Uteuzi wa Rais Kikwete umejaa utata


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 09 June 2009

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

UAMUZI wa Rais Jakaya Kikwete, kumteua Peter Ephraim Mayunga Noni, kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), umepokelewa kwa maoni tofauti.

Hii ni kwa kuwa Noni ametajwa katika maandishi na kauli mbalimbali kwamba, akiwa mtumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) alifanikisha au alinyamazia ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kutoka akaunti ya madeni ya nje (EPA).

Kabla ya uteuzi huo, Noni alikuwa Mkurugenzi wa Mipango Mkakati na Utendaji ndani ya BoT. Anajaza nafasi ya William Mlaki ambaye amestaafu utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria. Uteuzi wake ulianza 27 Mei 2009.

Kabla ya kuwa Mkurugenzi wa Mipango Mkakati na Utendajindani ya BOT, Noni alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Fedha za Nje ndani ya benki hiyo.

Uteuzi wa Noni unakuja baada ya kutajwa na Imani Mwakyosa, mmoja wa washitakiwa katika kesi za EPA zilizoko mahakamani kwamba ndiye alikuwa akiridhi baadhi ya malipo.

Hata wakili wa Mahakama Kuu, Bydinka Sanze, katika hati yake ya kiapo anasema kwamba Noni alikuwa katika kikao klichohudhuriwa na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Ni katika kikao hicho, Sanze anasema Rostam alimtaka ashuhudie mikataba iliyotumiwa na kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, kuchota fedha za EPA.

Uteuzi wa Noni, anayesemwa kuwa karibu na Rostam Aziz, kuongoza taasisi ambayo Rais Kikwete alisema ndiko zitapelekwa fedha za EPA zinazorudishwa na watu binafsi na makampuni yaliyokuwa yamezipora, kunajenga hoja yenye utata.

Uteuzi wa Noni basi unaweza kuwa unalenga kudhibiti taarifa zozote zile juu ya fedha za EPA zitakazopelekwa BIT au ambazo hazitapelekwa kutokana na sababu mbalimbali.

Kikwete anajua vema kwamba kuweka mkuu TIB, ambaye ataanika ukweli na uwongo kuhusu fedha za EPA, hakutasaidia utawala wake kujinyofoa kwenye utata na kashfa zinazoambatana na wizi huo.

Kwa kuwa Noni ametajwa kuwa katika kikao ambamo wakili anasema aliitwa na Rostam Aziz; na kikao hicho kuhusishwa pia na rais mstaafu Benjamin Mkapa na Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Philip Mangula, basi Noni aweza kuwa chaguo bora la kuziba taarifa zisitoke.

Rais ana haki ya kuteua mtu yeyote kushika nafasi yoyote anayoona anaiweza; lakini wananchi au hata watazamaji wa wafuatiliaji wa siasa za nchi, wana macho na masikio juu ya yanayotendeka.

Kwa hiyo, uteuzi aliofanya Kikwete, wa mtu ambaye yuko karibu na matukio makuu yaliyohusisha wizi BoT, unaweza kutafsiriwa kwa njia nyingi, hata kama tafsiri hizo hazitafanya uteuzi huo kubatilishwa.

Moja ya majukumu ya Noni pale TIB ni kulinda na kuwezesha matumizi bora ya mabilioni ya shilingi za serikali ambazo zimewekwa kwa ajili ya kuendeleza wafanyabiashara na wakulima.

Wachunguzi wa masuala ya utawala wanaweza kuuliza iwapo hali iliyojitokeza BoT inaweza kujirudia TIB wakati Noni akitazama tu. Na hilo likitokea, Kikwete ataendelea kufumba macho?

Hii yaweza kuwa bahati mbaya kwa Kikwete. Ni kama alivyomteua Yusuph Makamba kuwa Katibu Mkuu wa CCM huku akijua ni Makamba aliyeasi utaratibu wa CCM wa kupitisha mgombea wa ubunge, baada ya kumtangaza Yusuf Manji kuwa “mbunge wa Kigamboni.”

Ni Kikwete aliyemteua Basil Mramba kuwa Waziri wa Miundombinu, huku akijua kuwa anakabiliwa na lundo la tuhuma.

Kikwete alijua Mramba alikuwa anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka; upendeleo kwa kampuni ya Alex Stewart na kauli mbaya kwamba ndege ya rais itanunuliwa, kwa vyovyote vile, hata kama wananchi “wanakula nyasi.”

Katika mlolongo huohuo, Kikwete aliendelea kumteua Andrew Chenge kuwa waziri wa miundombinu huku akijua kuwa Chenge alikuwa tayari anatuhumiwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada.

Vivyo hivyo kwa aliyekuwa Gavana wa BoT, Dk. Idris Rashid. Ni Kikwete aliyemteua kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) huku akijua fika kuwa tayari amehusishwa katika ununuzi tata wa rada.

Orodha ni ndefu. Kuna Francis Isaack Mtinga, sasa mkuu wa wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara. Hata kabla ya kuidhinishwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), tayari alituhumiwa kuwa na mali zisizolingana na mapato yake.

Wakati imefahamika kuwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ilikuwa inamchunguza, Kikwete alimuopoa Isaack na kumfanya mkuu wa wilaya.

Aidha, Isaack alituhumiwa na vijana wenzake ndani ya UV-CCM kushirikiana na mwekezaji kutoka kampuni ya M.M. Integrated Steel Mills Limited (MMISML) na Estim Construction Company Limited (ECCL) zilizoingia mkataba na jumuiya hiyo ambao ulishupaliwa na mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Edward Lowassa.
 
Hata pale wajumbe karibu wote wa baraza la wadhamini walipoamua kuanika ukweli na hatimaye kumkana mwenyekiti Lowassa, bado Isaack alitetea uamuzi wa Lowassa wa kusaini mkataba huo.

Haifahamiki kama haya yanafanyika kutokana na udhaifu wa vyombo vya usalama vya taifa au Kikwete mwenyewe hafuati ushauri wa wataalamu wake.

Haitashangaza kusikia siku moja Kikwete akimteua mmoja wa watuhumiwa wakuu wa ufisadi kuwa waziri wa nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora. Tusubiri.

0
No votes yet