UV-CCM wamekosa adabu, maadili


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

KWA kuzingatia mila na desturi za Kiafrika, tunaweza kutamka kwa uhakika kuwa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), umekosa adabu.

Hili linahusishwa na kile ambacho kinaitwa “malumbano kati ya viongozi wa UV-CCM na viongozi wastaafu serikalini na baadhi ya mawaziri wa sasa ndani ya serikalini ya CCM.

Wiki mbili zilizopita tulisikia matamko ya UV-CCM mkoani Pwani, Dodoma, Kilimanjaro na Tabora. Hali kadhalika tulisikia tamko la waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye na pia kauli ya waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta kuhusu shutuma alizotupiwa na viongozi wa umoja huo.

Katika yote hayo, kuna harufu ya vijana wa CCM kuonekana wanakosa adabu kwa kulumbana na wazee wa aina ya Sitta na Sumaye. Kama wamefanya hivyo kwa kutumwa, basi hata aliyewatuma hana adabu kama wao.

Kwetu tuliolelewa na kukulia ndani ya CCM, kuna ukweli mmoja wa kutisha unaojitokeza pale tunapotazama na kutafakari juu ya matamko ya UV-CCM.

Jumuia hii muhimu imeshuka hadhi katika kila fani. Ukianza na ukomavu na uadilifu wa viongozi, utaona kuna ufa mkubwa kati ya UV-CCM ya sasa na ile ya zamani.

Mathalani, huwezi kumlinganisha katibu mkuu wa sasa wa umoja huo, Martine Shigella na waliomtangulia ambao walijenga taswira ya UV-CCM iliyokuwa lulu na chombo cha kujivunia.

Kwa mfano, Mohamed Seif Khatibu, Salum Juma Othman na Sukwa Said Sukwa walikuwa ni vijana walioambukiza vijana wengine kuiga uzalendo wao na jeuri yao isiyo na hila ndani yake.

Kwa watu wengi, jengo la Makao Makuu ya UV-CCM, pale Lumumba, Dar es Salaam, kama ilivyokuwa ikulu ya Mwalimu Julius Nyerere, liliheshimika na liliwatisha sana watu wasio na maadili wala uzalendo. Siku hizi majengo hayo yote yamegeuka vijiwe. Hata mafisadi wakuu hawayaogopi.

Wenyeviti wa UVCCM kama Andrew Masanje, John Guninita na miaka ya mwanzo ya Emanuel Nchimbi, huwezi kuwalinganisha na makamu mwenyekiti wa sasa Beno Malisa na genge lake.

Kinachotofautisha vijana hawa ni ukweli kuwa wa sasa ni vishada vyepesi: hawana kishindo cha hoja, hekima wala adabu na hawajui siasa; wakati wale wa zamani walikuwa ni vijana kweli; waliopikwa wakaiva na kukipa chama hadhi mbele ya umma.

Hukumu hii inahitaji mafafanuzi isije kuonekana vijana hawa wameonewa. Baba wa taifa alianza siasa akiwa kijana. Sambamba naye walikuwa vijana wengine wengi akina Rashid Kawawa, Oscar Kambona, Saidi Fundikira na wengineo.

Kilichoonyesha ujana wao si umri waliokuwa nao, bali ni misimamo thabiti ya kizalendo na kujitoa mhanga; wakitanguliza maslahi ya taifa. Vijana hao, baadhi yao walipoteza kazi, walishitakiwa, walifungwa na hata kutengwa katika familia zao na dini zao kwa sababu ya kutoyumba katika misimamo yao iliyojaa uzalendo.

Haikuwahi kutokea kusikia wakipigania marafiki zao, makabila yao wala maeneo wanakotoka. Baadhi yao walifikia hata kutofautiana na chama cha Tanganyika African National Union (TANU) pale walipohisi kinataka kwenda kinyume na ajenda ya uzalendo kwa taifa lao.

Miaka mingi baadaye, Mwalimu Nyerere alikiri kuwa katika Tanu Youth  League (TYL) kulikuwa na wajamaa safi kuliko hata yeye.

