Vigogo wachafua Daily News


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version

MVUTANO mkubwa umeibuka ndani ya serikali katika kumtafuta mhariri mtendaji mpya wa kampuni ya magazeti yake.

Wakati Bodi ya Wakurugenzi ikiagiza kuchapishwa kwa tangazo la nafasi ya mhariri mtendaji mpya, kiongozi mmoja wa ngazi ya juu ameagiza kung’olewa kwa tangazo hilo dakika chache kabla ya gazeti kuchapishwa.

Taarifa zinasema, tangazo lililong’olewa lilipangwa kuchapishwa mara tatu - Jumamosi iliyopita, Jumatatu na jana Jumanne. Kampuni ya TSN inamiliki na kuchapisha magazeti ya HabariLeo na Daily News.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, magazeti ya serikali hayana mhariri mtendaji baada ya aliyekuwa akishika nafasi hiyo, Isaac Mruma kuondolewa katika kile kilichoitwa, “Kumalizika kwa mkataba wake.”

Tokea Mruma kuondoka katika nafasi hiyo, 11 Mei 2009, nafasi hiyo imekuwa ikikaimiwa na mwandishi wa siku nyingi nchini, Mkumbwa Ally.

Harakati za kutaka tangazo hilo lisichapishwe zilionekana mapema pale baadhi ya maofisa waandamizi wa serikali na Ikulu walipoingia chumba cha habari cha TSN na kutaka wapatiwe tangazo hilo.

“Nakuambia kaka, kuna makubwa serikalini. Tangazo lilishaandaliwa kutoka, lakini ghafla zinakuja taarifa ling’olewe,” kinasema chanzo cha taarifa cha gazeti hili kutoka ndani ya serikali.

Mtoa taarifa anasema, “Hatujui hasa nini kimetokea, maana tangazo lile halijachapishwa tena wakati kuna watu wanataka kujitosa kuomba nafasi hii.”

Chimbuko la hali hiyo imeelezwa kuwa ni mbinu za kumlinda mhariri aliyepo sasa ambaye kwa mujibu wa sifa zilizotajwa katika tangazo hilo, anatupwa nje ya kinyang’anyiro cha kuongoza shirika hilo.

Alipoulizwa mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Wilson Mkama sababu ya kung’olewa kwa tangazo lake, alisema, utaratibu wa kumpata mtendaji wa taasisi ya serikali hauko kama yalivyo magazeti mengine kama “hilo lenu…”.

Alipobanwa kuwa gazeti hili inalo tangazo ambalo ameagiza lichapishwe, Mkama alisema, “ …Hapana, hapana, hapana.”

Alisema, “sikiliza nipo sobre (niko makini). Hatuendi hivyo ndugu yangu,” alisema na kukata simu.

Kwa mujibu wa tangazo sifa za waombaji wa nafasi ya mhariri mtendaji ni kuwa na shahada ya uzamili (Masters degree) ya uandishi wa habari na stashahada ya juu ya utawala au kiwango kinacholingana nayo.

Sifa nyingine ni kuwa na uzoefu wa kazi wa angalau miaka kumi, mitano ikiwa ya kufanya kazi ya ngazi ya juu ya uongozi katika taasisi ya habari yenye hadhi.

Sifa nyingine ni kuwa na mbinu makini za  uongozi, uwezo wa kuzungumza kwa ufasaha lugha ya Kiswahili na Kiingereza, kuwa na stadi za hali ya juu za mawasiliano na kuwa na mbinu nzuri za uongozi.

Tangazo lilitaka wenye sifa hizo kuwasilisha maombi yao kwa mwenyekiti wa bodi; tarehe ya mwisho ya kupokea maombi hayo ni 7 Januari 2011.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani ya TSN, Ikulu na wizara ya habari, mhariri aliyepo sasa amepungukiwa na sifa zilizotajwa, lakini kigogo aliyeagiza tangazo lisitoke, amepanga kumbeba.

“Huyu bwana amezuia hili tangazo ili kupata muda wa kupunguza masharti yaliotajwa katika tangazo la awali, kwani mtu wao hana shahada ya pili iliyotajwa katika lile tangazo. Hata hapa ndani wapo wenye sifa hizo, tena wengine wanawake…,” anaeleza mtoa taarifa wetu.

MwanaHALISI limeelezwa kuwa mmoja wa wafanyakazi wa kike ameapa kujitosa katika kinyang’anyiro cha nafasi hiyo.

Inaelezwa kwamba awali Bodi ya TSN ilipanga kumpata mtendaji wa magazeti hayo kabla ya mkutano wa Bunge wa Februari ili aweze kutambulishwa rasmi kwa wabunge.

0
No votes yet