Vijana CCM wamgeuka Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 23 March 2011

Printer-friendly version
Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa CCm

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), umemgeuka Rais Jakaya Kikwete.

 Unamtuhumu kushindwa kazi. Unamtaka kuachia nafasi ya uongozi katika chama chake ili kuwepo mchakato wa kukiimarisha. 

MwanaHALISI limeelezwa kuwa Baraza la Vijana limeona kuwa Kamati Kuu (CC) ya chama, ambayo huwa chini ya mwenyekiti Kikwete, imeshindwa kusimamia serikali.

Baraza limetaka, pamoja na mambo mengine, Kikwete afanye mabadiliko kwenye muundo wa CC kwa kuwaondoa wajumbe ambao ni mawaziri ikiwa njia ya kukiimarisha chama.

Mapendekezo ya vijana ya kumtaka Kikwete kuachia ngazi katika nafasi ya mwenyekiti, yamepangwa kuwasilishwa kwake mwenyewe Alhamisi wiki hii na viongozi wa umoja huo wakiongozwa na kamanda wao, Kingunge Ngombale Mwiru.  

“Pale Dodoma tulikubaliana kuwa na maamuzi ya aina mbili, ameeleza mjumbe mmoja wa baraza la vijana kwa sharti la kutotajwa gazetini.  

Amesema, “Kwanza ni yale ambayo yatasomwa kwa waandishi wa habari na kufahamika na umma na pili, yale ya siri ambayo tutamkabidhi rais moja kwa moja.”  

Taarifa kutoka ndani ya baraza la vijana lililokutana jijini Dodoma, Jumamosi iliyopita, zinasema uamuzi wa kumtaka Kikwete kuachia nafasi ya mwenyekiti uliibuka wakati wa mjadala juu ya ajenda ya ushiriki wa vijana katika uchaguzi mkuu uliyopita.  

Mjadala uliibuka pale baadhi ya wajumbe walipochangia kwa kudai kuwa matokeo mabaya ya uchaguzi yalitokana na Kikwete kusafiri sana nje ya nchi, jambo ambalo lilimfanya ashindwe kujenga chama chake.  

Mbali na kutaka kutenganisha kofia ya mwenyekiti na ile ya rais, UV-CCM wanaituhumu Usalama wa Taifa kwa kile unachodai “kushindwa kumsaidia rais.”  

“Idara hii imeshindwa kuisaidia serikali. Inashughulika na mambo madogo yanayohusu watu, badala ya kumshauri rais kuhusu mambo makubwa ya kitaifa yaliyo muhimu kwa wananchi,” inasema sehemu ya mapendekezo ya vijana wa CCM ambayo yatapelekwa kwa rais.  

Mapendekezo ya vijana, taarifa zimeeleza, yatawasilishwa kwa Rais Kikwete kesho. Ujumbe utakaowasilisha mapendekezo hayo umetajwa kuongozwa na kamanda wao, Kingunge Ngombale-Mwiru.  

“ Kama usalama wa taifa wangekuwa wanafanya kazi vizuri,” UV-CCM imenukuliwa ikihoji, “wangemweleza rais kuhusu makundi yaliyopo katika chama chake. Lakini badala ya kufanya kazi, wameingia katika siasa za makundi ya ndani ya CCM.”

  Wanasema, “Hawa watu (usalama), wameshindwa kufanya kazi yao kwa weledi…”  

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja huku kukiwa na habari kuwa mnyukano mkubwa uliibuka ndani ya kikao cha baraza la vijana, kati ya makundi mawili – lile linalomuunga mkono Edward Lowassa na ile linalompinga.  

Hoja nyingine inayopelekwa kwa Kikwete inahusu “udhaifu wa mawaziri katika kutimiza kazi zao.” UV-CCM wanadai  mawaziri hawafanyi maamuzi; badala yake wanategeana ili atakayethubutu kufanya maamuzi “aharibikiwe na aonekane mbaya.”  

Umoja huo umesema mawaziri wanapofanya kazi zao wanatekeleza ilani ya uchaguzi ya chama chao, lakini hilo halifanyiki kwa kuwa mawaziri wengi wamejikita katika biashara zao binafsi au wanasaka madaraka ya urais kwa mwaka 2015.  

“Mawaziri hawafanyi kazi kwa sababu hawataki kufanya maamuzi. Matokeo yake rais anaonekana hafai. Hatua ya mawaziri kuacha kufanya maamuzi mazito, imechangia kwa kiasi kikubwa rais  kushambuliwa kila uchao na vyombo vya habari,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.  

Vyanzo vya taarifa vya gazeti hili vinasema, ndani ya baraza la vijana baadhi ya wajumbe walipangwa kutetea baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi.

Mmoja wao (jina tunalo), alinukuliwa akisema kuhusu kashfa ya Richmond na kujiuzulu kwa Lowassa kuwa, “ Kama kuwajibika katika kashfa hiyo, aliyepaswa kuwajibika ni rais mwenyewe aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la mawaziri.”  

Kauli ya mjumbe huyo kumtetea Lowassa ilifuatia mjumbe wa baraza kutoka mkoani Arusha, Mrisho Gumbo kutaka chama chake kuwatosa watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini ambao wanashilikia nafasi katika chama.

 Akichangia katika kikao hicho, Mrisho alisema, “Ukiwa kijana, na ukawa mnafiki, basi ukiwa mzee utakuwa mchawi. Kama tunataka chama hiki kijivue gamba, basi mwambieni Rais Kikwete awaondoe Lowassa, Rostam na Chenge katika vikao vya maamuzi.”  

Alisema, “Naiomba meza kuu; mpelekeeni salamu mwenyekiti. Kama anataka chama kijisafishe awaondoe Lowassa, Rostam na Chenge katika vikao vya maamuzi. Hawa ndio wanaosababisha chama chetu kitukanwe.”

Naye Shy-Rose Banji, akizungumzia matokeo mabaya ya uchaguzi kwa chama chake alisema, “Makamba is the problem (Makamba ndiye tatizo). Tumefika hapa kwa sababu yake kushindwa kazi,” alisema Banji huku akielekeza macho yake kwa Makamba aliyekuwa miongoni mwa wajumbe wa mkutano huo.  

Alisema, “Kila kukicha katibu mkuu anaandikwa kwenye vyombo vya habari, mara hivi, mara vile. Hili ni tatizo kwa chama…”  

Lakini Makamba hakuwa na simile. Haraka aliinuka na kusema, “Shy Rose…mbona wewe unaandikwa sana . Unavaa nguo fupi na una hawara, tena mtu wa CHADEMA…?”  

Alikuwa Edwin Sanda, mjumbe Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kupitia UV-CCM, aliyeingilia kati “mipasho” ya Makamba.  

Alisema, “… katibu mkuu anaingilia mambo binafsi ya watu. Hii si ajenda. Mjumbe amejadili tatizo la chama, linalosababishwa na mtendaji mkuu wa chama, lakini mzee Makamba unakuja kuelezea maisha binafsi ya mjumbe. Hii si sahihi.”  

Naye Husseni Bashe akitetea Makamba na kuhusu madai kuwa uongozi wake ulichangia kufanya vibaya alisema, bunge lililopita pia lina mchango mkubwa sana katika kutofanya vizuri kwa chama chetu kwenye uchaguzi huo.  

Alisema spika wa wakati huo, Samwel Sitta “aliongoza bunge ambalo lilizidisha mpasuko wa wabunge na hatimaye wana-CCM wote katika kipindi cha kuelekea uchaguzi.”  

Alitoa mfano wa kashfa ya mkataba tata wa Richmond iliyosababisha kujiuzulu kwa Edward Lowassa katika nafasi yake ya uwaziri mkuu.  

Bashe alidai ndani ya kikao kuwa ana ripoti mbili za Richmond , lakini zikizungumzia jambo moja, huku zikiwa na maudhui tofauti.  

Alisema, “Jamani watu hapa wanazungumzia habari ya Richmond , ukweli mimi ninaujua…Hii ilikuwa ni chuki binafsi kati ya Sitta na Dk. Mwakyembe dhidi ya Lowassa.”  

Kuhusu udhaifu wa Makamba, Bashe alisema, “Makamba hajajiteua. Ameteuliwa. Kama kuna makosa, basi aliyemteua ndiye awajibike” – bila shaka Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete.  

Kwa upande wake, Ridhiwani Kikwete aliasa wajumbe kujadili hoja, akisema “wenzetu wa CHADEMA wana mikakati ya kufanya vitu vyao na wana uwezo wa kuitekeleza.” Hata hivyo, hakuna aliyejali rai yake.  

Mtetezi mashuhuri wa Lowassa, James Millya alisema, “Chama hiki kinavurugwa na Sitta na Dk. Mwakyembe kwa kueneza vitu vya uwongo dhidi ya Lowassa.”  

Katika hatua nyingine UV-CCM wamemtaka Kikwete kuagiza Makamba kumfukuza Tambwe Hiza kutoka idara ya porapaganda ya chama hicho kwa kuwa “ameshindwa kazi.”

0
Your rating: None Average: 3.8 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: