Uwakilishi wanawake CCM utata mtupu


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 14 January 2009

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa katika mchakato wa kutafuta utaratibu wa kupatikana asilimia 50 ya uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya uwakilishi.

Tayari chama hicho kimeunda kamati itakayoratibu mchakato huo. Mwenyekiti wa kamati hiyo ni Waziri Kiongozi mstaafu wa Zanzibar, Dk. Mohammed Gharib Bilal ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma.

Uamuzi wa kutaka kuongeza uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya uwakilishi unatokana na serikali ya sasa kutaka kutimiza matakwa ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Wanachama wa SADC wameazimia kila nchi mwanachama kuchukua hatua zitakazoiwezesha kufikisha uwakilishi wa angalau asilimia 50 ya wanawake katika Bunge na mabaraza ya madiwani.

Ingawa SADC haikuweka ukomo wa kutekelezwa azimio hilo, serikali ya CCM, chini ya Rais Jakaya Kikwete, inataka kutimiza azimio hilo ifikapo mwaka 2010 utakapofanyika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Baada ya kupata maoni mbalimbali, kamati ya Dk. Bilal iliwasilisha taarifa ya mapendekezo ya njia ya kupata uwakilishi wa idadi hiyo ya wanawake. Taarifa ya kamati ilijadiliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ilipofanya kikao mjini Dodoma mwishoni mwa mwaka jana.

Miongoni mwa mapendekezo ni kuundwa upya kwa majimbo ya uchaguzi, hatua inayopaswa kutekelezwa kwa kuvunja majimbo ya sasa.

Kamati ilipendekeza pia kila chama cha siasa kitakachoingia kwenye uchaguzi mkuu, kisimamishe wagombea wawili kwenye jimbo au kata, mmoja akiwa mwanamke.

Kwa kuwa mchakato huo unafanywa na CCM ambacho ni chama tawala, mtu ungesema waachiwe waendelee na utaratibu wao. Lakini kwa sababu suala la kuongeza uwakilishi kwenye vyombo vya maamuzi linahusu Watanzania wote, sharti raia waulizwe maoni yao.

Isitoshe, CCM imekuwa na mtindo wa mawazo ya wanachama wake kukomazwa na kuchukuliwa kuwa ndio mawazo ya Watanzania wote, hata wale wasiopendelea vyama vya siasa.

Zipo taarifa kwamba baadhi ya wana CCM wenyewe, walipinga mapendekezo ya kuvunja majimbo ya sasa na nguvu yao ya ushawishi ilisababisha NEC kuagiza kamati ya Dk. Bilal kufanya uchambuzi tena na kuwasilisha maoni yake.

Pendekezo jingine lililojadiliwa ni haja ya kuzifanya wilaya zote nchini kuwa majimbo ya uchaguzi kwa ajili ya wanawake. Hili lilikubaliwa ingawa lilihitaji hatua zaidi.

Pendekezo hilo la kuzifanya wilaya kuwa majimbo ya uchaguzi, litawezesha uwakilishi wa wanawake bungeni kufikia asilimia 38. Hii ina maana kwamba kutakuwa na pengo la asilimia 12. Kamati ilisema pengo litafidiwa na majimbo mengine ya kawaida ya uchaguzi pamoja na nafasi 10 za rais za kuteua wabunge.

Pendekezo hilo linahitaji kuwasilishwa serikalini ili kuendelezwa katika utaratibu wa kulitungia muswada wa sheria ndipo lifike bungeni.

Zinapokuja taarifa kwamba pendekezo hilo ndilo litatungiwa muswada, maana yake lile la kuvunja majimbo limekataliwa.

Watetezi wa pendekezo hili, wanasema litasaidia kupunguza idadi ya wabunge wa upinzani maana katika mazingira ya sasa hawataweza kukidhi matakwa ya sheria ya kusimamisha mwanamke kila jimbo.

Lakini wapo baadhi ya wanachama wanaopinga wakiamini kwamba huo ni utaratibu unaominya demokrasia.

Moja ya kanuni za demokrasia ni wale wachache baada ya uchaguzi, nao kusikilizwa. Utaratibu unaopendekezwa na CCM unapingana na hili na unaendeleza mtindo wa mshindi kuchukua yote.

Wanasema utaratibu huo unaojali, kutathmini na kuhesabu thamani ya kila kura inayopigwa, utanufaisha upinzani.

Wengi wa wajumbe wa NEC waliohudhuria mjadala wa mapendekezo ya kamati ya Dk. Bilal, walipendelea utaratibu wa uwakilishi wa kura za uwiano unaotumika sana nchi za Skandinavia. Huu unawezesha hata vyama visivyopata kura za kutosha, kushirikishwa kwenye utawala.

Utaratibu wa kuzifanya wilaya zote kuwa majimbo ya uchaguzi kwa wanawake, umeungwa mkono na wengi. Hata hivyo, kwa kuzingatia uwezo wa bunge la sasa kukaa wabunge wasiozidi 360, wabunge wanaweza kufika 400.

Pamoja na kwamba ukumbi uliopo hautatosha, idadi hiyo ya wabunge inakaribia ya India, taifa la pili duniani kwa kuwa na watu wengi na lina uchumi mkubwa zaidi ya Tanzania.

Kwa sasa, serikali ina maombi yapatayo 40 ya wilaya mpya na zaidi ya 30 ya majimbo. Ni dhahiri, kuongeza wilaya na majimbo kutaongeza wabunge na fedha nyingi za kuwahudumia.

Uchumi wa Tanzania hautahimili mzigo huo, hasa pale inapoelezwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta kwamba gharama za kumtunza mbunge kwa mwaka ni kiasi cha Sh. 270 milioni.

Lipo tatizo jingine. Kuna hatari ya kuzidi kukandamiza na kubagua wanawake kwani kwa kutenga wilaya kama majimbo yao, wengi wa wale wanaoshikilia majimbo watanyanyasika.

Hii ina maana kwamba wanawake watakaoingia bungeni au katika mabaraza ya udiwani, wataingia kwa shingo upande maana watakuwa wamebebwa.

Mwandishi ni mjumbe wa NEC-CCM
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: