UV-CCM hawamsaidii Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), unazidi kumdhoofisha Rais Jakaya Kikwete.

Hili lilidhihirika Alhamisi iliyopita, 20 Januari 2011 pale viongozi wa umoja huo walipokutana na wahariri wa vyombo vya habari, Hotel Peacock jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, vijana walitoa tamko lililosheheni mada tano: Hali ya CCM na UV-CCM iliwasilishwa na Mathayo Marwa, mwenyekiti wa umoja huo mkoani Mara.
 
“Mpango wa Dk. Willibrod Slaa na Chadema wa kuvuruga amani na kuifanya nchi isitawalike.” iliwasilishwa na Martine Shigela, katibu mkuu wa umoja huo.

“Viongozi wa dini na mjadala wa siasa,” iliwasilishwa na Benno Malisa, kaimu mwenyekiti wa UV-CCM taifa na makamu mwenyekiti wa umoja huo, wakati “Sakata la Dowans,” iliwasilishwa na James Milya, mwenyekiti wa umoja wa vijana mkoani Arusha.

Naye, Zainabu Kawawa, mbunge wa kuteuliwa na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) aliwasilisha “Matatizo ya vijana nchini.”

Katika yote hayo, kinachoonekana kuwa na baraka za wakubwa ni ajenda tatu – hali ya CCM, Dk. Slaa pamoja na Chadema na viongozi wa dini katika siasa. Yaliyosalia yalichomekwa na waliodaiwa kuwa wafuasi wa kambi ya aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa.

Kwa ujumla viongozi wa vijana walikwenda katika mkutano na wahariri wakiwa katika kundi moja, lakini lenye malengo tofauti. Hii ni kwa sababu, ndani ya UV-CCM kuna mgawanyiko.

Kwa mfano, wakati Malissa, Shigela na Ridhiwani, wakilenga kumtetea Kikwete, Marwa na Millya walikuwa na kazi moja ya kutaka kumsafisha Lowassa.

Ridhwani ambaye alikacha mkutano wa wahariri, ni miongoni mwa wajumbe 19 waliohudhuria kikao cha kamati ya utekelezaji na alikuwa mtu wa 11 katika orodha ya wajumbe waliosaini muhtasari wa kikao.

Mara baada ya mkutano kumalizika, baadhi ya wajumbe walisikika wakilalamikia Milya kuwa ameongeza vitu nje ya yale “tuliyokubaliana.”

Katika maelezo yake ya awali, Milya ambaye anafahamika alivyo mtiifu wa ndani wa Lowassa, alijitahidi kutotaja jina la kiongozi huyo.

Hata hivyo, alipobanwa na wahariri ili aeleze nani amemlenga na kwa dhamira ipi, alishindwa kujizuia.

Haraka alisema, “…tunataka kujua iwapo Kamati Teule ya Bunge chini ya Dk. Harrison Mwakyembe ilifanya kazi yake ipasavyo, au mheshimiwa Lowassa alijiuzulu kwa makosa.”

Kinachoonekana kupata baraka za wakubwa, ingawa nacho kinaweza kuwa “kilichakachuliwa,” ni mashambulizi dhidi ya Sitta, Mwakyembe, Dk. Slaa na viongozi wa madhehebu ya dini.

Ni Sitta na Mwakyembe ambao wamekuwa mstari wa mbele kupinga malipo ya Dowans/ Richmond. Katika hili Marwa alisema, “Wapo baadhi ya viongozi ndani ya serikali wanaoendeleza siasa za chuki, visasi na uhasama.”

Anaeleza, “Tunawataka kuacha mara moja mchezo huo mchafu,” vinginevyo “UV-CCM itawataka vijana kote nchini kuandamana na kuwalaani, maana uhasama na chuki zao zinaleta mipasuko katika jamii na chama kwa jumla.”

Hata hivyo, tuhuma dhidi ya Dk. Slaa na viongozi wa madhehebu ya dini ndicho kinachoonekana kutoka moja kwa moja jikoni. Hata waliosoma matamko hayo mawili, ni viongozi wakuu wa UV-CCM – Shigela na Malisa.

Kabla viongozi hao wawili wakuu ndani ya UV-CCM kufanya kikao cha Kamati ya Utekelezaji, taarifa zinasema walifanya kikao kirefu na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu serikalini na katika chama.

Karibu yote aliyoeleza Shigela kwa wahariri kuhusu Dk. Slaa yalikuwa ni yaleyale yaliyokuwa yanaelezwa na viongozi wakuu wa chama hicho, Yusuph Makamba na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu.

Ni yale ambayo yamekuwa yakiripotiwa na kuchapishwa kwenye vyombo vya habari vya serikali – gazeti la Habari Leo na Daily News, magazeti ya CCM – Uhuru na Mzalendo na magazeti ya Rostam Aziz – Rai, Mtanzania na The African.

Hata hivyo, alipobanwa na Khamis Dambaya kutoka Mlimani Televisheni, kuthibitisha madai yake, Shigela aliishia kusema, “Haya yanafahamika kwa kila mmoja.”

Dambaya aliuliza, “Shigela umepatwa na nini? Mbona hufanani na hiki unachokisema…? Unaumwa? Badala ya kutetea chama chako, umekuja kushambulia Dk. Slaa?”

Alisema, “…Unaeleza hatari ya Dk. Slaa kuangamiza Chadema, huelezi chama chako kitaathirika vipi kwa kufa kwa Chadema?”

Hata Malisa aliyetuhumu viongozi wa dini kujiingiza katika siasa, alishindwa kueleza sababu zilizofanya umoja huo kuamka sasa, wakati mwaka 2005 haukuinua kidole pale viongozi wa kidini walipomuita Kikwete “chaguo la mungu.”

Kama vijana wa UV-CCM walilenga kupiga vita ufisadi na kumsaidia Kikwete, wangetaka kwanza serikali itaje mmiliki wa Kagoda – kinara wa wizi wa mabilioni ya shilingi ndani ya Benki Kuu ya Taifa (BoT).
 
Wangemtaka Rostam Aziz aeleze jinsi alivyoweza kupata nguvu za kisheria za kusimamia malipo ya Dowans, wakati Novemba 2005, Dowans yenyewe ilikuwa haijasajiliwa?

Hata hivyo madai ya vijana na kutaka utata wa Richmond urejeshwe bungeni, hakuwezi kulenga kumsaidia Kikwete. Kunalenga kumuangamiza.

Hii ni kwa sababu, aliyekuwa mwenyekiti wa kikao cha Baraza la mawaziri kilichoridhia mkataba wa Richmond, alikuwa Kikwete.

Aliyeongoza kikao hicho na kuridhia mkataba kuvunjwa, alikuwa Kikwete; aliyepokea ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kabla ya kuwasilishwa bungeni na kuridhia kusomwa hadharani, kwa mujibu wa Lucas Selelii, aliyekuwa mjumbe wa kamati teule, alikuwa Kikwete.

Na aliyebariki kujiuzulu kwa Lowassa na mawaziri wengine wawili, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha alikuwa Kikwete pia.

Hivyo, kutaka kurejesha suala hili upya bungeni kutatoa fursa kwa baadhi ya wabunge kuhoji umakini wa serikali na kuhoji ushiriki wa rais katika suala hili.

Watapa nafasi ya kuhoji maslahi ya waliohusika katika mradi huu, ama kile walichoahidiwa.

Huu ndio utakuwa wakati muwafaka wa wananchi kudai maelezo kutoka kwa Kamati Teule kuhusu kile kilichoripotiwa kuwa kilifichwa ili “kunusuru serikali.”

Kukubaliana na hoja ya vijana, kutawapa  nafasi wabunge kumtaka Lowassa kuwataja washirika wake wengine katika suala hili.

Kulipeleka tena bungeni suala hili, kutatoa fursa kwa wabunge kumhoji Rostam kuhusu uhusiano wake na anayeitwa mmiliki wa Dowans. Jinsi alivyoshiriki kuileta kampuni nchini; na madai ya kutumia ikulu kulazimisha malipo.

Naye Sitta atatakiwa na bunge kuthibitisha taarifa zilizozagaa mitaani kuwa baadhi ya wajumbe wa kamati teule waliandaliwa mtego wa hongo na mmoja wa vigogo kwa lengo la kuficha baadhi ya taarifa za kamati hiyo. Atamtaja.

Dk. Mwakyembe naye atatakiwa kueleza jinsi mke wa mmoja wa watuhumiwa wa Richmond alivyofika nyumbani kwake na kumpigia magoti, akitaka kumuokoa mumewe.

Haya yote yakifanyika, Rais Kikwete hatabaki salama; CCM hakitakuwa kimoja; bunge litakatika vipande viwili – jambo ambalo linaweza kuangusha hata serikali.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: