Uteuzi wa majaji unazingatia nini?


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 12 June 2008

Printer-friendly version
Jaji Mkuu,  Augustino Ramadhani

HIVI karibuni Rais Jakaya Kikwete ameteua majaji wapya 11, wakiwemo wanawake saba, wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Msajili wa Mahakama ya Rufani kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu, Phillemon Luhanjo.

Uteuzi huo kwa kumbukumbu yangu ni wa tatu tangu Rais Kikwete aingie madarakani. Alianza kuteua majaji 20 mwaka juzi, idadi iliyovunja rekodi. Baadae mwaka jana aliteua majaji watano wa Mahakama ya Rufani.

Rais ametumia pia uwezo wake wa kikatiba kumteua Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi, Augustino Ramadhani na Salum Massati baada ya kustaafu Barnabas Samatta na Amir Manento.

Uteuzi wa majaji wapya katika Serikali ya Awamu ya Nne, umekuwa na mtazamo wa mchanganyiko wa uzoefu katika masuala ya sheria kwani haukuangalia wale tu waliobobea katika masuala ya mahakama kama ilivyozoeleka mara nyingi.

Majaji walioteuliwa ni wanasheria wazoefu waliokwishafanya kazi kama mahakimu, wasajili wa mahakama, mawakili, waendesha mashtaka, walimu wa sheria kwenye vyuo vikuu na watetezi wa masuala ya haki za binadamu.

Wengine wamefanya kazi ya uanasheria katika taasisi kama Bunge, Baraza la Mawaziri, Wizara za Serikali, Tume ya Haki za Binadamu na kadhalika.

Mchanganyiko huo wa uzoefu unaifanya Mahakama kuwa na majaji wenye mitazamo mbalimbali ya kiuzoefu katika kutenda haki kwani baadhi yao wana taaluma za ziada kama za usuluhishi, uchumi na biashara, zilizo muhimu katika kutatua migogoro.

Ongezeko la majaji wanawake nalo limekuwa ni mtazamo mwingine wa Serikali ya sasa kwani kwa mfano, katika Mahakama Kuu kuna majaji zaidi ya 20 wanawake wakiwemo hao saba walioteuliwa hivi karibuni kati ya majaji 57 wa mahakama hiyo.

Nayo Mahakama ya Rufani ina majaji watatu wanawake kati ya majaji 15 waliopo.

Lakini kwa mtazamo wangu, naona mhimili huu nyeti na muhimu wa dola unaimarishwa bila ya kuangalia kwamba majaji wanapaswa kutoka katika jamii yote ya nchi kijiografia na siyo eneo au maeneo fulani tu.

Wakati tunajitawala na hata katika miaka ya 1970, ilikuwa ni vigumu kupata wanasheria kutoka maeneo mengine ya nchi, yaani kanda au mikoa yote. Hii ni kwa vile wasomi wengi walikuwa kutoka maeneo machache kutokana na sababu za kihistoria, kiuchumi na hata kisiasa.

Kwa sasa dhana hii haina nguvu. Kila eneo nchini lina wasomi wa taaluma mbalimbali wakiwemo wanasheria wa kiwango cha kuwa mawakili, mahakimu na majaji wazuri. Kwa hivyo, kuna fursa nzuri ya kuteua majaji kutoka kila jamii na mahali popote nchini.

Suala si tu kuwa na wanawake wengi, au kushirikisha pia makundi maalum kama ya walemavu, ila ni vizuri pia kuhakikisha tusiwe na majaji ambao theluthi moja au zaidi ya asilimia arobaini wanatoka sehemu moja tu ya nchi.

Hii itatuletea migongano ya kimaslahi katika kutenda haki hata kama majaji hao ni waadilifu na wenye upeo mkubwa kiasi gani kitaaluma.

Nimekuwa mara nyingi najiuliza hivi kuna sababu yoyote kwa sasa tena katika karne hii ya wasomi wengi nchini kutoka sehemu mbalimbali ya nchi kuwa na majaji 20 kati ya majaji 57 wa Mahakama Kuu kutoka sehemu moja tu ya nchi?

Au kuna mantiki yoyote ya kuwa na majaji watano kati ya 15 wa Mahakama ya Rufani kutoka sehemu moja tu ya nchi?

Theluthi moja ya majaji wa Mahakama ya Rufani wanazungumza lugha moja ya mama ikiwemo pia utamaduni mmoja. Hii naona ni hatari.

Nionavyo, hali hii imeanza kujitokeza pia katika mahakama za chini ingawa huko kuwapata mahakimu kunategemea tu vigezo vya elimu katika kuomba kazi ya uhakimu na siyo uteuzi kama ilivyo kwa majaji.

Hatari ninayoiona ni kwa mfano pale mashauri mengi yanayoendeshwa kwa msaada wa mawakili yanavyoleta picha isiyo nzuri. Si ajabu siku hizi kukuta kuna kesi mbele ya jaji ambaye ni kutoka sehemu moja na wakili wa upande wa utetezi na pia mteja mwenyewe anayetetewa.

Hutokea pia upande wa mashtaka ukawa una mwendesha mashtaka anayezungumza lugha moja ya mama na jaji na pengine hata mashahidi. Halafu hakuna anayegundua hali hiyo kati yao ili aweze kujiondoa au kuomba kubadilishwa.

Kuna tetesi kwamba hata ile kesi ya Padre aliyeachiwa huru kwa kutokuwa na hatia ya kulawiti kijana, alipokata rufani Mahakama Kuu ilitokana na hali hiyo ya mgongano wa kimaslahi.

Kwani si tu Jaji, Wakili na Mtuhumiwa walikuwa wanatoka sehemu moja ya nchi, ila wamekua, kulelewa na kusoma pamoja.

Hata hivyo tunahitaji kuwa na majaji wenye tamaduni zote za nchi kutokana na makuzi yao. Tukihitaji jaji mwenye makuzi na utamaduni wa maeneo ya pwani apatikane; tukitaka jaji wa maeneo ya utamaduni wa Wandengereko au Wamakonde au Wamakua au Wayao naye awepo.

Hata tukitaka jaji wa maeneo ya Wagogo apatikane. Tukitaka jaji wa maeneo ya Waha wa Kigoma au wa Chakechake, Pemba naye awepo. Tukitaka jaji mwenye asili ya Sumbawanga na Mpanda apatikane kwa kuwa wapo wanasheria wengi tu kutoka huko.

Hebu tufanye kama madhehebu ya dini yanavyojitahidi kupata viongozi wa makanisa, misikiti na mahekalu (mfano: katika majimbo, usharika, mitaa au parokia) kutoka kila eneo la nchi.

Tukumbuke Mahakama ndio mhimili mkuu katika dola wenye jukumu au mamlaka pekee ya kutoa haki kwa mujibu wa Ibara ya 107A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 inayosema: "Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama."

0
No votes yet