Uwapi umakini wa serikali?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 03 February 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KUONDOSHWA kwa Muswada wa Sheria ya Baraza la Usalama wa Taifa katika mjadala bungeni kunatupa fundisho moja kubwa: Serikali imechoka kuwajibika.

Ni kitu kisichotarajiwa kwamba miaka minne na zaidi tangu serikali ya Rais Jakaya Kikwete iliposhika madaraka inajikuta ikilazimika kuondoa muswada wake bungeni ili kuufanyia marekebisho.

Muswada huo uliwahi kusomwa kwa mara ya kwanza mwaka jana, ukakataliwa. Serikali ilitakiwa kuuandaa tena kwa kuzingatia marekebisho mbalimbali.

Maswali mengi yanazuka katika hali kama iliyoukumba muswada huu uliowasilishwa tena bungeni tarehe 30 Januari na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba.

Tumeshtushwa kwa matokeo haya. Sababu za mshtuko ni nyingi zikianzia na kuhoji umakini wa Baraza la Mawaziri lililopaswa kuujadili kwa kina kabla ya kuukubali.

Hapa tunapata shaka kwamba inawezekana vikao vya baraza hili vinaitishwa katika mazingira mabaya au mawaziri na rais wanaogopana kiasi cha kushindwa kukosoana na kuondoa kasoro hizo.

Vile vile, tunajiuliza: Hivi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na kikosi chake cha wanasheria mahiri, alikuwa wapi asione kasoro zilizomo kwenye muswada?

Labda aliziona kasoro. Je, alizieleza kwa waziri mhusika? Je, waziri huyo alizitambua na kuzirekebisha?

Taarifa tulizopata ni kwamba Mwanasheria Mkuu alimshauri waziri Simba asiupeleke muswada bungeni. Lakini taarifa hizi zinatia shaka kwa kuwa mshauri mkuu huyo wa masuala ya kisheria kwa serikali alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu kasoro zilizotolewa na wabunge alisema, “muswada hauna kasoro.”

Kwanza, katika ngazi ya Bunge, muswada ulipaswa ujadiliwe kwa kina na Kamati ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje yenye uzoefu na masuala yanayogusa ulinzi na usalama wa nchi.

Pili, kuna mtazamo kwamba huenda muswada wenyewe umekusudiwa kutimiza matakwa ya watu fulani katika utawala huu, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Mtazamo huu unakuzwa na ukweli kwamba zaidi ya mara moja, serikali imehusishwa na kuandaa miswada kwa kuwalenga watu wasiokubaliana na matakwa ya wakubwa.

Tunapotafakari kwa undani zaidi, tunang’amua kwamba mazingira yaliyopotisha muswada huu ni kama yale yanayoifanya serikali kuingia katika mikataba mibovu na wawekezaji.

Hali hii inawafanya Watanzania kutilia shaka uwezo na umakini wa serikali ya awamu ya nne.

0
No votes yet