UV-CCM wanatumwa, wanatumika


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version

MWAKA 1994 John John Guninita alikuwa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wakati huo pia akiwapo Katibu Mkuu wake, Sukwa Saidi Sukwa, hawa waliokuwa ni wanasiasa vijana wa wakati huo walioonekana ni watu jasiri sana.

Uongozi wa Guninita ambaye leo hii ni mwenyekiti wa chama hicho mkoani Dar es Salaam, ulikuwa na ujasiri ambao ni nadra sana kuuona katika miaka ya hivi karibuni.

Guninita akiwa ama ametumwa au kwa kujituma mwenyewe, walikaa na kuamua kufanya kitu ambacho kilimgharimu mno kisiasa. Hawa waliamua kuwaidhinisha wanachama wa CCM au tusema makada ambao walidhani kwa upeo wao walistahili kurithi mikoba ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Waliotajwa na akina Guninita kwamba wanastahili kuwa wagombea urais kupitia chama hicho, ni Jakaya Kikwete; Dk. Salim Ahmed Salim; Edward Lowassa na Jaji Mark Bomani. Tamko lao lilizua taharuki kubwa ndani ya chama chenyewe.

Wakongwe kama Mzee Kingunge Ngombale Mwiru wakati huo akiwa ndiye Katibu wa Uenezi na Itikadi, aliwajia juu akina Guninita kwamba walichofanya ni kinyume cha taratibu na kanuni za CCM, kwa kuwa taasisi yoyote ndani ya chama hicho hairuhusiwi kumpitisha mgombe yeyote bila kwanza kupitia katika mchakato wa chama.

Guninita ambaye aliamini kuwa alikuwa amekalia kiti cha uenyekiti wa UVCCM vilivyo, alimjibu kwa kiejeli na mbwembwe Kingunge kwamba “Kingunge si CCM.”

Sote tu mashuhuda kilichotokea pake makao makuu UVCCM, walisambaratishwa wote. Mwisho Guninita alikuja kuibukia CHADEMA ambako ripoti zinasema alipigika hadi akajisalimisha mwenyewe CCM, baada ya kutema ukuu wa wilaya na kujaribu kusaka jimbo kupata ubunge katika uchaguzi wa mwaka 1995.

Kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa kuna picha inajengeka pale makao makuu ya UVCCM ambayo inafanana kwa karibu sana na ile ya mwaka 1994 ya akina Guninita na wenzake.

Safari hii vijana wamejitia ukiranja wa juu kabisa wa CCM, wanawakemea viongozi wastaafu, wanawakemea hata mawaziri; lakini taarifa za ndani kabisa zinasema wameamua sasa kumtaka hata mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, aivunjilie mbali sekretariati ya chama chao.

Vijana hawa wamekwenda mbali zaidi na sasa wanatisha baadhi ya makada wakongwe wa chama hicho kwamba kama hawataacha kuikosoa serikali, watapiga kampeni chafu dhidi yao hata kama watakuwa wamepitishwa na chama chao kuwania nafasi za juu za uongozi.

Ingawa muda uliobaki hadi kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwingine ni mrefu kwa maana kuwa uchaguzi utafanyika mwaka 2015, harakati za vijana hawa zinaonyesha dhahiri kulenga kwenye uchaguzi mkuu.

Vijana wa CCM mikoani wamegawanyika, wanaonyesha dhahiri kuna makundi ya wazi yamejijenga kuelekea uchaguzi mkuu.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya mwelekeo mpya wa siasa za CCM, waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alisema wazi kwamba wapo watu wamekwisha kuanza kukusanya fedha kwa ajili ya uchaguzi.

Alisema wengi wao wameshaanza kuunda mtandao; ndiyo maana kila anayesema lolote kuhusu chama au serikali anashambuliwa kwa kuwa anadhaniwa kuwa anasaka urais pia.

Katika makala zangu nyingi nilizowahi kuandika huko nyuma nimekuwa na tabia ya kuwahoji vijana swali moja tu: “Hivi wanatumwa na pengine kujitoa mhanga kwa ajili ya watu kupata ukubwa halafu iwe nini?” Wengi ninaopata bahati ya kukutana nao uso kwa uso aghalabu huwa hawana jibu la kunieleza mbali tu ya kuamini wanawajibika kutumwa.

Wengi wa vijana wanaotumwa wanakuwa na matumiani dhaifu mno jinsi ya kunufaika katika nchi yao; wapo wanaoamini kwamba kwa kutumwa kuzoza ovyo ovyo tu, au kwa kutumwa kufanya vitu ambavyo vinaonyesha dhahiri havitumii hata chembe ya bongo zao, huenda wakaambulia ukuu wa wilaya baada ya uchaguzi.

Ukitafakari sana kuna nafasi ngapi za ukuu wa wilaya ni kichekesho; kwanza wilaya zenyewe hata hazifiki 200 na hata kama nafasi zote zingekuwa ni kwa ajili ya UVCCM bado zisingewatosha.

Lakini ni bahati mbaya kwamba nafasi hizi zinatolewa macho na kila kada wa CCM aliye hoi, ambaye aliacha kufikiri siku nyingi na kuamini maisha yake yako katika kutumwa tu.

Kwamba UVCCM kama taasisi ambayo ingekuwa chimbuko la vijana wenye fikra pevu; kwamba wao wangekuwa ni sehemu ya chama kukimbilia kuchota nguvukazi yenye nguvu, ari na uwezo kufanya kazi, imeamua kujiua kuwa kokoro la kutumiwa na yeyote ilimradi tu ana fedha za kuwalambisha ili wafanye kile wanachotumwa.

Vijana hawa hawajawahi kujiuliza maswali magumu kwa muda mrefu sasa, tangu zama za akina Guninita na hata sasa kama unavyoonekana ni makundi ya kutumwa.

Angalau wangelikuwa wanatumwa kwa ajili ya kutibu taifa, ingeweza kueleweka, bali ni bahati mbaya vijana hawa wanatumwa kwa sababu ya njaa zao tu.

Wapo vijana wengi ndani ya UVCCM wanamini kuwa UVCCM ni ajira; hawajishughulishi kwa kazi yoyote, wamekaa kusubiria kazi ya kutumwa, wamekaa mkao wa kuambiwa nenda kafanye hiki au kile na kwa sababu kimsingi hawawezi kusimama kwa miguu yao wenyewe basi, hujikuta wakishindwa kuamua kwa utashi wao wenyewe ni nini hasa wanachosimamia.

Kwa muda mrefu sana siasa za ndani ya CCM zimejielekeza kuruhusu watu waliokimbia shule kuwa ni ndio makada, kila unayemgusa ukitaka kuchungulia CV yake utaishiwa nguvu.

Wengi wao wana upeo mdogo kwa sababu waliamini katika majungu, fitna na kupiga domo; ni wachache sana waliokwenda shule ipasavyo, ukiacha wale wachache wenye nasaba za ndani kabisa na wakubwa.

Matokeo ya kuwa na UVCCM iliyojaa watu wepesi namna hii, kwao kuhoji mambo kwa nia ya kusaka mantiki ya ndani ya hoja haipo, njia pekee wanayoweza kufanya ni kutishana, kuchafuana na kuwa tayari kutumwa kokote kwa nia ya kumng’ata yeyote anayeelekea kupingana na kutaka kupambana na huyo anayewafadhili.

Unapokuwa na umoja wa vijana wa namna hii, hakika unafikia kwenye lile hitimisho alililopata kulitoa Jaji Joseph Warioba mwaka 1994 wakati akijieleza kuhusu hoja yake binafsi aliyokuwa amewasilisha bungeni.

Warioba akiwa amewasilisha hoja binafsi juu ya mambo ya Muungano na akilitaka Bunge kupitisha azimio la kuitaka serikali isibadili mambo ya Muungano bila kwanza kupitia taratibu zilizoainishwa kikatiba, alishangazwa na kauli za Sukwa.

Ingawa Warioba baada ya kuombwa na baadhi ya wabunge wakiwamo mawaziri aliamua kuondoa hoja hiyo bungeni, alizungumza kwa kina juu ya mchango wa Sukwa.

Wakati akichngia hoja ya Warioba, Sukwa alitoa kauli ambazo hazitofautiani sana na za vijana wa UVCCM wa sasa. Alimjadili Warioba badala ya kujadili hoja.

Warioba alitoa angalizo kwa wabunge na CCM akisema kama hoja za Sukwa ndio aina vijana wa CCM, basi chama kilikuwa na tatizo. Alitaka vijana wafundishwe kujenga hoja kwa kuwa ni kitalu cha kujenga viongozi wa chama.

Nikipiga picha nyuma mwaka 1994, leo ni takribani miaka 17 tangu Warioba atamani vijana wa UVCCM wafundishwe kujenga hoja, kwa bahati mbaya sana ugonjwa ule wa Sukwa wa mwaka ule ndio huo huo vijana wa leo wa UVCCM wanaugua.

Hawajiwezi kihoja na kifikra, wameishia kuwa watu wa kutumwa na kushambulia watu badala ya kujenga umoja wao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: