Utata wagubika uandikishaji Z'bar


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 22 September 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

UANDIKISHAJI wapiga kura unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) unaendelea katika visiwa vya Unguja na Pemba . Lakini niseme mapema kwamba bado unakabiliwa na mazonge makubwa.

Mazingira yanayoonekana vituoni yanasikitisha kwani yanajenga taswira kwamba zoezi hili si huru hata kidogo. Askari ni wengi vituoni kuliko raia wanaopaswa kuandikishwa. Baadhi ya watu wanapelekwa vituoni na magari ya serikali, yakiwemo ya vyombo vya ulinzi na usalama.

Ila kwa Zanzibar, haya ni mazingira yasiyoshangaza. Kinachotokea vituoni, kinathibitisha mantiki ya kauli walizotoa viongozi wa serikali tangu uandikishaji ulipokwama Pemba kufuatia vurugu.

Mawaziri wa serikali ya Zanzibar ambao walichukizwa na uamuzi wa Tume kusitisha uandikishaji uliokuwa umeanza 6 Agosti kisiwani Pemba, walisema uandikishaji utakapoanza tena, serikali itaimarisha ulinzi vituoni na katika maeneo ya nje ya vituo.

Maana ya uimarishaji ulinzi kwao ni kuongeza idadi ya askari. Tatizo la serikali ni kuamini kwamba ulinzi ni idadi kubwa ya askari wenye silaha za moto.

Mbaya zaidi ni kwamba kwa SMZ, askari siyo tu wale wa jeshi la Polisi ambao wamepata mafunzo ya uaskari na maadili ya utendaji kazi. Hawa ni tofauti na askari wa vikosi maalum vilivyoanzishwa na serikali.

SMZ ina vikosi vitano vya ulinzi: Chuo cha Mafunzo (KMF) au Magereza kama vilivyozoeleka kuitwa; Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM); Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU); Kikosi cha Zimamoto na Uokozi (KZU) na Valantia (KVZ).

Askari wanaokutwa kituoni inafikia 60 na wengi wao hubeba bunduki zenye risasi za moto. Kati yao, polisi hawazidi 15. Waliobaki ni wale wa vikosi vya SMZ ambao hawana mafunzo ya kazi wala ujuzi wa sheria na maadili ya utu.

Askari wa SMZ hawakufundishwa haki za raia, bali wamefundishwa kutii amri hata ikiwa imetoka kwa aliyevaa kijaji na nyeusi, kwao ni halali.

Asili ya kazi ya uaskari ni kutii amri ya mkuu wako; lakini wanatii hata amri haramu. Hawajali yanayotokea kwingineko duniani ya askari kushitakiwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa kutii amri zilizokiuka sheria na haki za binadamu.

Kuna matukio mengi ya watu kujeruhiwa kwa kupigwa na baadhi ya askari hao. Kuna hata madai ya mauwaji yanayodaiwa kufanywa na askari hawa.

Mazingira mabaya yanayotawala kwenye vituo vya uandikishaji, yanajenga taswira kuwa uandikishaji ambao ni zoezi la kiraia unafanyika kimabavu na si tena zoezi la kiraia.

Kama zoezi hili halikudhibitiwa na dola kijeshi, kwanini kwenye vituo vya uandikishaji kuwe na askari wengi tena wenye silaha? Kwanini zana za kijeshi kama vile vifaru na magari ya deraya yanaopeperusha vitambaa vyekundu zioneshwe mitaani na maeneo ya karibu na vituo vya uandikishaji?

Majibu ya maswali haya ni rahisi: Uandikishaji unafanywa ndani ya shinikizo za kisiasa zinazopangwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kinataka kuendelea kung’ang’ania madaraka hata ikibidi kuua raia kama ilivyotokea baada ya uchaguzi wa 2000.

Katika hali ya kawaida huwezi kuamini unapoambiwa kwamba baada ya ZEC kuanza tena uandikishaji, 12 Septemba, makundi ya watu wamekuwa wakipelekwa vituoni kwa kutumia magari ya serikali, yakiwemo ya vikosi vya ulinzi. Unakuta askari 50 wanasindikiza watu sita kuingia kituoni ili waandikishwe.

Baadhi ya watu wanaopelekwa kwa mtindo huu, wamenukuliwa wakisema wametoka mbali na majimbo walikopelekwa kujiandikisha. Wengine wameomba kusaidiwa kurudi makwao ili kukwepa kujulikana na kuchukuliwa hatua.

Haiwezekani watu hawa wakawa ni waliotumwa na vyama vya upinzani. Katika mazingira ya Zanzibar, ni jambo gumu mno kwa chama cha upinzani kupandikiza watu vituoni. Wanajua wakishikwa watashitakiwa.

Nazungumzia mazingira mabaya yaliomo maeneo ya vituo vya uandikishaji wapiga kura wanaokusudiwa kuingia katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) – wapiga kura watakaoshiriki kuchagua Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani wa Zanzibar .

Hofu yangu ni kwamba wapiga kura wanaoandikishwa na ZEC sasa, ndio walewale watakaokuja kuchagua mbunge na rais wa Tanzania katika uchaguzi unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

NEC hutegemea wapiga kura walioandikishwa katika daftari la Zanzibar. Yenyewe hupita baadaye kuandikisha wale Watanzania waliokosa sifa za kuandikishwa kwa ajili ya uchaguzi wa Zanzibar.

Katika uchaguzi uliopita, takwimu za NEC zinaonyesha ilipata watu 15,000 tu ilipopita kuandikisha wapiga kura baada ya kukamilika kwa uandikishaji wa daftari la Zanzibar.

Wakati unasikia kauli za kutia moyo upande wa NEC, yanayofanyika kupitia ZEC, ni mizengwe na vituko. Ungedhani katiba na sheria ndio zikaongoza zoezi la uandikishaji.

Wakati mtu anatakiwa kuwa na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi ndipo apate kuandikishwa kwa daftari la Zanzibar, mpiga kura aliyeko Tanzania Bara huandikwa akishaonesha uthibitisho wa kuzaliwa au shahada aliyotumia katika uchaguzi uliopita.

Katiba ya Zanzibar ya 1984 inatambua vielelezo hivi; lakini SMZ baada ya kushindwa mwaka 2005, iliingiza kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi mwaka 2006 kuwa ni sharti la mtu kuandikishwa kuwa mpiga kura Zanzibar.

Kitambulisho isingekuwa sharti baya kama kinatolewa kwa haki, tatizo ni kutolewa kibaguzi. Kwa sasa, kundi kubwa la Wazanzibari hawanacho na jitihada za kukipata zimegonga mwamba, hata kama serikali inasema imetoa kwa watu 503,895.

Ukiona maelfu ya watu wamefika vituoni na kurudishwa bila ya kuandikishwa kwa sababu hawana kitambulisho, hutakubalia serikali bali watu hawa. Huo ni uthibitisho usio shaka kuwa siku ya mwisho wa uandikishaji, maelfu yao watakuwa wameachwa nje ya daftari.

Mazingira mabaya katika vituo vya uandikishaji hayashangazi kwa Zanzibar. Haishangazi kusikia kauli tofauti kati ya viongozi wa ZEC na NEC inayoongozwa na Jaji Lewis Makame.

Tatizo la ZEC ni kwamba siyo tu ina usiri mkubwa katika utendaji wake, bali pia ndani yake kuna tume mbili: moja ya mwenyekiti na makamishna wake, na ya pili anayoongoza Mwenyekiti na mkurugenzi wa uchaguzi.

Angalau mtu unafurahi kusikia mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC anahamasisha watu wafike vituoni kuandikishwa. Mkurugenzi katika ZEC, Salum Kassim Ali, maneno yake mazuri ni "uchaguzi utafanyika hata wakiandikishwa watu watano." Amesema haya mbele ya waandishi wa habari.

Nataka hapa NEC ipate funzo kwamba kutegemea daftari la Zanzibar itaadhirika huko twendako. Hivyo ni vema ikatafakari na kinachotokea Zanzibar. Lazima haki ionekane inatendeka.

UANDIKISHAJI wapiga kura unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) unaendelea katika visiwa vya Unguja na Pemba
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: