Uzembe, hujuma nyingine Bohari ya Madawa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

HII ni kashfa nyingine kwa menejimenti ya Bohari Kuu ya Madawa Nchini (MSD). Katikati ya tuhuma kwamba MSD imeacha dawa zenye thamani ya Sh. 8 bilioni kuharibika, imepokea shehena nyingine ya dawa yenye thamani ya Sh. 500 milioni ambayo muda wake wa matumizi utaisha miezi mitano ijayo.

Katika semina iliyoandaliwa na MSD mjini Dodoma wiki mbili zilizopita, wabunge waliishutumu menejimenti yake wakidai hawaridhishwi na utendaji kazi katika taasisi hiyo ya umma.

Walisema taasisi hiyo nyeti kwa afya ya binadamu inafanya kazi kwa mazoea hivyo kushindwa kukidhi matakwa ya kuwepo kwake.

“Nashangaa mnakuja hapa mnaanza kutuambia mafanikio yenu. Mafanikio gani hayo wakati zahanati hazina dawa? Mimi napendekeza MSD ipate mshindani ili ukiritimba uondoke na kama ikiwezekana pia watu binafsi waruhusiwe kufanya kazi za MSD,” alisema Naibu Spika wa Bunge, na mbunge wa Kongwa Job Ndugai.

Baada ya semina hiyo na baada ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwasilisha makadirio ya matumizi kwa mwaka wa fedha 2011/ 2012, MSD imenunua dawa za kupambana na maradhi ya ukimwi ambazo zinatakiwa kutumika kabla ya Januari 2012.

Dawa hizo ni zilizotengenezwa na viwanda vya Hetero Drugs, CIPLA na Aurobindo vya nchini India. Shehena hiyo yenye thamani ya Sh. 500 milioni, ilipokewa nchini 6 Julai, 2011. Nyaraka zinaonyesha:

  • Dawa aina ya Lamivudine Oral Solution zilizotengenezwa na kiwanda cha Aurobindo Agosti 2010, muda wa mwisho wa matumizi ni Januari 2012 yaani miezi mitano ijayo.

  • Dawa aina ya Nevirapine Oral Suspension kutoka kiwanda hicho hicho iliyotengenezwa Julai 2010 muda wa mwisho wa matumizi ni Juni 2012.
  • Aidha, dawa aina ya Lamivudine 150mg + Stavudine 30mg + Nevirapine iliyotengenezwa na kiwanda cha Hetero Drugs Septemba 2010, mwisho wa kutumia ni Septemba 2012.
  • Vilevile Zidovir Oral Solution iliyotengenezwa na CIPLA Aprili 2010, mwisho wa matumizi ni Machi 2012; dawa aina ya Duovir -N- Tablets kutoka CIPLA iliyotengenezwa Aprili 2010, mwisho wake wa matumizi ni Machi 2012.
  • MSD imeagiza dawa aina ya Lamivudine 150mg + Stavudine 30mg + Nevirapine 200mg kutoka Hetero Drugs ambazo zilitengenezwa Aprili 2010 huku muda wake wa mwisho wa matumizi ni Novemba 2011 na nyingine ni Januari 2012.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Joseph Mgaya amesema hana habari lakini anaziamini taratibu za manunuzi za taasisi hiyo.

“Ninachoweza kusema hapa ni kwamba siwezi kukupa taarifa yoyote kwa sasa kwa sababu mezani kwangu hakuna taarifa hiyo. Tunafanya manunuzi kwa kufuata taratibu na kuna kitengo kinachohusika,” anasema Mgaya kwa njia ya simu.

Utetezi wa Mgaya hauna tofauti na uliotolewa na maofisa wake mbele ya wabunge. Katika semina hiyo mjini Dodoma. Maofisa hao wa MSD walijitetea kuwa dawa zilizoharibika ni kiwango cha kawaida tu katika mfumo wa biashara duniani kwa viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Maofisa hao walidai pia katika utetezi wao kwamba eti ni mrundikano wa dawa za kuanzia mwaka 2002 hadi 2010. Kwa utetezi huu, maofisa wa MSD hawajuti kiasi kikubwa hicho cha dawa kuharibika, ndiyo maana wamethubutu tena kuagiza dawa ambazo zinatakiwa ziwe zimesambazwa na kutumiwa kabla ya Januari 2012.

Kutokana na miundombinu mibovu na taratibu mbovu za ugawaji na usambazaji dawa mikoani, wilayani na hadi kwenye zahanati vijijini, kiasi kikubwa cha dawa hizo kitaharibika huku wananchi wakifa kutokana na ukosefu wa dawa.

Majibu ya maofisa wa MSD waliyotoa kwa wabunge yanaonyesha hawashtuki dawa kuharibika bila kutumika labda tu ziwe zimevuka viwango vya WHO.

Taratibu za upokeaji dawa zilizowekwa na Bodi ya MSD (Standard Operating Procedures) zinatamka wazi kwamba mali inayotakiwa kupokewa kwenye bohari kutoka kwa mzabuni ni lazima muda wake wa matumizi uwe zaidi ya asilimia 80.

Lakini kwa makusudi kabisa wafanyakazi wa ngazi za chini wanashinikizwa na vigogo wa MSD kupokea hata mali ambayo muda wake wa matumizi uko chini ya asilimia 80.

Maswali

Je, ni hujuma au uzembe? Walioagiza na kupokea dawa hizo wanajua athari ya kuingiza dawa ambazo muda wa matumizi unakaribia kwisha?

Ili kuondoa kiwingu cha hujuma, menejimenti ya MSD inaweza kueleza kwanini wamenunua dawa ambazo wanajua wazi zitakuwa zimeharibika hata kabla ya kusambazwa? Je, wanataka kutumia utetezi uleule kwamba hicho ni kiwango cha kawaida tu katika mfumo wa biashara duniani kwa viwango vya WHO?

MSD itatumia muda gani kusambaza dawa ili zitumike kabla ya kufikia muda wa mwisho wa matumizi? Wanafaidikaje shehena ya dawa ikiharibika na kuteketezwa huku wagonjwa wakihangaika?

Dawa hizi, ambazo baadhi zilitengenezwa kati ya Machi na Agosti 2010, kama ilivyoelezwa hapo juu, zilikuwa wapi kwa kipindi cha karibu mwaka mzima? Kwanini wamekwenda kusafisha maghala ya wafanyabiashara waliochelewa kuuza mapema?

Nani atawajibika kufidia hasara hii ya wazi kama zitabaki bila kutumika hadi ukifika mwisho wa muda wa matumizi yake?

Wakati Watanzania wanakufa vijijini kwa kukosa dawa kwa ukosefu wa watumishi na dawa, kwanini MSD wanafuja mali ya umma kiasi hiki?

Wakati umefika sasa kwamba itumike falsafa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kujivua gamba. Kwamba tuhuma hizi ni nzito kwa menejimenti ya MSD ipime uzito na ikae kando au wahusika na hujuma hii waondolewe na kushtakiwa.

Hakuna haja ya kusubiri ripoti ya Mkakaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu hasara iliyopatikana, wahusika wachukuliwe hatua. Mkurugenzi mkuu apime pia nafasi yake kwamba anataka ipatikane hasara kubwa kiasi gani ndipo awajibike?

0
No votes yet