Kauli hii iliwashangaza wengi kwa sababu watu walikuwa wanaamini kuwa Nyerere alikuwa mjamaa Na. 1 na mtu pekee wa kuigwa katika kuulezea na kuutekeleza ujamaa.

Uzalendo huu wa vijana uliambukiza chachu ya uzalendo kila idara ya serikali na hata katika kada nyeti kama usalama wa taifa. Maafisa wa serikali wenye hulka ya ufisadi, waliwaogopa vijana. Walijua hawaongeki. Hawanunuliki.

Chachu hii ilivuka hadi Visiwani. Vijana na uzalendo wao, walisimamia muungano tulio nao sasa. Majaribio yote ya kuuvunja yalifichuliwa na kuhujumiwa na vijana na TYL/UVCCM wakisaidiana na idara ya usalama wa taifa.

Kwa ujumla, vijana wakawa nguzo muhimu ya chama na kielelezo halisi cha uzalendo katika serikali ya awamu ya kwanza na, kwa sehemu fulani, awamu ya pili.

Bali inasikitisha sasa kuona waliolelewa na kukulia ndani ya jumuia ya vijana, ndio vinara wa ufisadi na madalali wa kueneza ufisadi ndani ya chama chetu.

Ufisadi uliofanywa chini ya uongozi wa akina William Lukuvi na Didas Masaburi, katika mradi wa mabasi ya wanafunzi jijini Dar es Salaam, au ule ulioghubika mikataba tata ya ujenzi wa kitega uchumi cha UV-CCM chini ya uongozi wa Francis Isaac, Emmanuel Nchimbi na Benno Malisa, ni dalili ya wazi kuwa chachu ya uzalendo katika UV-CCM imeisha, kilichobaki ni ujasiriamali na udalali wa raslimali za taifa na jumuia yake.

UV-CCM ilikuwa kiwanda cha kuzalisha viongozi ndani ya chama na serikali. Kwa hiyo kuenea kwa ufisadi ndani ya chama na serikali ni ushahidi kuwa UV-CCM imedhoofika, imechoka, imechafuka na inaeneza kirusi cha ufisadi katika taifa.

Watu kama Isidory Shirima, Ole Njoolay, Leonidas Gama, Hinju, Henjewele, Paschal Mabiti na mamia ya makada walikuwa viongozi na watumishi katika sekretariati ya UV-CCM huko nyuma. Baadhi yao, kama Lowassa, wanapotajwa kuhusishwa na ufisadi, hakika inatia doa historia tukufu ya UVCCM.

Lakini pia wapo ambao chachu ya uzalendo haikuzimika kabisa. Watu kama akina Ole Sendeka, Frank Uhahula, Philip Mangula, Wilson Mukama, na wengine wachache, ni mifano ya mbegu ya uzalendo ya wakati wa TYL na baadaye UV-CCM ilipokuwa na vijana siyo wababaishaji.

Ni vigumu kujua UV-CCM ya sasa inawawakilisha akina nani katika taifa maana mtandao wake hauonekani katikati ya vijana, bali mtandao wao umejikita katikati ya wazee wanaotafuta urais na nafasi nyingine za chama.

Vijana hawa na viongozi wao, kazi yao kubwa imekuwa ni kutapeli watu kwa madai kuwa watawasaidia kupata nafasi za uongozi. Hii ndiyo sababu hata katika tamko la hivi karibuni, wamediriki kusema watahakikisha wazee wanaokikosoa chama hawapati nafasi ya kuongoza.

Kundi hili la vijana wa leo, likiongozwa na Shigella, linatembea nchi nzima na karatasi zenye nembo ya ikulu na sahihi za kughushi, likiahidi watu vyeo katika serikali na chama.

Kwa kuwa UV-CCM imetekwa na kundi hili ambalo halina mawasiliano kabisa na maisha halisi ya vijana ndani na nje ya chama, ni vema kwa usalama wa CCM kufuta jumuia hii na kuiunda upya na kwa vigezo vipya.

Halikuwa kusudi la CCM kuunda jumuia ya matapeli na vibaka ndani ya UVCCM, bali jumuia yenye maadili na inayokuza uzalendo miongoni mwa vijana.

>Mwandishi wa makala hii, amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI. Anapatikana kwa imeil: tutikondo@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: