Utawala wa vitisho, risasi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 09 November 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

NILIPOKUWA Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Oljoro, mkoani Arusha, afande mmoja alizoea kukejeli makuruta wa kiume waliosomea masomo ya sanaa.

Utasikia, “Hapa wangapi wamesomea typing? Nyosha mikono!” Walionyoosha walijipalia makaa, afande yule alikuwa akianza kwa kicheko.

“Hivi wewe baba zima na ndevu zako unaweza kujisifu umetoka kazini wakati kazi yako ni kutumwa kuchapa barua tu? Hata mwanamke yule anakushinda? Ndiyo, yule ni engineering (engineer),” alikejeli.

Mwishoni akiwataka wote kujiunga na Jeshi la Wananchi au Polisi, akisema, “Join army where we kill and confuse”. Hapo ataeleza kwa kirefu kuanzia siku ya kwanza alipopewa taarifa ya kwenda vitani Uganda.

Ataeleza alivyojificha kwenye migomba Bukoba ili asiwe katika ‘bogi’ la kwanza; alivyoibuka; alivyopokewa kwa ‘meshmesh’ na alivyosonga mbele hadi akarudi salama. Lakini ataeleza walivyofurahia kuua adui na kuwaacha wengine wamechanganyikiwa kwa mizinga.

“Kazi ya kuua adui imeisha, sasa nitaua kuruta yeyote mzembe,” alitisha. “Baba zima eti kwararakwarararaa,” aliigiza mlio wa taipureta wakati wa kusogeza karatasi. Kwa mkwara ule, baadhi walijiunga na JW na Polisi.

Tangu wakati ule, Tanzania haijapigana vita yoyote na nchi jirani isipokuwa wanajeshi kushiriki shughuli za kulinda amani maeneo mbalimbali duniani. Huko ndiko wanaua na kuchanganya akili wengine.

Nazikumbuka tambo za afande yule ninapotazama Jeshi la Polisi linapotisha na kuua raia huku chama tawala CCM kikifurahia.

Mifano michache: Mwaka 1998, polisi waliopaswa kulinda raia ndio waliua Waislamu msikitini Mwembechai.

Januari 26-27 mwaka 2001 Polisi walilenga shabaha na kuua wafuasi wa CUF walioandamana kwa amani Unguja na Pemba.

Polisi wakijua kwamba uwezo wa mahabusu ya wilaya ya Mbarali ulikuwa kuchukua watu 10, waliwajaza 40. Kufika asubuhi, 17 walikufa kwa kukosa hewa.

Mwaka 2005, IGP Omari Mahita alikusanya mapanga mitaani akadai yameingizwa na CUF waliojiandaa kwa vurugu. IGP alitaka CUF walianzishe halafu atume vijana wake waue wananchi.

Januari 2006 polisi waliwateka wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja Sinza na kuwapeleka msitu wa Pande, Mbezi, walikowaua kwa risasi. Mahakama Kuu ikawaachia polisi waliohusika.

Januari 2011 polisi walichinja kwa risasi wafuasi wawili wa CHADEMA na mpitanjia Mkenya mjini Arusha kwa madai waliandamana bila kibali.

Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama akawatafutia polisi kazi ya kuua wapinzani katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga. Kwanza alidai CHADEMA wameingiza mungiki kutoka Kenya, kisha akadai wameingiza makomandoo waliopata mafunzo Libya, Afghanistan na Palestina.

Mwezi huu, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akadai amepigiwa simu na al Shabaab kwamba watashambulia maandamano ya wanaopinga serikali kuilipa Dowans.

Arusha akaibuka OCD Zuberi Mwombeji na kujipa kazi ya kuzuia Baraka za Mungu kumfikia Mbunge Godbless Lema. OCD anadai kitendo cha Lema kutembea kwa miguu na wafuasi wake kutoka mahakamani hadi ofisini kwake ni maandamano.

Kama kutembea kwa miguu ni kosa, vipi wanaotembea kwa ajili ya kuupokea na kuutembeza Mwenge wa Uhuru? Hawa si wanafanya kosa kila siku? Naona CCM wanaamini udhalimu huu hautawarudia. Tusubiri.

0
No votes yet