UVCCM, kiota cha fikra finyu, matusi?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 27 May 2008

Printer-friendly version

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) tangu zama za TANU umechukuliwa kama kiota cha kulea na kutayarisha wanachama na viongozi wa kisiasa na hata wa kiserikali kwa lengo la kujenga siha njema ya kujitawala.

Ndio maana waasisi wa taifa hili kama Mwalimu Julius Nyerere walipata kusema lazima vijana wajengwe kuweza kujenga hoja. Wafundishwe na kujizoeza kujenga hoja, kutathmini vitu kwa kutumia tafakuri kwa sababu ni kwa njia hiyo tu wanaweza kutumia hazina waliojaliwa na Mungu; ubongo, kukabiliana na changamoto za maisha.

Pengine ni katika kutambua hili, mwaka 1994, Jaji Joseph Warioba, wakati huo akiwa mbunge wa kawaida alikumbusha vijana wa CCM wajibu wa kujifunza kujenga hoja na si kujiingiza katika malumbano ya kisiasa yanaoendeshwa kwa hisia.

Warioba alisema hayo akijibu tuhuma za aliyekuwa Katibu Mkuu wa UVCCM ambaye alikuwa mbunge pia, Sukwa Said Sukwa. Sukwa akisukumwa na hisia zisizokuwa na hoja, alipandisha mori na kumsakama Warioba bungeni.

Alimwambia amesukumwa na tamaa ya madaraka ndiyo maana aliwasilisha hoja binafsi ya kulitaka Bunge kuishurutisha serikali izingatie maoni ya wananchi kabla ya kufanya mabadiliko ya katiba na hasa, mambo yanayohusu Muungano.

Sukwa akasema Warioba amesukumwa na ubinafsi zaidi ndiyo maana wakati akiwa Waziri Mkuu hakufanya hayo aliyokuwa anayapendekeza.

Hakuishia hapo. Alitaka waziri mkuu wa wakati huo, Cleopa Msuya, akiondoka kwenye kiti hicho asiwe kama Warioba. Kwa kifupi, kauli za Sukwa zilivuka mpaka wa kutambuwa mantiki ya hoja. Alikuwa ameishiwa hoja na kupumzisha ubongo.

Warioba alikuwa amewasilisha hoja hiyo na kwa hakika baadaye aliiondoa baada ya serikali kumuomba kwa sababu tayari ilikuwa katika mchakato wa kutekeleza hayo aliyokuwa anapendekeza.

Akijibu michango mbalimbali ya wabunge waliokuwa wamechangia hoja yake, kabla ya kuiondoa, Warioba alisema: ?kuhusu Sukwa sina la kusema kwa sababu alichokizungumzia ni hisia zake. Siwezi kujibu hisia. Ila kama aliyoyasema yanawakilisha nguvu ya umoja wa vijana, basi kuna tatizo kubwa katika umoja huo.?

Warioba alikumbusha kwamba ni vema vijana wakajifunza kujibu hoja. Kujenga hoja, kwa sababu huko ndiko viongozi wa taifa hili wanaandaliwa.

Nimekumbuka kauli hiyo ya Warioba baada ya kuikuta kauli inayofanana na ya Sukwa iliyotolewa takribani wiki mbili sasa na kiongozi mwenye wadhifa ule ule wa Sukwa mwaka 1994. Huyu ni Katibu Mkuu wa UVCCM, Francis Isaac Mtinga.

Mtinga kwa sababu zozote, akijibu kauli za viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kuhusu kutokuwa radhi kurejea kwenye mazungumzo na viongozi wa CCM juu ya mwafaka wa Zanzibar, aliwataja viongozi wa CUF kwa lugha isiyovumilika.

Pamoja na mambo mengine. Mtinga alisema Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ni profesa wa mitishamba, na kwamba Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, ana akili ya kuku, yaani anasahau mapema!

Sina sababu ya kurejea wasifu wa Profesa Lipumba hapa, lakini yatosha tu kusema hakuna ubishi juu ya kiwango cha elimu yake. Huyu ni profesa wa uchumi.

Dunia inamtambua na inamtumia kitaalamu, wanafunzi wake wamezagaa duniani kote tena wengine ni mawaziri katika baraza la mawaziri la Rais Jakaya Kikwete. Huwezi kuwaza achilia mbali kuthubutu, kusema Lipumba ni profesa wa mitishamba.

Kadhalika kwa Maalim Seif, mtu aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, msomi aliyeweka rekodi ya kufaulu vizuri alipokuwa akisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ambaye ujanani kwake kama kada wa CCM, alitumika ipasavyo kujenga chama katika Idara ya Uchumi.

Mtu kudai leo kwamba Maalim Seif ana akili ya kuku, si kwamba tu anamtukana msomi huyu mahiri, bali anajitukana hata yeye binafsi huku akithibitisha alivyo dhaifu katika uelewa wa mambo. Naye amepumzisha ubongo.

Naweza kuelewa hasira za Mtinga. Anataka kutetea chama chake dhidi ya mashambulizi ya CUF kuhusu suala la mwafaka. Naweza pia kutambua ana damu inayochemka, ya ujana, anataka kuendesha mapambano.

Lakini nashindwa kumwelewa anataka kuendesha mapambano ya hoja au ya matusi? Kama ni matusi, naona hana ubavu wa kufikia makuli kule bandarini, au sokoni Kariakoo. Wao wamebobea kwenye matusi.

Sitaki kuamini kuwa ndani ya UVCCM kuna nafasi ya matusi, si kwa mwanachama wa kawaida bali hata kwa kiongozi tena wa ngazi ya juu kama yeye.

Lipo fundisho moja kubwa: yale aliyoyazungumza Warioba miaka 14 nyuma, hayajafanyiwa kazi. UVCCM haijafanikiwa kujenga viongozi wake katika uwezo wa kujenga hoja. Wakikasirishwa wanaporomosha matusi badala ya hoja za kubomoa wapinzani wao. Hii ni hatari.

Hatari inayojitokeza hapa ni kwamba UVCCM ilitarajiwa kuwa kiota kama si tanuri la kupika vijana, wawe makada walioiva wa CCM au viongozi mahiri kwa taifa. Wajenga hoja.

Mwaka 1994 Sukwa alithibitisha kukosa sifa hizo. Alijikita katika hisia, mwaka 2008, mshika kiti kama chake, anajikita katika matusi. Je, hii si kuyumba kwa msingi wa taifa katika kupata viongozi bora?

Ayubu Rioba, katika makala zake, anasema kuna hatari ya taifa letu kupata viongozi waliodumaa kiakili kutokana na kukosa lishe bora wakiwa watoto na sasa wamepitia mchakato wa kusaka uongozi na kukalia ofisi za umma huku bongo zao zikiwa zimevia. Hawana cha kutoa kwa ajili ya kujenga taifa.

Akina Sukwa na sasa Mtinga ni mfano hai. Katika hali ya kawaida inakuwa vigumu kuelewa inakuaje watu wa aina yao kufikia kilele cha uongozi wa UVCCM halafu wakose kujenga hoja na kubaki kutoa matusi na hisia!

Kama akina Sukwa na Mtinga ndio tunda la mchakato wa kupika viongozi wa taifa kupitia umoja huu, si tunaanza kutambua chimbuko hasa la kudumaa maendeleo ya nchi?

Mwalimu Nyerere alisema ili tuendelee tunahitaji mambo matatu: watu, siasa safi na uongozi bora. Ardhi ilikuja kuongezeka baadaye. Tangu uhuru, taifa hili halina shida ya ardhi, wala watu, labda siasa safi au uongozi bora.

Lakini kwa jinsi mambo yanavyojidhihirisha kubuni siasa safi ni matokeo ya uongozi bora. Haya mawili yanategemeana. Kama una viongozi ovyo, hakika siasa safi haiwezi kupatikana.

Tanuri la kupika viongozi bora, yaani UVCCM, limepandikizwa watu ovyo, na kwa hivyo tunaishia kupata siasa ovyo na viongozi ovyo. Vijana wasioweza kujibu hoja, wanaoporomosha matusi, ni watu dhaifu wasioweza kuhimili mikikimikiki ya siasa shindani achilia mbali kuweza kubuni mikakati ya kukwamua taifa lao kutoka lindi la umasikini.

Hawa ni ndio CCM inatuandalia waje kuwa viongozi, mawaziri wa kesho na Mungu aepushe mbali, marais wa kesho. Kweli tumo katika mkwamo mkali.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: