Utafiti wa dawa ya ukimwi usichochee ngono zembe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 21 July 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KWA muda wa wiki moja iliyopita kumekuwa na habari njema juu ya maendeleo ya utafiti wa dawa ya kuzuia na kutibu ugonjwa wa ukimwi.

Vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti kwamba wanasayansi watafiti wa dawa kutoka Marekani, wamefanikiwa kupata dawa inayoaminika ina uwezo wa kuzuia maambukizi mapya na kutibu ugonjwa huo.

Hata hivyo, katika taarifa yao kwenye Kongamano la 43 la Kimataifa kuhusu Mapambano dhidi ya Ukimwi, watafitii hao wametaja mambo makuu matatu ya kuzingatia ili tiba hiyo iweze kufanya kazi kwa mgonjwa.

Kwanza wamesema wanaotaka kutumia dawa hiyo wanapaswa kupima ili kujua afya zao kwa vile dawa hiyo hutegemea pia muda wa maambukizi.

Pili wanapaswa kuwatibu wagonjwa wa ukimwi, na tatu kuachana na dawa za kurefusha maisha zinazotumika kwa sasa.

Habari hizo zitakuwa zimepokewa kwa furaha sana na waathirika wakiamini siku za kuteseka kwao kutokana na ugonjwa huo zinatibika.

Japokuwa taarifa za utafiti huo zinatoa matumaini juu ya maendeleo ya utafiti huo, tunapenda kuonya kuwa habari za mafanikio hayo zisitumike kama tiketi ya watu kujiachia na kufanya ngono zembe.

Wananchi wafahamu kwamba, hata kama wanasayansi watathibitisha pasi na shaka kwamba dawa hiyo inatibu au inazuia maambukizi mapya, hiyo haitakuwa suluhu kwa ugonjwa huo ambao tunaamini mpaka sasa hauna chanjo wala tiba.

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba habari za kupatikana dawa ni jambo moja, suala la dawa kufanya kazi yaani kutibu na kuzuia maambukizi ni jambo jingine.

Isitoshe dawa hiyo bado iko katika hatua za utafiti tu, itachukua muda mrefu kufikia kuthibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili ianze kutengenezwa kwa wingi na kusambazwa duniani kote.

Ikumbukwe pia kwamba ugonjwa kama wa malaria una dawa nyingi, lakini bado unaongoza kwa vifo hasa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Hivyo, dawa hiyo, inaweza isiwe suluhisho la kudumu.

Kutokana na hali hiyo, tunawashauri vijana kwa wazee, wake kwa waume waendelee kuzingatia kanuni za sasa za kujizuia kuwa na wapenzi wengi, kujizuia kufanya ngono zembe. Tunashauri wasubiri, wawe na mpenzi mmoja na ikiwa watashindwa basi watumie kinga.

0
No votes yet