Uteuzi wa Rais: Wafanyakazi wanaumia


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 05 May 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

LIKITOKEA pengo la kiongozi wa kisiasa serikalini linajazwa mara moja. Likitokea pengo la mwanataaluma linalohusu wafanyakazi, litaachwa wazi kwa muda mrefu.

Hiyo ndiyo staili ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Anapenda kujaza nafasi za siasa na siyo nafasi za uongozi zenye manufaa kwa wafanyakazi.

Matokeo yake ni kwamba wafanyakazi walio katika mashirika ya umma, ambako rais amechelewesha uteuzi wa viongozi, maslahi ya wafanyakazi yametupwa kapuni.

Hiki ndicho kiini cha manung’uniko, malalamiko na hata mipango ya kufanya maandamano na hata migomo kukumbusha rais wajibu wake.

Ushahidi ni mpevu. Umo katika mashirika zaidi ya 15 ambako rais hajachukua hatua kuteua wale ambao wangeshughulikia matatizo ya wafanyakazi.
Kuanzia Shirika la nyumba Tanzania (NHC), Shirika la Ndege la Taifa (ATCL), Shirika la Bima la Taifa (NIC), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA), Shirika la Magazeti la Serikali (TSN), Shirika la Umeme Taifa (TANESCO) na pengine pengi, kunaendeshwa na watu wanaokaimu.

Nafasi ya mkurugenzi mkuu wa NIC ilitangazwa Machi 2009, lakini uteuzi umefanyika mwaka mmoja baada ya nafasi kutagazwa.

Ni ucheleweshaji huo uliomuibua Nehemiah Mchechu kutoka meneja mkuu wa benki ndogo ya Commercial Bank of Africa (CBA), isiyokuwa na matawi yoyote mikoani, na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba (NHC).

Tayari manung’uniko yameibuka kwamba Mchechu si mhandisi kama tangazo la kazi la serikali lilivyotaka na hakuwa miongoni mwa waombaji.

Malalamiko mengine yanadai kuwa Mcheshu “ameumbwa” na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo – ndani ya ikulu.

Kiongozi wa shirika aliyecheleweshwa, aliyepatikana kwa njia inayodaiwa kutokuwa sahihi, aweza kuwa na fikra haba juu ya wafanyakazi na maslahi yao.

Hali ndivyo ilivyo ATCL. Kikwete hakuteua mtendaji mwenye sifa kuongoza shirika hilo.

Mtendaji Mkuu David Mattaka ni mtaalam wa biashara za bima. Hana utaalam wa uendeshaji mashirika ya ndege.

Kabla ya kukabidhiwa ATCL, Mattaka alikuwa mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa Pesheni Tanzania (PPF).

Huko ndiko alikotemwa na rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, kwa kile kinachodaiwa, “tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka” katika ujenzi wa nyumba za shirika.

Ukuu wake ATCL na hata PPF alikokuwa mwanzo, licha ya kuvunja moyo wafanyakazi, hauwezi kuzingatia maslahi ya wafanyakazi bali waliomteua.

Katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu cha 9 Aprili mwaka huu, kilichofanyika Dar es Salaam, Waziri wa Miundombinu, Shukuru Kawambwa alisema serikali haina imani na uongozi ATCL.

Kama serikali inaweza kukiri hilo, wakuu hao wa ATCL watasikilizaje maslahi ya wafanyakazi ambao hawawajibiki kwao?

Tayari ATCL inatuhumiwa kutumia fedha kinyume cha taratibu zilizowekwa na serikali katika kununua ndege mpya za kampuni hiyo. Fedha hizo zilitumika kununulia magari ya wakurugenzi.

Aidha, muda wa miaka mitatu wa bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo umeisha. Katika hali hii nani awezaye kujali wafayakazi?

Matokeo yake, kazi zimesimama, ufanisi umepungua, wafanyakazi hawajalipwa mafao yao na minong’ono na tuhuma vimepamba moto.

Huko TPC hakuna mtendaji mkuu. Deo Mndeme amekuwa akikaimu nafasi hiyo kwa zaidi ya mwaka sasa.

PTC inakabiliwa na ushindani mkubwa kibiashara, lakini mipango yake mingi imekwama kwa Kikwete kushindwa kuteua mtendaji mwenye mdaraka kamili ya kuongoza shirika.

Ndani ya NIC hakuko salama. Kikwete amerudisha watu walewale wanaokabiliwa na tuhuma lukuki za kuhujumu NIC kuongoza shirika.

