haki na uhuru wa habari. Vyombo vya habari vinatishwa kwa njia mbalimbali, waandishi nao wanakutana na vitisho vya kidola, na hata wahariri nao wanatiwa misukosuko si kwa sababu nyingine yoyote isipokuwa kwa kuwa tu wameamua kuwa wakweli, kuacha ukweli usambae na usomwe na kuonekana na kila mmoja.

Ni kwa nini serikali imeamua kuchukua mwelekeo huu mpya? Jibu ni jepesi sana, imeshindwa. Serikali imeshindwa sana. Imeshindwa katika mambo mengi hata yale ambayo hayahitaji maarifa mpya wala fedha nyingi kuyasimamia ili yatekelezwe.

Nitatoa mifano michache. Serikali hii ilisema haitakuwa na mchezo na wala rushwa, ukweli wa mambo ni kwamba si tu imeacha kuwa na mchezo wowote na wala rushwa bali pia imewakimbia na kujificha na kuawaacha wala rushwa wakitamba. Ni ukweli usiokuwa na chembe ya shaka kwamba rushwa imezidi kuota mizizi nchini katika kipindi hiki. Kila mahali huduma kwa umma zinapotolewa, rushwa ni lazima.

Wapo watuhumiwa wakubwa, majabali wa rushwa, mapapa ambao wanajulikana kwa vitendo vyao vya ulaji rushwa, utajiri wa kutupwa wenye kutiliwa shaka, hawa wanaitisha serikali na haiwezi hata kuwagusa. Wapo wengi tu. Serikali inawaogopa na badala ya kushughulika nao, inawaandama wabunge wa upinzani na vyombo vya habari vinavyopiga kelele kuhusu ufisadi na kushindwa kwa serikali nia ikiwa ni kuwanyamazisha.

Serikali imeshindwa kuwaelekeza wananchi kujiletea maendeleo yao; imeshindwa kuwajengea mazingira ila maisha bora kwa kila Mtanzania yawezekane; matokeo yake, serikali ikihojiwa juu ya kushindwa kwake inakuwa mbogo, inatisha wananchi na watawala wanafikia hatua ya kutamani kuwa madikteta.

Siku baada ya siku serikali inathibitisha kwa vitendo halisi kwamba haipo pamoja na wananchi wake, mfano mmojawapo ni uteuzi wa viongozi katika nafasi za uteuzi, wakuu wa mikoa na mabalozi. Wale wote ambao wananchi walisema hapana katika nafasi za uongozi ndio wanachukuliwa, ndio wanaonekana kuwa wanaweza na kufaa kutekeleza majukumu ya umma. Maamuzi ya kiutawala ya kuteua watu wote waliokataliwa na wananchi ni kielelezo cha kuwapuuza na kuwakejeli wananchi, ni kielelezo kingine cha ubabe na kutokujali hisia na matarajio ya wananchi.

Watawala wasiojali hisia na matarajio za wananchi ambao kimsingi ni waajiri, ni utawala wa kibabe. Ni utawala usiojali na kwa maneno mengine ni utawala unaokwenda kinyume cha matakwa ya umma, huu ni utawala uliojiamulia kufuata njia yake mbali na wananchi.

Jeuri ya watawala hawa inatoka wapi? Ni jeuri na matokeo ya kujiegemeza kwenye nguvu za dola, kwenye kamatakamata, kwenye ufunguaji na utungaji wa mashitaka ya kudhalilisha na kutaka kulazimisha kukubalika hata katika mambo ambayo ni dhahiri watalawa wameshindwa.

Watawala wenye jeuri ya kuwaambia wafanyakazi kuwa watawafukuza kazi kwa kuwa wanadai haki yao, watawala ambao wameshindwa kutatua kero za wanafunzi wa elimu ya juu na badala yake kubuni mikakati ya kuwafukuza usiku na mchana kwa kuwa tu wanadai haki zao, ni utawala ulioshindwa.

Watawala wambao wanashindwa kutimiza ahadi zake nyingi, hujawa na hasira kila wanapokumbushwa kwa kuulizwa mfano ulipo umeme wa hakika, zilipo ajira za vijana, ilipo mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, yalipo malimbikizo ya mishahara ya walimu, kutaja kwa uchache tu.

Kwa kuwa watawala hawana majibu ya maswali haya, njia pekee ya kujinusuru na maswali magumu ya haki kutoka kwa wananchi, ni kujitia jeuri, kutumia nguvu za dola kunyamazisha kila sauti inayopazwa dhidi yake. Mwendo huu ni mwelekeo halisi wa utabiri wa Sumaye wa mwaka 2005, kwamba baada ya kutumia magazeti kuingia madarakani watatumia risasi kusalia madarakani.

0
No votes yet