UVCCM bora wageuke njiwa wa Nuhu


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version
Tafakuri
Mwenyekiti wa UVCCM, Beno Malisa

MWAKA 1994, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) chini ya Mwenyekiti John Guninita, uliingia katika malumbano na chama chao. Tuseme na baadhi ya vigogo wa chama.

Mmoja alikuwa Kingunge Ngombale-Mwiru, wakati huo akiwa ndiye kinara wa itikadi na uenezi wa chama.

Malumbano hayo yalitokana na kitu kimoja tu: Vijana waliamua kuwatangaza baadhi ya wana-CCM walioamini ndio wanaofaa na kustahili kugombea urais baada ya uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi kukoma.

Waliotajwa walikuwa Edward Lowassa, Dk. Salim Ahmed Salim, Jaji Mark Bomani na Jakaya Kikwete. Vijana walijikuta katika wakati mgumu baada ya tangazo lao kuonyesha dhahiri kuunga mkono “watu wao.”

Msimamo huo ulikuwa na maana kuwa kama taasisi katika chama waliamua kupitisha wagombea wao kabla ya utaratibu rasmi.

Tatizo lililojitokeza lilikuwa UV-CCM kutumika kupitisha majina ya wagombea fulani na kujenga taswira kuwa jumuiya ndiyo imeamua.

Ilionekana kwa kuwa sasa kulikuwa na hatari ya kutokea mparaganyiko ndani ya chama na taasisi zake, basi wakubwa hawakuwa na njia isipokuwa ‘kuangamiza’ vijana wote waliokuwa viongozi wakuu makao makuu.

Baadhi waliteuliwa ukuu wa wilaya; wapo waliofungwa jela ya kisiasa kimkakati kama ilivyo ada ya CCM, “kushughulikiana.”

Kabla ya uchaguzi mwaka jana, UV-CCM waliamua kushughulikiana wenyewe safari hii wakisaidiana na wakubwa wa CCM. Hapo ndipo alipokumbwa Nape Nnauye kwa kile kilichoelezwa ni kutoa kauli za kupingana na maamuzi ya umoja.

Ilikuwa mwanzo na pengine utamaduni uleule wa kuendeleza mbinu za kushughulikiana, kwa kuwa kimkakati UVCCM ni mabuti, ni magwanda, ni bunduki, ni mishale na hata pinde za kutumiwa na watu ndani ya chama ili kufanikisha matakwa ya kisiasa.

Hata yaliyompata Mwenyekiti wao, Hamad Masauni, ilikuwa mkakati huohuo wa kutumika na kutumiwa.

Ndiyo maana kwa miaka yote hii, umoja huu pamoja na kuwa ni taasisi yenye mpangilio unaoeleweka vizuri kikatiba, wakiwa na raslimali nyingi na kuwa ni jumuiko la vijana wenye siha ya mwili, umeshindwa kuwa chimbuko la mageuzi CCM kwenyewe na hata kwa taifa.

Vijana wamebakia maboi wa kutumwa kumwandama huyu, watagawanyika katika makundi makundi, watasakamana, na katika kufanya hayo, wanajikuta wakishindwa kukidhi matumaini ya vijana wenzao wa taifa.

Ile nguvu ya UV-CCM kuwa mfano wa nguvu ya kujenga mapinduzi ya kimaendeleo haina nafasi kwao.

Katika siku za karibuni, wamejitutumua kuja hadharani kuzungumzia mambo yanavyokwenda ovyo nchini. Hoja zao kuu zipo katika sura mbili:

Moja, ni utendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) na pili, malipo ya Sh. 94 bilioni kwa Dowans.

Katika hoja zote mbili, vijana wamekosa waziwazi kiwango kikubwa uhalisia cha kile wanachotaka waonekane wakisimamia.

Hili ni dhahiri kwa sababu, suala la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu si la kusumbua Umoja huo kwa kiwango hicho, au hata Dowans si jambo la kuwasumbua vijana wanaotamba kuwa na uwakilishi wa vijana wengi zaidi nchini.

Matatizo ya vijana wa taifa hili ni juu ya kukosa ajira, nyenzo na mikakati ya kuunganisha kundi lao kubwa ambalo hakika hata kidato cha nne hawakufika, kama walivyo baadhi ya viongozi wa UVCCM, ili watazame ni kwa njia gani nzuri na halali serikali inalazimishwa kuelekeza nguvu kwenye mambo hayo.

Ukombozi wa vijana, washiriki katika kuendesha uchumi wa taifa lao, ndiyo changamoto halisi ya UVCCM na si Dowans au Bodi ya Mikopo!

Lakini kubwa zaidi, nchi hii inayumbishwa na kikundi kidogo sana cha watu wale wanaoshiriki kila mpango mchafu wa kuibia serikali mabilioni ya shilingi.

Ninaamini UVCCM wanawajua watu hawa na wameona wanavyochuma kupitia serikali kiasi cha kuigeuza shamba la bibi wapendavyo.

Tatizo imekuwa vigumu kudhibitiwa na serikali ya CCM kwa kuogopa au kwa kuwa ipo kitandani nao imewaacha hata pale walipothibitisha wenyewe kuwa ni wezi kama walivyoiba kupitia EPA.

Ninasema haya kwa sababu ili kujitakasa mtu hana budi kuoga, si kunawa. Ukinawa utasugua miguu na mikono, labda na uso, lakini kwapa litabaki na harufu mbaya. Huwezi kukaa kwa raha.

Kila nikiwatazama vijana wa CCM na kelele wanazopiga kuhusu utendaji wa serikali napatwa na hasira kwa kuwa ni jambo la fedheha kuona vijana kama wale katika umri kama ule wameamua kuwa buti, gwanda, mshale au upinde wa kutumiwa na wengine kwa manufaa yao.

Wenyewe hawana ufahamu na mwelekeo wa kuanzisha vuguvugu la kweli la kuleta mapinduzi kama timu kubwa ya kimapinduzi. Wanaishia kuendeleza siasa zilezile za enzi za kina Guninita na Sukwa Said Sukwa. Wanatumiwa kisawasawa.

Zipo habari kwamba mkubwa mmoja mwishoni mwa wiki iliyopita alikuwa na wakati mgumu kusikiliza kundi la vijana wanaodaiwa waliunda timu ya kusambaza fomu za mgombea urais wa CCM mwaka jana kwa ahadi ya kupatiwa ajira.

Mkubwa huyo anadaiwa kupokea nyaraka za wasifu wa vijana hao ili kutafuta jinsi ya kuwapatia ajira.

Hebu tafakari, kiongozi aliyekuwa madarakani kwa miaka mitano, akiwa na nguvu zote za kusimamia mageuzi ya kiuchumi ili kila raia afurahie maisha mazuri kama raia mwingine yeyote, alishindwa kazi.

Badala yake akaahidi kikundi cha wana-CCM wachache wamfanyie kazi ya umma kuwa atawapa ajira kama ujira wa kazi hiyo. Hili linatokea na UVCCM wanajua. Ila wanapozungumza matatizo ya nchi hii wanakuwa wamefunga jicho moja. Hawaoni!

Leo nawaambia UVCCM hawawezi kupata uhalali wowote wa kuwakilisha vijana wa taifa hili kwa kukubali uboi; kwa kushindwa kuwaona kwa mapana yake vijana wenzao wanavyoishi maisha ya utwana bila ya kujali mwenye elimu au asiyesoma.

Haidhuru wanaishi mijini au vijijini, hali ni ngumu na mbaya kwa vijana, lakini UVCCM wanaungana na wale wanastahili adhabu kwa kulifikisha taifa katika matanga tuliyonayo leo.
 
Kwa Wakristo wanamfahamu vema yule kunguru aliyeachiwa na Noha kwenye safina kwenda kutazama kama maji yamepungua juu uso wa nchi baada ya gharika. Kunguru hakurejea bali aliishia kula mizoga.

Alitumwa kwenda kutafiti kwa niaba ya wengine mle safinani lakini hakurejea. Aliishia huko.

Niwaulize viongozi wa UVCCM wao ni kunguru wa Noha, au ni yule njiwa aliyetumwa baadaye na kurejea na jani kuashiria uhali unarejea juu ya uso wa nchi?

Vijana wanawezaje kusaidia kukomboa taifa kwa kukataa kuwa sehemu ya wafilisi nchi, kukataa kutumwa kusafisha uoza; kukumbuka kuwa ukombozi wa taifa hili ni lazima uanze na wao kwa kukataa kuwa maboi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: