Utambuzi raia usichezewe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 11 January 2012

Printer-friendly version

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanza usajili wa wananchi wa Tanzania. Itasajili pia wageni wanaoishi nchini.

Hii ni hatua ya mwanzo kuelekea utoaji wa vitambulisho kwa kila Mtanzania na kila mgeni anayeishi nchini. Awamu ya kwanza ya utoaji vitambulisho  itakuwa Aprili mwaka huu.

Mradi wa utoaji wa vitambulisho vya taifa umekuwa simulizi kwa muda mrefu sasa. Lakini baada ya serikali kuanzisha mamlaka mahsusi kuratibu jambo hili, nuru imewadia kwa kuanza rasmi kwa utambuzi na usajili wa watu.

Utambuzi na usajili vinakwenda sambamba. Utambuzi na usajili utawezesha serikali kutambua wananchi na wageni: Kwamba nani ni nani; yuko wapi; anafanya nini; na huyo anayesajiliwa anamiliki nini?

Mfumo wa utambuzi na usajili utahusisha pia wageni waliopatiwa vibali vya kuishi nchini. Utambuzi na usajili kwa wageni utabainisha aliyepewa kibali ana haki au anastahili kuendelea kumiliki kibali alichonacho?

Huu ndio wakati wa ukweli kudhihiri na uongo kujitenga. Kwanini tuseme hivyo? Kumekuwa na mazoea ya miaka mingi ya wageni kupata haki wanazostahili kupata Watanzania, kwa kutumia mbinu chafu.

Inajulikana baadhi ya watu wanaomiliki pasipoti si raia halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Walipataje hati hizi? Hili ndilo swali linalokaribia kupatiwa dawa.

Mamlaka itatoa vitambulisho katika makundi makuu matatu – Watanzania, wageni wakaazi na wakimbizi.

Mfumo mzima wa utambuzi na usajili wa watu wote wanaoishi ndani ya nchi yetu utafanywa kwa ushirikiano na taasisi nyingine mbalimbali chini ya NIDA wenyewe ambao ndio wasimamizi wakuu.

Washirika wa kazi hii ni Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, TAMISEMI, itakayoshughulikia utambuzi wa watu; Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) atakayeshughulikia usajili kwa upande wa Bara na Mrajis Mkuu wa Vizazi na Vifo wa Zanzibar atakayesimamia usajili kwa upande wa Zanzibar.

Uhakiki wa watu waliosajiliwa utafanywa na Idara ya Uhamiaji.

Utambuzi na usajili pamoja na hatua ya mwisho ya utaoji wa vitambulisho katika mradi mzima wa vitambulisho vya taifa una manufaa makuba kiuchumi, kisiasa na kijamii. Suala la usalama wa nchi nalo lina umuhimu wa aina ya kipekee katika mradi huu.

Kusajili kila mwananchi kuna matatizo yake maana wapo watakaotoa taarifa za uongo ili kulaghai watendaji husika waamini kuwa wamekuwa raia halali wa Tanzania.

Ratiba ya NIDA inaonesha kuwa utambuzi na usajili utaanzia kwa wafanyakazi wa serikali na taasisi zake. Watafuatia wafanyabiashara kabla ya kundi kubwa la wananchi wa kawaida kuguswa.

Muingiliano wa watu katika kanda hii ya Afrika Mashariki, na hata mataifa yaliyo karibu na kanda yetu, umekuwa mkubwa kiasi kwamba ni vigumu kumtambua mtu kwa kumuona sura kuwa ni raia au si raia.

Uongozi wa NIDA umesema wazi kuwa usajili na utambuzi unafanywa bila ya mtu kutakiwa kutoa kiasi chochote cha fedha. Wanaohusika kutambua na kusajili ni watumishi waliopewa tu mamlaka na NIDA.

0
No votes yet