Kaimu Mkurugenzi mkuu, Justine Mwandu, aliwahi kuwa mkurugenzi wa bodi katika kampuni ya Bima ya Tudor Insurance Corpotion Ltd., ambayo imefilisika.

Agnes Bukuku aliyewahi kuwa msajili wa hazina mwenye mamlaka ya kulinda mali za serikali na mjumbe wa Bodi ya NIC, ameteuliwa kuwa katibu wa kikosi kazi.

Katika kipindi cha menejementi ya kukodi ya Margret Ikongo, ambapo tuhuma za ubadhilifu, wizi, ufujaji wa mali ya umma na matumuzi mabaya ya madaraka zilishamiri, Bukuku alituhumiwa na wafanyakazi kulinda Ikongo na menejementi yake.

Leo hii ambapo kimeudwa Kikosi Kazi “kuinusuru” NIC, tayari kimetumia Sh. 500 milioni kutoka serikalini na kuongezewa muda tangu Machi kilipomaliza muda wake bila tija, hadi Oktoba mwaka huu.

Nako Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), hakuko salama. Serikali iliyokuwa na asilimia 51 ya hisa imeshindwa kuteua mwenyekiti wa bodi.

Kushindwa huko kwa serikali, kumefanya mbia kuendesha benki bila kuwapo kwa bodi ya wakurugenzi.

Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA) hali ni hiyohiyo. Mwantumu Malale bado anaendelea kukaimu nafasi ya mwenyekiti wa bodi.

Kuendelea kukaimu uongozi wa bodi ndiko kunakotajwa na wafanyakazi kupunguza ari ya kazi.

Inadaiwa hicho ndicho chanzo cha madai ya kushindwa kwa TCAA kuweka hata kiyoyozi katika chumba cha kupokelea mizigo katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mbali ya hilo, ni mashine moja tu – kati ya mbili – ya kusukumia mizigo ambayo inafanya kazi.

Shirika la Magazeti la Serikali (TSN) linalochapisha magazeti ya Daily News, Sundey News na Habari Leo, nalo halina mtendaji mkuu.

Isaac Mruma ambaye aliteuliwa na Kikwete kuongoza TSN miaka minne iliyopita, ameondolewa katika nafasi yake katika mazingira ya kutatanisha. Hivi sasa, nafasi ya Mruma inakaimiwa na Mkumbwa Alli.

Hata hivyo, bado Mruma anaendelea kupokea mshahara wa shirika na anaendelea kuishi katika nyumba ya serikali.

Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi, Wilson Mukama ameteuliwa kuongoza shirika hilo mwaka mmoja baada Adolar Mapunda kumaliza muda wake.

Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO), halina mtendaji mkuu. Ni baada ya Dk. Idris Rashidi kumaliza muda wake.

Dk. Rashidi ni miongoni mwa watuhumiwa wa rushwa ya rada na ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT).

Tangu Dk. Rashid amalize mkataba wake Novemba mwaka jana, pamoja na kuwa mchakato wa kutafuta mtendaji mpya umekamilika, Kikwete hajateua mtendaji mpya.

Naye, Balozi Fulgence Kazaura alipomaliza muda wake kama mwenyekiti wa Bodi, rais alichukua mwaka mmoja kuteua Peter Ngumbullu kushika nafasi hiyo.

Ingekuwa vyema iwapo kimya hicho kirefu kingekuja na tija. Sivyo ilivyo. Ngumbullu anakabiliwa na matatizo ya afya.

Rais anajua kuwa kiongozi anayekaimu hana madaraka kamili ya kufanya maamuzi. Anajua kuwa maamuzi mengi yanahitaji fedha, mtaji, rasilimali na mafunzo. Haya hayawezi kufanywa na “watendaji kibogoyo.”

Jingine linalokwaza wafanyakazi ni taasisi ya rais kunyamazia mapendekezo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) yanayotaka wabunge kutokuwa wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi katika mashirika ya umma.

Ni rais ambaye anaendelea kuwateua watendaji wa wizara kuwa wenyeviti wa bodi katika mashirika yaliyo chini ya wizara zao.

Mfano hai ni mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF).

Mapungufu mengine ni kama uteuzi wa Adolar Mapunda, mtaalamu wa mawasiliano, kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Muhimbili (MUCHS).

Hapa kuna nafasi finyu ya kufikiria mfanyakazi, kwani hata mazingira ya kazi yenyewe ni mapya kwa mteule.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: