Vijana wasema udini, ukabaila vimo CCM


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umebaini kuwepo ukabila na udini katika chama hicho.

Ukabila na udini vilitumika zaidi wakati wa kura za maoni ndani ya chama na ni baadhi ya sababu zinazokifanya chama hicho kupotea njia yake ya asili.

Sababu nyingine, ni udhaifu wa serikali wa kushindwa “kuchukulia hatua watendaji wake na baadhi ya viongozi waliojigeuza “miungu watu.”

Hayo yamo katika kile kinachoitwa, “Ripoti ya zoezi la kampeni za vijana wa CCM – Taifa,” waliojipa kazi ya kutafuta chanzo cha mpasuko ndani ya chama.

Wakati haya yakiibuka, Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete anazunguka nchi nzina akitoa taarifa zilizoelezwa kuwa za “kiini macho” kwamba wanaohubiri udini na ukabila waepukwe.

Ripoti ya vijana iliandaliwa mara baada ya ziara ya viongozi wakuu wa Umoja wa Vijana (UV-CCM), katika mikoa kadhaa nchini, kati ya 1 Septemba na 27 mwaka huu.

Imelenga kukipatia “CCM ushindi katika ngazi zote tatu za uchaguzi – rais, wabunge na madiwani na kutafuta chanzo cha CCM kuonekana hakikubaliki mbele ya wananchi katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.”

Aliyeongoza ujumbe wa vijana ni Makamu Mwenyekiti wa UV-CCM, Beno Malisa. Aliongozana na wale wanaoitwa, “makada na viongozi wanne kutoka makao makuu ya vijana,” ambao ni Mohameid Seif Malinda, Mboni Mhita, Angela Mwanri na Salum Masoud.

Ripoti inasema tatizo la makundi lipo katika kila eneo, kuanzia ngazi ya ubunge hadi udiwani.

Mfano hai ni mkoani Iringa ambako Frederick Mwakalebela anatuhumiwa kuhujumu kampeni za Monica Mbega.

Naye, mwenyekiti wa UV-CCM wilaya ya Iringa Mjini, anatuhumiwa kuhujumu chama.

Mkoani Tabora, mikutano ya mikakati ya ushindi ilifanyika kati ya 17 na 18 Septemba katika ukumbi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Nako ni tuhuma juu ya tuhuma.

Kama ilivyokuwa mkoani Iringa, kiini cha makundi, ni kura za maoni na jumuiya za chama kushindwa kufanya vikao vyake kwa mujibu wa katiba.

Mkoani Tabora, makundi makubwa yapo katika majimbo ya Urambo Mashariki na Urambo Magharibi.

Kwanza, taarifa inaeleza, “Mgombea ubunge katika jimbo la Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya, haungwi mkono katika kata ya Ulyankulu.”

Kisa: Ni mwenyekiti wa wilaya wa chama hicho, “kumpiga marufuku” kukanyaga Ulyankulu kuomba kura. Mwenyekiti huyo, taarifa ya vijana inasema, “anapata nguvu ya kuchochea mgongano kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta.”

Sitta na Kapuya, inaelezwa kuwa wamekuwa katika msuguano wa muda mrefu uliozidisha ufa ndani ya chama.

Hapa ndipo hata siri ya rais Kikwete kuongeza mikoa mipya, jambo ambalo limeongeza ukubwa wa serikali, ilipoibukia.

Ripoti inasema, “…ni vema juhudi za muda mrefu zikafanyika ili (kumaliza) mgogoro huu wa siku nyingi. Kugawa upande mmoja kwenda mkoa mwingine ni suluhisho namba moja, na kwamba huenda ikawa ni njia sahihi.”

Hata vyombo vya dola viliingizwa katika mgogoro ambapo askari polisi wa Kaliua, mkoani Tabora wanatuhumiwa kupendelea vyama vya upinzani hasa pale panapotokea vurugu.

Je, nini kifanyike? Kwanza, Malisa anasema, CCM wahamasishe vijana wao “kwa nguvu moja na ari moja, kuingia kambini ili kujijenga kimwili katika kipindi hiki cha kampeni ili kujibu mapigo ya wapinzani.”

Vijana wanaotajwa ni wale wa kundi la “Green Guard.” Kila kijana, kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa ndani ya chama, analipwa Sh.1,000 (elfu moja) kwa siku, kiasi ambacho wanasema, “pamoja na kufanya kazi ngumu, ni kidogo.”

Kwa kauli hii, sasa imethibitika kuwa vurugu zinazotokea katika maeneo mbalimbali ya nchi, chanzo chake ni makundi haya ya CCM.

Hata Profesa Kapuya ameeleza katika taarifa yake mbele ya “makada,” kwamba “vijana wa CCM ni legelege, na mara kwa mara wanaonewa na wapinzani.” Kwa mujibu wa ripoti, wanatakiwa wajibu mapigo hata kabla ya kuchokozwa.

Mkoani Kigoma, baadhi ya matatizo yaliyojitokeza, ni mahusiano mabaya kati ya mbia aliyeleta vifaa vya chama kutoka Dar es Salaam, kama vile baiskeli na pikipiki na viongozi wa CCM mkoani humo.

Hadi ujumbe wa makada walipofika Kigoma, mbia aliyevisafirisha vifaa hivyo alikuwa hajalipwa fedha zake. Ni Peter Serukamba aliyeahidi kulipa. Haifahamiki kama ameweza kutimiza ahadi hiyo.

Hapa ndipo pia liliibuka suala la udini. Mwenyekiti wa vijana wilaya ya Kigoma Mjini alinukuliwa akisema hadharani, “Siwezi kushiriki katika mapokezi ya makafiri.” Alikuwa anamaanisha Malisa na ujumbe wake.

Jingine ambalo lilijitokeza katika kila mkoa, ni vipi ilani ya CCM kushindwa kueleza itakavyoweza kumaliza tatizo la ajira, elimu na ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Mengi yaliibuka katika wilaya ya Kasulu katika mkutano uliofanyika 19 na 20 Septemba. Tatizo kubwa lilikuwa kutofanyika kwa kambi za vijana – Green Gard.
Viongozi kutoka makao makuu waliagiza wagombea ubunge watatu wanaotoka katika wilaya ya Kasulu wagharamie makambi ya Green Guard – angalau siku mbili kabla ya uchaguzi.

Lengo ni kundaa vijana na matokeo ya uchanguzi. Hata hivyo, haijafahamika makundi hayo yameagizwa kufanya nini hasa. Bali, imeelezwa kuwa watakaa wakisubiri amri kutoka kwa viongozi wao.

Katika wilaya ya Kibondo, taarifa inaonyesha kuna mahusiano yasiyoridhisha kati ya umoja wa vijana wilaya na uongozi wa CCM wilayani humo.

Ni kutokana na mahusiano hayo mabaya, vijana wa Gree Guard walishindwa kufundishwa kwa wakati. Malisa na wenzake waliamuru ifanywe kazi hiyo mara moja ili kujiandaa kwa uchaguzi.

Wilayani Biharamulo, mkoani Kagera, kwa jumla hali ya kisiasa ilikuwa shwari na matumaini ya CCM kupata ushindi yalikuwa makubwa.

Hata hivyo, taarifa inamtishia mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya kwa madai kuwa anakipinga chama hicho. Hata baadhi ya walimu wanatajwa kuwa wanapinga CCM katika maeneo yao ya kazi.

Tatizo la ukabila nalo linatajwa kuwa alimegawa wanachama wa CCM katika makundi mbalimbali wilayani Biharamulo.

Mgombea wa ubunge wa Biharamulo, Oscar Rwegasira Mukasa ambaye ni kutoka kabila la Wahanga ni mhanga katika hili.

Viongozi wa wilaya na baadhi ya wanachama, ambao ni Wasubi ambao ni wengi, hawataki kumuunga mkono.

Katibu wa vijana wilayani, naye ametuhumiwa kuendeleza makundi. Wanataka mara baada ya uchaguzi afukuzwe kazi.

Katika wilaya ya Ngara, changamoto ilikuwa kukosekana kwa mgombea ubunge wakati ujumbe unafika wilayani humo. Mgombea ubunge wa jimbo hilo, Deogratias Ntukamazina alikuwa nchini India kwa ajili ya matibabu.

Ilibidi mkewe kupanda jukwaani kumuombea kura ili kuondoa hofu kwa wapigakura.

Katika wilaya ya Karangwe, kikao kilichofanyika 25 Septemba, pamoja na mambo mengine, kilionyesha kushamiri kwa makundi kutokana na mchakato wa kura za maoni.

Wilayani Bukoba Mjini, mkutano uliofanyika 25 Septemba, Hamgembe. Wakati huo, mvutano unaotokana na kiti cha umeya ulikuwa unafukuta.

Jimboni Misenyi, wagombea ambao wameshindwa katika kura za maoni walikuwa wamegoma kupanda jukwaani kuunga mkono mgombea aliyepitishwa na chama. Sababu ni majigambo ya mshindi wa kura za maoni dhidi ya walioshindwa.

Kata ya Buselesele ni moja ya kata ambazo kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita imetawaliwa na upinzani.

Malisa anasema katika andishi lake, “…safari hii vijana wakiongozwa na katibu wao wa jumiya wa wilaya wamesema wako imara na kwa vyovyote vile, watarejesha kata hiyo mikononi mwa CCM.”

Taarifa inaeleza tatizo kubwa lililopo mkoani Kagera, ni vita vya kuwania uenyekiti wa halmashauri ambapo madiwani wa CCM wamekuwa wakihujumiana wenyewe kwa wenyewe.

Mkoani Mwanza, taarifa ya UV-CCM inasema hali ni tata. Katika jimbo la Magu mahusiano si mazuri kati ya UV-CCM na mgombea ubunge aliyepitishwa na chama hicho, kuwania nafasi hiyo.

Ni hali hiyo iliyofanya baadhi ya vijana, akiwamo mwenyekiti wa UV-CCM mkoani Mwanza, kugoma kushiriki katika kampeni.

Hapa kuna jingine ambalo limejitokeza na ambalo hata taarifa imelitaja. Linahusu mgombea aliyepitishwa kutoa maneno ya kashfa kwa wenzake kwa kuwaita “pumba” na yeye “ni mchele safi.”

Pamoja na majigambo na ushauri kadhaa, taarifa ya UV- CCM imempa nasafi finyu ya kushinda.

Katika jimbo la Nyamagana, wameingizwa hata wasiokuwamo. Kwa mfano, Lawarance Masha, ambaye anaonekana kamba iko hatarini kumkatikia, anashika uchawi Anthony Diallo, kwamba anamhujumu.

Hili linachochewa na taarifa ya Malisa inayosema, mpinzani wa Masha, Ezekia Wenje (CHADEMA), alirejeshwa katika kinyang’anyiro hicho kwa nguvu ya Diallo.

Lakini kila mmoja anajua kuwa aliyesimama imara kurejesha Wenje katika kinyang’anyiro hicho, ni wakili mashuhuri nchini, Mabere Marando, ambaye alisimamia rufaa ya Wenje na kuelekeza hata jinsi ya kuiandika.

Jingine ambalo limesababisha hali ya Masha kuwa ngumu ni hatua yake ya kuzima simu zake mara baada ya kubebwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Nyamagana, Wilson Kabwe, jambo ambalo lilimjengea chuki na wananchi na baadhi ya wagombea wa udiwani.

Lakini Malisa na wenzake wanasema katika taarifa yao, “…mgombea ubunge katika jimbo la Ilemela, Anthony Diallo, ni sehemu ya tatizo linaloikumba Nyamagana. Diallo amechangia kwa kiasi kikubwa kuondolewa kwa pingamizi za Wenje…”

Wanapendekeza kwamba ni lazima Diallo aonywe na asipewe nafasi yeyote ya uwaziri katika serikali itakayokuja.

Kasoro pekee ambayo ripoti imeitaja kuhusu Masha, ni kutumia nafasi yake ya uwaziri na ubunge kutimiza matakwa yake binafsi, badala ya kuwatumikia wanachi.

Katika mkoa wa Mara, hasa jimbo la Musoma Mjini, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Vedatus Mathayo yuko hoi. Ni kwa sababu, ana mahusiano yasiyoridhisha na wapigakura, hasa vijana.

Hali ni hivyo katika mikoa mingine, kama vile Kilimanjaro, Ruvuma, Mtwara, Arusha, Manyara na Dar es Salaam. Kila mahali ni makundi.

Ugumu wa kuvunja makundi unatajwa kutokana na hatua ya mtendaji mkuu wa chama, Yusuf Makamba kuvuruga zoezi zima la kura za maoni kwa kukaidi agizo la mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutaka wapigakura za maoni kuwa wanachama wenye kadi.

Siku mbili kabla ya kura za maoni, Makamba alikaidi agizo la NEC kwa kuagiza kila mwanachama kuruhusiwa kupigakura.

Matokeo yake, zoezi la kura za maoni katika maeneo mengi liliendeshwa kwa ubabe, matusi na kuchafuana.

Hadi mwisho wa mchakato, wagombea walikuwa na dhana ya “ama zangu ama zako.”

Ni wazi kuwa uchaguzi unapokuwa wa rafu kiasi hiki, hakuna uwezekano wa watu wale waliovuana nguo kuungana mkono kwa moyo katika uchaguzi mkuu. Labda kama walichokuwa wanakitetea kilikuwa ni matumbo yao.

Lakini kikubwa kinachoonekana kuwa fundisho katika taarifa hii ya UV-CCM, ni kuwa kama wenyewe wameumbuana kiasi hiki, nani anaweza kusalimika? Nani anaweza kusema CCM inaendesha kampeni za kistaraabu?

Kama wameweza kutuhumiana, wenyewe kwa wenyewe, kushambuliana hadi kujenga uhasama wa muda mrefu na kuibiana kura, hali itakuwaje wanapokuwa katika ushindani na upinzani?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: