Uvamizi wa kiwanja wahusishwa na Ikulu


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 07 October 2008

Printer-friendly version
Wavamiaji: Hii ni "dili ya ikulu"
Wakala Majengo ya Serikali kimya

UVAMIZI wa eneo la maghorofa ya serikali waliyouziwa wafanyakazi, yajulikanayo kama SIDA Flats, jijini Dar es Salaam, unadaiwa kupata baraka za ikulu, MwanaHALISI limeelezwa.

Ofisa mmoja wa Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA), aliyetaka jina lake lihifadhiwe, ameliambia gazeti hili kuwa uvamizi huo, “una baraka za wakubwa serikalini hadi za ikulu.”

Vuta nikuvute ya tangu Julai 2005 kati ya wafanyakazi wamiliki wa maghorofa hayo na TBA, sasa imeingia hatua mpya baada ya kiwanja chao kuanza kumegwa kwa uzio wa mabati kwa maandalizi ya ujenzi.

SIDA Flats ni maghorofa sita yaliyojengwa na Shirika la Mendeleo la Sweden chini ya kilichoitwa Mradi wa Ujenzi wa Sweden (Swedish Project Housing Estate) na kukabidhiwa kwa serikali.

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati alipoulizwa juu ya suala hili hajalielewa vizuri, “naomba muda zaidi ili niweze kulielewa.”

Katika maghorofa hayo, yaliyoko Kinondoni, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, wamekuwa wakikaa wafanyakazi wa ngazi za kati na chini wa serikali hadi yalipouzwa kwa wakazi wake.

Kwa mujibu wa ramani ya Idara ya Upimaji na Ramani, maghorofa yamo ndani ya Kiwanja Na. 93 kilichomo kwenye mpango Na. 34750 uliothibitishwa na Mkadiriaji Ardhi wa Jiji tarehe 13 Aprili 2002 na kupewa ithibati tarehe 29 Aprili mwaka huohuo.

Ndani ya kiwanja hiki pia kuna nyumba mbili zinazotumiwa na Umoja wa Mataifa (UN); moja ikiwa Zahanati ya wafanyakazi wa umoja huo na nyingine kama makazi na ofisi ya Idara ya Usafiri.

Eneo linalovamiwa, ndani ya kiwanja, ni sehemu ya kiwanja iliyoachwa ili kuleta upepo mwanana, kuwa viwanja vya watoto wa maghorofani kuchezea, kuleta mandhari nzuri na kwa matumizi mbalimbali ya kijamii kwa wakazi.

Hivi sasa uzio wa bati na milinga umeanza kujengwa kutenga nyumba za UN na maghorofa bila taarifa yoyote kwa wenye Kiwanja Na. 93 katika eneo maarufu jijini la ADA Estate.

Taarifa zinasema pia kuwa eneo la kiwanja hicho, Kusini Mashariki mwa maghorofa, kuelekea nyumbani kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, John Pombe Magufuli, nalo limevamiwa.

Kinachoongeza uchungu mkubwa kwa wenye maghorofa haya ni eneo la kuegesha magari ya wakazi wa maghorofani (angalia ramani: mviringo usiokamilika), ambalo nalo imefahamika kuwa limo mbioni kumegewa mtu moja mwenye asili ya kiasia (Mwarabu).

“Tuliona vijana wanakuja na kuvunja mabanda yaliyokuwemo kwenye kiwanja chetu; wakakata migomba na kuharibu bustani ndani ya kiwanja chetu na kuanza kuweka uzio,” wameeleza wenye kiwanja.

Ni wiki ya pili sasa tangu kiwanja kivamiwe na wanaoweka uzio wanadai kuwa anayetaka kujua wanatoka wapi “aulize Mkurugenzi wa Mipango Miji.”

“Sisi tunajua waliotuleta hapa wana hati ya kiwanja, kibali cha kujenga na wameruhusiwa na ngazi zote kuanzia ikulu. Hamuwezi kutubabaisha,” ameeleza msimamizi na vibarua ambao wanaweka uzio.

Hata hivyo, wakazi wa maghorofani walioongea na mwandishi wa habari hizi wamesema wavamizi “wanataka kutumia ikulu kuhalalisha uharamia wao lakini hawatarajii Rais Jakaya Kikwete akubaliane na uhuni huu.”

Kwa mwaka wa tatu sasa, tangu Julai 2005, kumekuwa na vita vya kimyakimya kati ya wenye maghorofa hayo ambao ni wafanyakazi wa serikali na TBA.

Wakazi wa maghorofani wameunda kamati ya kufuatilia lakini nayo imeshindwa kuwapa matumaini hadi kiwanja chao kikavamiwa rasmi. Baadhi ya wafanyakazi wanalaumu mwenyekiti wa kamati yao kwa kutoonyesha ukakamvu katika vita hivi.

Jumla ya familia 36 zinaishi katika maghorofa ya Kiwanja Na. 93. Familia hizo zina idadi ya zaidi ya watu 150.

Kuhusishwa kwa ikulu kunafuatia kimya cha Katibu Mkuu-Kiongozi baada ya wakazi kumlalamikia.

Aidha, mkono wa serikali katika uvamizi unaelezwa kwa matukio kadhaa ya viongozi wa serikali – Ofisi ya Waziri Mkuu na Idara ya Upimaji na Ramani kutembelea eneo la kiwanja Na. 93 na kuhojiana na walinzi kwenye egesho la magari ambalo linasadikiwa kumegwa tayari.

Wakazi wa maghorofani na walinzi kwenye egesho wanasema wamekuwa wakiona watu wanaojitambulisha kuwa wanatoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Idara ya Upimaji na Ramani, “wakija na kupima eneo bila hata kutoa taarifa kwa uongozi wa umoja wetu.”

Lakini kubwa zaidi ni taarifa za wakazi hao kwenda kwa orodha ndefu ya ofisi za serikali, hata ikulu, bila kujibiwa wala kufuatiwa na hatua yoyote.

Ofisa mmoja wa TBA alimwonyessha mwandishi, barua ya malalamiko ya wakazi wa maghorofani (nakala tunayo) ya Julai 2005, wakati wa mchakato wa kuuziwa nyumba hizo.

Nakala ya barua hiyo ilisambazwa sehemu nyingi zikiwemo Katibu Mkuu-Kiongozi, Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu (Dar es Salaam), Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu.

Wengine ambao tayari wamefikishiwa malalamiko ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Taarifa za umoja wa wakazi wa maghorofani zinasema, pamoja na kilio hicho, hakuna hata mmoja kati ya waliopelekewa taarifa ambaye ameitika, hadi kiwanja chao kilipoanza kumegwa wiki mbili zilizopita.

Hoja kuu zinazotolewa na wakazi ni kwanza, hakuna mwendelezaji anayepaswa kupewa kiwanja ndani ya kiwanja.

Pili, hakuna mwendelezaji anayeweza kupewa hati ya kujenga wakati hana kiwanja na wakati namba ya kiwanja anapotaka kuendeleza ni ya mtu mwingine.

Tatu, hakuna mwendelezaji anayeweza kupewa kiwanja cha mtu mwingine na kuanza ujenzi hata bila kutilia maanani mambo muhimu kama mazingira, mfumo wa majisafi na majitaka na suala la haki za binadamu na utawala bora.

Katika uvamizi wa Kiwanja Na. 93, misingi yote hapo juu imekiukwa; wote walioombwa ushauri wamekaa kimya na haki za wakazi wa SIDA Flats na nyumba mbili za UN, watabanwa na mwendelezaji mbabe ambaye anasadikiwa kuungwa mkono na serikali.

Eneo la ADA Estate, kilipo Kiwanja Na. 93 ni la viwanja vikubwa viitwavyo “Low Density.” Katika viwanja hivyo zinaweza kujengwa nyumba mbili au hata tatu kubwa za hadhi.

Hoja inakuja kwamba kama wenye nyumba mojamoja wanaweza kubaki na viwanja vyao vikubwa, bila kugawa viwanja vingine ndani yake, kwa nini wa maghorofani, ambao ni wengi (familia 36) wanyang’anywe eneo lao?

Hata hivyo ofisa wa TBA aliliambia gazeti hili kuwa kazi ya wakala wake ni kujenga, kutunza na kupanga nani aishi katika nyumba za serikali. Basi.

“Hata sisi wengine tunashangaa TBA inatafuta nini katika viwanja vya nyumba ambazo tayari serikali ilikwishauza,” kimeeleza chanzo hicho cha habari.

Taarifa za ndani ya TBA zinasema iwapo wakazi wa maghorofani wataporwa sehemu ya kiwanja chao, haitakuwa mara ya kwanza kwa wakala huyo kufanya hivyo.

Wakala wa Majengo ya Serikali analalamikiwa kwa kupora eneo la kiwanja cha nyumba za serikali zilizouzwa kwa wafanyakazi zijulikanazo kama Kinondoni Flats.

Nyumba hizo ambazo pia ni maghorofa ziko karibu na Ubalozi wa Ufaransa, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam.

Mmmoja wa wakazi wa maghorofa hayo alimwonyesha mwandishi wa habari hizi, eneo la kiwanja cha maghorofa hayo ambalo lilichukuliwa na wakala wa majengo ya serikali.

Eneo hilo, ambako tayari TBA inasadikiwa kujenga nyumba ya ghorofa tatu, lilikuwa limeachwa kwa ajili ya matumizi ya wakazi wa ghorofani kama mahali pa watoto wao kuchezea, wakazi kukutana kwa shughuli mbalimbali na kuleta mandhari bora na hewa safi.

Taarifa zinasema wakazi wa Kinondoni Flats waliungana na kufungua kesi mahakamani ambako amri ya kusimamisha ujenzi ilitolewa lakini TBA na wajenzi walikaidi na kuendelea.

Inadaiwa kuwa viongozi wote waliokimbiliwa kuombwa msaada hawakutoa msaada wowote na wakazi wachache waliokuwa mbele kupigania “haki ya miliki ya kiwanja chao, walikata tamaa na kuogopa nguvu iliyoonekana kutoogopa hata  mahakama.”

Hivi sasa jengo hilo jipya katika kiwanja cha Kinondoni Flats linakodishwa kwa watu binafsi kama makazi na ofisi kwa gharama ya chini ya eneo kwa Sh. 1 milioni kwa mwezi.

Kuchukuliwa kwa sehemu ya Kiwanja Na. 93 kwa uendelezaji wa mtu mwingine nje ya wamiliki wa kiwanja kisheria, kutajenga uhasama kati ya “wamiliki.”

Umilikishaji ndani ya kiwanja chenye miliki tayari, kutaweka msingi mbaya wa mahusiano kati ya serikali na wananchi.

Aidha, umilikishaji wa aina hii umeelezwa na mwalimu wa masuala ya utawala bora kuwa “lazima utakuwa umetawaliwa na rushwa kwa ngazi ya juu na ukiukwaji mkubwa wa misingi yote ya utawala bora.”

Bali biashara ya kujenga na kukodisha nyumba, hata kama TBA ni mbia tu, haiendani na shabaha na melengo ya kuundwa kwa wakala huyo wa serikali.

Biashara ya kujenga na kuuza ni ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na siyo wakala wa serikali.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: