Uvamizi: Gaddafi alijiandaa miaka 42 kabla


Zakaria Malangalila's picture

Na Zakaria Malangalila - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Kanali Muammar Gaddafi

UMOJA wa kujihami wa nchi za Ulaya (NATO) sasa umekiri kushindwa kumuondoa madarakani, Kanali Muammar Gaddafi wa Libya.

Ni baada ya takriban miezi mitatu ya tangu kuivamia nchi hiyo. Hata hivyo, makamanda wa vikosi vya NATO, wanasema bado wanamatumaini ya kumondoa Gaddafi.

Lakini hadi leo hii ushindi (kwa maana ya kutotimia azima ya NATO) uko upande wa Gaddafi huku nchi za umoja huo zikionekana kugombana zenyewe kwa wenyewe.

Habari kutoka Istanbul, Uturuki kuhusu maazimio ya mkutano wa nchi za NATO kuhusu suala la Libya zinatoa picha ya kushangaza.

Taarifa zinasema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton na wa Uingereza, William Hague wametaka azima ya kuubadilisha utawala wa Libya ibaki palepale kwa kuongeza mawasiliano na misaada kwa Kamati ya Waasi wa Benghazi.

Lakini wakati kauli hizo zinatolewa, aibu itokanayo na harakati za NATO kwa Libya zinaonekana kuingia katika vitabu vya historia kama tangazo la madhara makubwa ya kisiasa kwa kisingizio cha kile kinachoitwa “uingiliaji kati kwa sababu za kibinadamu.”

Haya yote yanasababishwa na kutokuwapo kwa umakini katika suala la kiintelijensia, ikiwamo hisia potofu kuhusu udondoshaji wa mabomu na uwezo wa kumiliki anga.

Kwa mfano, hakuna dokezo la kiintelijensia lililosema kwamba kuna uhasama mkubwa wa kihistoria kati ya watu wa Benghazi (ngome ya waasi) na wale wa Tripoli – makao makuu ya serikali ya Gaddafi? Hili walilitia maanani?

Aidha, nchi za NATO hazikutia maanani ukweli mwingine, kwamba idadi ya Walibya wote ni takriban milioni sita tu na Tripoli pekee ina watu milioni nne?

Vyombo vya habari vya magharibi, pamoja na Al-Jazeera havikusaidia katika hili?

Havikueleza kwa mfano, habari za awali kwamba Gaddafi aliamrisha “mauaji ya kimbari” dhidi ya watu wake, au kuamrisha vitendo ubakaji, zilitokana na habari zisizothibitishwa zilizokuwa zikitangazwa na vyombo vya parapaganda vya waasis wa Benghazi.

Hivi sasa, habari hizo zimekanushwa vikali na mashirika ya haki za binadamu yanayoheshimika duniani, kama vile Amnesty International na Human Rights Watch.

Isitoshe, hatua ya Mahakama ya Kimataifa ya The Hague (ICC) ya kutoa hati ya kukamatwa kwa Gaddafi na baadhi ya wasaidizi wake inaonekana dhahiri ni ya upendeleo kwa sababu ICC ni chombo cha NATO na kwa muda mrefu kimekuwa kinafuatilia kwa karibu agenda zake.

Ni tofauti na Amnesty International na Human Rights Watch ambayo yanaonekana kuwa huru.

Kwa hivyo kutokana na hatua ya mahakama ya ICC na propaganda za vyombo vya habari vya magharibi, nchi hizo zinajilazimisha kukumbatia dhana potofu kwamba zinapigana vita halali dhidi ya Gaddafi, ambaye ni adui wao mkubwa kwa miaka 42 sasa.

Suala lingine linaloonyesha uonezi wa NATO katika harakati zake dhidi ya Libya ni kauli kali za nchi za Umoja wa Afrika (AU), Russia na hata Ujerumani (ambayo imo katika umoja huo wa NATO) zikilaani ukiukwaji wa maazimio mawili ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa – lile la Februari na Machi mwaka huu ambayo kimsingi yalisisitiza azma tu ya kulindwa maisha ya raia wa Libya.

Maazimio hayo hayakutaja mahali popote mpango wa kubadilisha utawala wa Libya kwa kumuua Gaddafi. Baraza la Usalama lilikataza nchi yoyote ya nje kupeleka askari wa ardhini Libya.

Bila shaka umoja wa mataifa wasingelikataza hili, basi huenda yale yaliyoikuta Iraq mwaka 2003 yangemkuta Gaddafi.

Wachunguzi wa mambo wanasema hatua ya kuushambulia kwa mabomu mji wa Tripoli imelenga kuyapa kazi makampuni makubwa ya nchi za Ulaya pindi waasi wa Benghazi watakaposhika nchi ili kuinia uchumi wa nchi hizo ambao sasa unalegalega kutokana na migogoro ya kifedha na madeni.

Kwa mfano, hivi sasa nchi kama Italia imo mbioni kuanguka kifedha na mazungumzo ya kuomba misaada ya fedha kutoka Benki Kuu ya EU yanafanyika.

Kama ilivyokuwa Ugiriki, Ireland ya Kaskazini na Ureno, Italia ni nchi iliyomstari wa mbele katika kupeleka vikosi vya anga mjini Tripoli.

Machi mwaka huu, Rais Sarkozy wa Ufaransa alichangamkia ripoti ya swahiba wake, Bernard Henri Levy, aliyetembelea Benghazi (Machi 6) kwamba Libya na akiba yake kubwa ya mafuta inaweza kuwa halali ya nchi za magharibi.

Ripoti hiyo pia ilisema mabomu machahche yatakayoangushwa mjini Tripoli yangesababisha maelfu ya askari wa Gaddafi kumsaliti kiongozi wao.

Sarkozy alichukuwa hatua ya haraka ya kukitambua kikundi cha waasi cha Benghazi kama ndiyo utawala halali wa Libya. Wachunguzi wa masuala ya siasa nchini Ufaransa wanasema yote hii ilitokana na kura mbaya za maoni za Sarkozy kuhusu uchaguzi wa urais mwaka ujao.

Ofisa mmoja wa ngazi ya juu wa serikali ya Sarkozy alimdokezea Vincent Jauvert, mhariri mkuu wa Le Nouvel Observateur, gazeti maarufu nchini Ufaransa kwamba nchi za NATO zilikuwa zimechukulia Gaddafi kiurahisi mno.

Alisema, “Inavyoonekana kwa miaka 42 Gaddafi alikuwa katika matayarisho na uvamizi huu. Nchi za NATO hazikutilia maanani hilo. Hazikufikiria kwa mfano, Gaddafi angekuwa na uwezo wa kununua mamia ya magari ya aina ya Toyota Pickup kutoka nchi za jirani za Mali na Niger ambayo yalibebebeshwa vifaa vya kurushia makombora.”

Baada ya kuona anguko la Gaddafi halitokei, serikali ya Ufaransa imeanza kudondosha silaha kwa waasi wa Benghazi – kinyume na azimio ya baraza la usalama. Bila shaka Uingereza nayo inafanya hivyo.

Ukweli ni kwamba hivi sasa mshikamano katika NATO umeanza kusambaratika. Ujerumani inaanza kutengana na wengine, huku Italia, kutokana na matatizo yake ya kiuchumi na kisiasa pia nayo yaonekana imo imo tu.

Tayari Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Gerard Longuet amenukuliwa akisema, “harakati za kijeshi dhidi ya Libya zinaonekana kushindwa.”

Anashauri ni bora kuwepo mazungumzo. Anasema, “NATO itasitisha mashambulizi mara wananchi wa Walibya watakapoanza mazungumzo.

Kauli ya Ufaransa inaendana na wito wa Gaddafi wa kutaka kuwapo kwa mazungumzo, ingawa waasi walikuwa wakikataa na kumtaka aachie madaraka kwanza. Ni kwa sababu walipewa kibuli na NATO.

Baadhi ya wanasiasa na wachunguzi wa mambo wa nchi zinazopakana na Bahari ya Mediterranean wanahofu kubwa kuwa huenda Libya ikageuka Somalia ya eneo hilo; maharamia wa baharini wanaweza kuzuka mlangoni mwa nchi za Ulaya.

zakmalang@yahoo.com
0
No votes yet