Utata waibuka malipo ya Dowans


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 28 March 2012

Printer-friendly version

SERIKALI imekamilisha dhamana yake ya thamani ya dola 30 milioni (Sh. 48 bilioni) kuzuia ulipaji tozo kwa kampuni ya kufua umeme ya Dowans.

Tozo inayozuiwa ilitolewa na mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara (ICC) Novemba 2010.

ICC iliagiza Tanesco kulipa dola 65 milioni pamoja na riba na gharama kwa Dowans kutokana na Tanesco kuvunja mkataba wake wa kuzalisha umeme, Ubungo jijini Dar es Salaam.

Taarifa za Bodi ya Tanesco iliyokutana jijini Dar es Salaam 12 Machi 2012, zinasema tayari serikali imekubali kutoa dhamana hiyo, ili tozo hiyo isilipwe hadi rufaa waliyokata mahakama ya rufaa iamuliwe.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando ameithibitishia MwanaHALISI hatua ya kulipwa kwa dhamana hiyo.

Amesema hata wanasheria wanaowakilisha shirika lake katika shauri hilo wako jijini London, Uingereza na kwamba wanalipwa dola 90,000.

Akifafanua zaidi, Mwanasheria wa Tanesco, Godwin Ngwilimi, amesema awali Tanesco iliweka dhamana ya dola 5 milioni na sasa serikali imelipa dola 25 milioni. Dhama iliyokuwa inahitajika katika mahakama ya London, ni dola 30 milioni.

Mahakama hiyo ilitaka Tanesco kuweka dhamana hiyo ili kusitisha utekelezaji wa hukumu ya ICC kwa lengo la kusubiri rufaa inayoendelea katika mahakama ya rufaa Tanzania.

Shauri hilo lilifunguliwa na Dowans London, ikiomba kukazia hukumu ya ICC baada ya mahakama kuu nchini kutupa pingamizi la Tanesco lililokuwa likipinga kusajiliwa kwa tozo hiyo.

“Tulipoieleza mahakama ya London kuwa shauri la kupinga tozo bado linaendelea hapa kwetu, Jaji alisema kwa kuwa Tanesco ndiyo ilikuwa imeshindwa katika kesi, basi iweke dhamana hiyo ya dola 30 milioni ili kusimamisha shauri hilo,” alisema Ngwilimi.

Naye mwandishi wetu, Saed Kubenea, aliyeko South-End East, Uingereza anaripoti kuwa uvumi umeenea jijini humo miongoni mwa Watanzania kuwa tayari Dowans wameanza kumwagiwa mabilioni ya shilingi.

Makampuni yanayodaiwa kulipwa ni Dowans Holdings SA, Richmond Development Corporation (RDC) na Dowans Tanzania Limited (DTL).

Haya ni makampuni yanayowakilishwa na Rostam Aziz; mmoja wa maswahiba wa Rais Jakaya Kikwete na tayari walikuwa wamehusisha hatua ya malipo na “maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka 2015.”

Taarifa zilidai kuwa mabilioni hayo ya shilingi yameanza kulipwa kupitia Benki ya Ujerumani iitwayo Deutsche Bank AG, yenye tawi lake jijini London, Uingereza.

Kulipwa kwa fedha hizo kunafuatia makampuni ya Dowans kufungua shauri kwenye mahakama kupinga hatua ya serikali kuvunja mkataba yaliyourithi kutoka kampuni ya Richmond.

Serikali ilivunja mkataba na Dowans baada ya kujiridhisha kuwa kusainiwa na hata kuhuishwa kwake, kutoka Richmond kwenda Dowans, kulifanywa kinyume cha taratibu.

Hata hivyo, wakati wote wa mgogoro wa Richmond na wanaojiita Dowans Holdings SA, hakukuwa na kampuni ya Dowans Tanzania Limited ambayo ilifungua kesi ICC.

Hata hivyo, taarifa za Dowans kuanza kulipwa zimejengwa kwenye kumbukumbu za hatua ya haraka ya kampuni hiyo kupeleka ankara Hazina kudai malipo mara tu baada ya ICC kutoa uamuzi.

MwanaHALISI lilimuuliza waziri wa fedha, Mustafa Mkullo ambaye alithibitisha hazina kupokea ankara lakini alisema serikali ilikuwa haijatoa malipo.

Mbunge Victor Mwambalaswa ambaye ni mjumbe wa bodi ya Tanesco alipoulizwa kuhusu uwezekano wa serikali kuanza kulipa Dowans alisema kwa kadri anavyojua, hilo halijaanza kutekelezwa.

Mbunge huyo wa Lupa, wilayani Chunya, amesema hakuna fedha zozote zilizolipwa Dowans kwa kuzingatia tozo iliyotolewa na mahakama.

“Kwanza wewe nani amekwambia haya? Ninachojua ni kwamba fedha haziwezi kulipwa kwa kuwa shauri bado liko mahakamani,” alisema.

Alisema mtu atasema kwa kuwa ana mdomo tu, lakini hakuna fedha zozote zilizolipwa.

Wachunguzi wa mambo wanasema wangeshangazwa na hatua ya serikali kuilipa Dowans haraka wakati imeshindwa au imekataa kulipa wengi ambao madai yao yalishaamuliwa zamani na mahakama kuu na mahakama ya rufaa.

Miongoni mwa madai ambayo serikali imegoma kulipa ni yale ya mfanyabiashara mashuhuri nchini D.P. Valambia.

Kwa miaka 14 sasa, Valambia kupitia mawakili wake, amekuwa akihaha mahakamani kutaka kulipwa stahiki zake.

Tayari kuna zaidi ya hukumu 10 zilizotolewa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa zinazoagiza serikali kumlipa mfanyabiashara Valambia aliyekuwa akidai Sh. 56 bilioni.

Uamuzi wa kwanza wa mahakama, katika kesi ya madai Na. 210 ambapo serikali ilishindwa kesi, ulitolewa na mahakama kuu mwaka 1989.

Tangu hapo, na siku zote ilipotamkiwa na mahakama kuwa imeshindwa na inastahili kulipa, serikali imekataa kumlipa Valambia.

Aidha, serikali imegoma kuwalipa, tokea mwaka 1986, wananchi wa kijiji cha Kitondoloni, wilayani Kisarawe mkoani Pwani, waliohamishwa kutoka makazi yao ili kupisha kilichoitwa “shughuli za jeshi.”

Kupitia waziri wa fedha wa wakati huo, Profesa Kighoma Malima, serikali ilikubali kulipa stahiki za wanakijiji hao, lakini hadi leo haijatekeleza ahadi yake.

Serikali imekataa pia kuwalipa Ally Mwang’omba na wenzake 143 katika kesi Na. 144 ya mwaka 1996. Hiyo ni baada ya kushindwa kesi kama ilivyoonyesha hukumu ya Jaji Hamisi Msumi ya 18 Novemba 1996, ikiwapa wanakijiji hao haki ya kupata fidia.

Nyaraka zilizopatikana jijini Dar es Salaam wiki hii, zinaonyesha serikali imeidhinisha malipo ya dhamana kupitia benki ya Ujerumani – Deutsche Bank AG, yenye tawi lake jijini London.

Inaelezwa katika mkabata wa dhamana Na. 840BG1200371, kuwa “malipo husika yatafanywa kulingana na masharti yaliyokubaliwa na kubainishwa katika dhamana.”

Nyaraka za makubaliano zinasema, “Tanesco, shirika lililoanzishwa kwa sheria za Tanzania, limeomba mdhamani na mdhamani amekubali kudhamini malipo hayo.”

Ni mwaka mmoja sasa tangu MwanaHALISI ifichue “mpango wa siri” wa viongozi waandamizi ndani ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuilipa Dowans kinyemela.

Hati ya dhamana hiyo imesainiwa na Jim McSweeney na Simon Smith, waliotambuliwa kuwa wanatoka Deutsche Bank AG, Tawi la London.

Utata wa uhalali wa Dowans Holding SA, ulianikwa na ofisa katika ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali ya nchi hiyo.

Bernal Zamora Arce ndiye mwanasheria mkuu wa serikali ya Costa Rica. Mwaka 2008, alieleza katika barua yake kwa bunge la Tanzania kuwa, hana kampuni iliyoandikishwa kwa jina la Dowans.

Aliongeza kuwa hata kama ingekuwepo, haina anwani kwa maana ya ofisi, simu, sanduku la barua; wala chombo cha kusafiria – gari, pikipiki au baiskeli.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: